WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, June 5, 2013

Lipumba amepoteza hadhi ya kuwa Mwenyekiti CUF

WAKATI mwingine unafikiria vitu vimefika pabaya; halafu vinaharibika kabisa! Ni sawa sawa na uone gari lako linapasuka tairi na unajitahidi kwa ufundi wote kuliegesha pembeni na unajua hili ni baya lakini unashukuru Mungu kuwa angalau ni tairi tu utabadilisha.

Unapoegesha gari na kuanza kutoa tairi la akiba na jeki kabla hujatulia rejeta ya gari inaanza kuchemka na moto unalipuka kwenye injini na kabla hujafanya lolote moto unalipuka na kuanza kuteketeza gari lako.
Ukiwa umekaa chini unasikitika maana hata kujaribu kuzima huna nafasi simu yako inaita na unaambiwa mtoto wako kagongwa na gari amekimbizwa hospitali! Kwenye Kiingereza wanasema when you think things are bad, they get worse!

Suala la udini Tanzania tumelizungumza na kufika mahali kujua kuwa tuko pabaya. Tumeshuhudia kauli za ajabu na za kichochezi, hadi tumefika tunagombea nani achinje na nani asichinje huku wengine wakitaka Mahakama ya Kadhi iingizwe kwenye Katiba na wengine wakipinga. Wakati hatujatulia tunaona video za kina Ilunga na wengine wakichochea mauaji ya viongozi na waumini wa Kikristu.

Tukiwa bado tunatafakari hayo na tukiwa hatujatulia katika suala la kuchinja na masuala mengine yenye harufu zote udini, Profesa Ibrahim Lipumba mmoja wasomi mashuhuri wa Tanzania akaja na lake jipya.
Akizungumza kwenye Msikiti wa Idrissa Kariakoo jijini Dar es Salaam, Prof. Lipumba amesikika akisema kuwa chama chake kilifanya kampeni ya kidini ili kumsaidia Rais Jakaya Kikwete – Muislamu mwenzao ili asije akaangushwa. Bila kumung’unya maneno Prof. Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (Wakiislamu?) amesema kuwa pamoja na kuwa uchaguzi wa 2010 kutokuwa huru na wa haki yeye na wenzie ilibidi watumie mbinu za ziada ili kuokoa “jahazi”.

Pamoja na kauli hiyo Prof. Lipumba ameonekana akiwagawa Watanzania kwa misingi ya kidini upande mmoja wakiwepo Waislamu ambao licha ya kumsaidia Kikwete kuupata urais hawakupata matunda yoyote hadi hivi sasa na upande wa pili ni “wenzetu” ambao ni wazi akimaanisha ni Wakristu. Prof. Lipumba akizungumzia hili amesema kuwa “Kwa hiyo kama Waislamu tunataka kupata haki zetu, kama tunataka kuishi kama raia wa daraja la kwanza katika nchi yetu, lazima tujipange kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015; na sisi tuanze kujipanga kwa sababu wenzetu wameanza kujipanga, vinginevyo tutaendelea kubaki masikini na raia wa daraja la nne katika nchi yetu wenyewe”

Prof. Lipumba amesema mengi sana kwenye hadhara ile kiasi kwamba maswali makini yanahitaji kuulizwa ama kuhusu usomi wake na hekima ambayo watu walitarajia kuwa nayo au amesema vile kwa sababu anajua sasa hivi njia ya kutokea ni hii ya udini. Kwa mtu ambaye ametumikia serikali (kama mshauri wa Rais) na kama mmoja wa wasomi kauli zake ambazo nyingi zinaonesha dalili ya ujinga (siyo tusi) ni wazi ile imani ambayo watu walikuwa nayo kuwa Prof. Lipumba ni msomi inabidi kuangaliwa upya.

Ni usomi gani unaoweza kumfanya mtu kuwa mbaguzi wa wazi ambaye anaiangalia jamii anayotaka kuiongoza kwa misingi ya “sisi dhidi ya wao”? Hivi alipogombea urais mara nne alikuwa anataka kuwa Rais wa Waislamu ili awape Waislamu maendeleo? Wakristu na wale wasio na imani hizi mbili wangeishi vipi katika Tanzania chini ya Lipumba ambaye Sheikh Basaleh akimtambulisha alimtambulisha kama “Rais mtarajiwa”? Kweli Wakristu wanaweza kuwa salama chini ya mtu kama Lipumba?

Lakini pia inabidi twende mbali zaidi na kuhoji kama Lipumba anaweza “kuweka imani yake mbele” kama alivyopongezwa na Sheikh Basaleh mara baada ya Uchaguzi Mkuu (kwa kauli yake mwenyewe) je, anaweza kukiongoza chama cha siasa ambacho ni cha kitaifa ambamo ndani yake wamo Wakristu? Je, inawezekana ndani ya CUF Mwenyekiti Lipumba na Katibu Mkuu Maalim Seif (wote Waislamu) Wakristu wanaweza kuwa na haki yoyote sawa au wanaonekana kama watu ambao wanachukuliwa kama ishara tu ya kitaifa lakini chama kwa kweli ni cha Waislamu chenye kupigania harakati za Waislamu?

Sasa binafsi sina tatizo kabisa na Lipumba kama Muislamu kuzungumzia mambo ya Uislamu – kwangu haijalishi sana; lakini shida inakuja kuwa kiongozi wa umma anaposimama na kuzungumza lugha ya kuligawa taifa jinsi alivyofanya Lipumba kweli anaweza kuaminika? Inawezekana ni kweli Watanzania walitambua huu mwelekeo wa Lipumba ndio maana walimkataa mara nne na tena mara ya nne walimkataa vibaya zaidi?

Lakini swali ambalo linabakia ni jinsi gani Lipumba anaweza kuendelea kuwa mwenyekiti wa chama cha siasa wakati Mwenyekiti wake anapigania maslahi ya kidini kwa kupitia chama chake akithibitisha kuwa CUF ilifanya hivyo mwaka 2010? Sheria ya vyama vya siasa inakataza kabisa vyama kuundwa kwa maslahi ya kupigania dini au maslahi ya kidini. Kwamba CUF kimefanya hivi na Lipumba amethibitisha swali kubwa linabakia – Je, Msajili wa Vyama vya Siasa ana ujasiri wa kufanya lolote?

Kama Lwakatare kwa maneno ya video ameweza kushtakiwa na kunyimwa dhamana kwa sababu ameoneka na akipanga njama – wengine walisema ugaidi – je, Lipumba ambaye ameonekana akithibitisha kuwa chama chake ni chama cha kupigania haki za Waislamu na hili liko wazi kwenye video na yeye mwenyewe hajakanusha je, John Tendwa ana uwezo wa kusema lolote au ataumauma maneno ya kutaka “kuletewa malalamiko rasmi”?

Ninapoacha maswali haya na mengine nabakia kujiuliza tunafikiri tumefika pabaya je, inaweza kuwa mbaya zaidi ya hivi? Muda utajibu

source: raia mwema: Lula wa Ndali Mwananzela

No comments:

Post a Comment