WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, June 24, 2013

Uchambuzi Wa Habari; Mwigulu, Msigwa Na Hamu Ya Vurugu Mechi!

9 4d716

Ndugu zangu,

Leo jijini  Dar wanakutana wanahabari na wadau wa habari zaidi ya 150. Watajadili maadili na wajibu wa wanahabari kwenye hali ya migogoro. Watachambua pia hatari ya lugha za chuki, udini na mengineyo. Wataangalia pia  namna njema  ya kukabiliana  na hali hizo.

Ni hatua njema kabisa na imekuja wakati muafaka. Na hapa nawasifu MCT kwa kufanikiwa kuwakutanisha wanahabari katika hili. Kila la kheri.

Na kwenye hili la wanahabari na migogoro tunaweza kuona mfano wa moja ya habari kubwa jana Jumapili; Iliwahusu Wabunge Mwigulu Nchemba ( CCM)  na Peter Msigwa ( CHADEMA)

Hakika niliamka nikisikia vichwa vya habari vya uhasama vikitamkwa

redioni. Kisha  nikajionea mwenyewe nilipoyanunua magazeti kadhaa ya jana.

Naam; “ Mwigulu  na Msigwa nusura wazichape!”. Mengi ya magazeti yalibeba habari hiyo katika staili ya kufanana- Waheshimiwa nusura wachapane! Na picha kubwa ya waheshimiwa hao ikawekwa mbele kwenye magazeti hayo.

Kabla hata sijaisoma habari yenyewe, nilipoangalia picha tu,  nikajiuliza; hivi walio kwenye nusura ya kuchapana makonde ndio hawa?!

Picha tu ilijieleza, kuwa Msigwa na Mwigulu ni watu wenye kufahamiana na pengine hukutana kunywa kahawa pamoja. Kwamba pale, na kwa mujibu wa habari yenyewe, walikuwa kwenye mabishano ya hoja. Ni kawaida. Maana, sikuona hata mahali wametukanana.

Masikini Msigwa na Mwigulu, hawa ni watu wazima na familia zao. Fikiri mtoto wa mheshimiwa anaambiwa na mwenzake shuleni; “ Eeh, nimesikia baba yako anataka kuzichapa na mwenzake huko bungeni!” Ni mambo ya kudhalilisha kwa kweli, si kwa familia tu. Hata kwa Mheshimiwa kwa wapiga kura wake. Naam, Waheshimiwa wakianza kuchapana makonde hadharani badala ya kuzungumza wanaacha kuwa waheshimiwa. Wanabaki kuwa wahuni tu, kama wale wa mitaani.

Na hapa ndipo tunauona udhaifu wetu wanahabari, kuwa tunapenda sana kushabikia ‘vurugu mechi’. Maana,  utotoni tulipokuwa tukenda viwanjani, moja ya burudani tuliyoona ni ya kufurahisha ni pale ilipotokea ‘ vurugu mechi!’ Kwamba hapo rafu mtindo mmoja na kinachofuatia refa kukimbia mwenyewe au kukimbizwa kwa fito.

Naziona dalili za media yetu kuanza hulka ya kushabikia ‘ vurugu mechi’ badala ya mambo ya msingi. Ona jana, wabunge wale wapambanaji wa UKIMWI waliudhuria semina ya UKIMWI. Lakini, kilichoongewa na wabunge hao kuhusu UKIMWI hatukukisikia hata kimoja!

Hivyo, wakati wanahabari wakikusanyika hii leo pale Dar kujadili maadili ya kazi zao na wajibu wao kwenye migogoro waiangalie pia mifano kama ya jana kwenye media. Maana, badala ya media kuchangia kwenye kupunguza tension na migogoro, inaweza kuchangia kwenye kuichochea! Na hilo si jukumu la media yenye kuwajibika  na kuzingatia uzalendo.

Maggid Mjengwa,
Iringa.
0754 678 252

No comments:

Post a Comment