WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, June 16, 2013

Mwinyi asisitiza ushindani uzingatie nguvu ya sera

 
Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi.

Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, amesema demokrasia ya vyama vingi ni lazima ikwepe chuki, uhasama na badala yake ihimize ushindani wa nguvu ya sera kutokana na ushawishi wa kisera bila ya kumwaga damu nchini.

Mzee Mwinyi alitoa matamshi hayo jana wakati akifunga rasmi kampeni za CCM katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mapape, Mkoa Kusini Pemba.

Alisema mwanasiasa ambaye si mufilisi wa hoja hawezi kutamani na kuutumia mfumo huo kinyume na misingi ya upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa hivyo ni lazima jamii ianze kuwaepuka na kuwa na tahadhari na wanasiasa wa aina hiyo.

Akihutubia mamia ya wananchi, Mzee Mwinyi alisisitiza kuwa enzi ya utawala wake ndipo mfumo wa vyama vingi ulipoingia na kwamba hakuelekeza uwe mfumo wa mapigano, uhasama na chuki bali serikali yake ilikusudia kuwapo ushindani wa sera na nguvu ya hoja.

Aidha, alisema demokrasia ya vyama vingi isipotoshwe na wanasiasa ili kuibadili Tanzania kuwa uwanja wa mapigano na machafuko na badala yake akasema kila chama cha siasa kitambue kina wajibu na ulazima wa kuheshimu sheria za nchi.

Alisema si haki litokee kundi moja kulizungumzia jingine na badala yake kila mtu apate fursa ya kutoa mawazo yake ipi ni namna bora itakayoliongoza Taifa kwa misingi ya usawa, haki na demokaria ya kweli.
Akimnadi mgombea wa CCM jimbo la Chambani Mattar Sarahan Said aliwataka wananchi wa jimbo hilo kumchagua mgombea huyo kwa kuwa anatokana katika chama kinachofuata miiko, umoja na kwamba mgombea huyo ni bora kuliko wa vyama vingine vya siasa.

“Nimekuja kwa unyenyekevu na staha , kila mmoja atambue hilo , umoja siku zote si shari bali ni hiari ya mtu binafsi, msikubali kuitupa fanaka ya ustawi wa Taifa letu la sasa na lijalo ” alisisitiza Mzee Mwinyi.

Aliwataka wananchi wa jimbo la Chumbani kumchagua kwa kura nyingi Mattar ili awe mbunge wao kwasababu ni kijana hodari na mwepesi katika kupambanua mambo mema na kukataa mabaya.
Wagombea wa ubunge katika uchaguzi mdogo jimbo la Chambani kisiwani Pemba ni pamoja na Mattar (CCM), Said Miraji Abdallah (ADC), Yussuf Salum Hussein (CUF) na Sitti Usi Shaib (Chadema).
 
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment