WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, November 13, 2012

WALIOFICHA MABILIONI YA FEDHA USWISI NI KIELELEZO CHA WATU WASIOJALI UZALENDO


Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema).
NIMSHUKURU Mungu kwa kuniwezesha leo kuwa na wazo la kuzungumzia mustakabali wa nchi yetu ambayo baadhi ya watu wanataka kuifanya mali yao binafsi. Mungu awape moyo wa huruma.
Baada ya kusema haya nikumbushe tu kwamba wiki iliyopita tulishuhudia mjadala mkali ukiibuka bungeni baada ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema) kuwalipua baadhi ya viongozi wa serikali, wafanyabiashara na watu wengine ambao hakuwataja akitaka wachunguzwe kwa makosa ya kuficha mabilioni ya fedha nje ya nchi.
Mbunge huyo kijana alitoa kauli hiyo bungeni wakati akiwasilisha hoja yake binafsi akilitaka Bunge kuchunguza na kuielekeza serikali kuchukua hatua dhidi ya watu hao wanaojifanya wenzetu walioficha fedha na mali haramu nje ya nchi.
Zitto aligusia kuwa watu hao kwa nyadhifa ni wale walioshika nyadhifa za uwaziri mkuu katika kipindi cha 2003 hadi 2010, walioshika nyadhifa za uwaziri wa nishati na madini katika kipindi hicho na waliokuwa makatibu wakuu wa Wizara ya Nishati na Madini.
Wengine ni mawaziri na makatibu wakuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, wakuu wa majeshi, wanasheria wa serikali, makamishna wa nishati, walioshika wadhifa wa Ukurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Uenyekiti na Ujumbe wa Bodi wa TPDC katika kipindi cha mwaka 2003 hadi 2010.
Kutokana na hilo, Zitto aliitaka Serikali kupeleka muswada wa sheria bungeni wakati wa Mkutano wa 11 wa Bunge wa Aprili mwakani.
Hakuishia hapo, alipendekeza kuwa iwe ni marufuku kwa kiongozi yeyote wa umma, mume au mke wake au mtoto wake kuwa na akaunti nje ya nchi isipokuwa kwa sababu maalumu na kwa kibali rasmi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Alitoa ushauri kwa serikali kwamba iwasiliane na Benki ya Dunia kupitia kitengo cha ‘Assets Recovery Unit’ ili mabilioni ya fedha na mali ambazo zimetoroshwa nje ya nchi kwenda Uswisi, Dubai, Mauritus na maeneo mengine ziweze kurejeshwa nchini.
Aliwataka Watanzania wote wenye akaunti za fedha nje ya nchi waeleze wamezipata wapi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wachukue hatua za kisheria dhidi ya watu wote wanaomiliki fedha hizo kinyume cha sheria.
Zitto alisema katika Mkutano wa Bunge la 11 na baada ya taarifa ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu raia wa Tanzania wenye kumiliki fedha za kigeni kwenye benki na mali nje ya Tanzania, ilete taarifa ya hatua ilizochukua ili kuziba mianya ya utoroshaji wa fedha nje ya nchi.
Zitto alisema Benki Kuu ya Uswisi ilitangaza kuwa jumla ya dola za Marekani 196 milioni zilikuwa zimehifadhiwa kwenye akaunti za benki za nchi hiyo.
Akaongeza kuwa pamoja na Mkurugenzi wa Takukuru, Dk. Edward Hosea kukaririwa akisema kuwa ataiandikia serikali ya Uswisi barua kuomba kurejeshwa kwa fedha hizo , lakini mpaka sasa hakuna hatua zilizochukuliwa.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema alisema serikali imeanza kuzifanyia uchunguzi tuhuma hizo lakini tulio wengi tunajiuliza, serikali hii kwa nini imechelewa kujua na kuchukua hatua? Hakuna vyombo vya kubaini aliyobaini Zitto?
Nilisikiliza bunge siku ile Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka alisema hata kama ni rais aliyeko madarakani au waziri mkuu ama kiongozi yeyote atajwe bungeni ili Bunge limwondolee kinga aburutwe mahakamani, ninachosema mimi ni kwamba kutajwa siyo hoja, kinachotakiwa ni kuthibitisha tuhuma, hivyo hoja ya Zito ya kuundwa kamati au tume ni jambo la msingi sana.
Lakini Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliwataja marehemu Daudi Balali, Andrew Chenge na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Gray Mgonja kwamba walihusika na tuhuma za ufisadi wa Tan Gold hivyo Bunge linapaswa kuchukua hatua. Si fahari kwa serikali kuwa na watendaji ambao siyo waaminifu, sasa wanaomlazimisha Zitto awataje wahusika wana hoja dhaifu sana.
Kama amesema wizi ulipitia Kampuni ya Meremeta, Tan Gold, Epa na kadhalika kuna ugumu gani kuanzia kwenye makampuni hayo na mabenki aliyoyataja? Wanaotoa hoja hiyo dhaifu hawajui kuwa makampuni au mabenki kulikuwa na viongozi? Wahojiwe hao na wezi watapatikana.
Wapo Watanzania wanaotoa fedha nyingi kwenye uchaguzi na kutoa misaada mbalimbali kiasi cha kuiharibu nchi, hao peke yake wanatosha kutiliwa shaka hasa kama wanatajwatajwa kwenye ufisadi, kwa nini wasichunguzwe?
Tulishuhudia Bunge la Tisa yalipozuka masuala ya Dowans, Richmond na Epa, wabunge waliposimama imara, viongozi wa serikali walitia vikwazo kuzuia mjadala.
Kama alivyoonya Ole Sendeka, watu wote wanaojineemesha kwa fedha za umma watambue kwamba wanafanya dhambi kubwa ambayo kila raia wakiwemo wabunge wataathirika siku za usoni na hakika ni hatari kwa usalama wa taifa.
Tusikubali kabisa wezi hao kuwaachia kwani watu hao walioficha mabilioni ya fedha Uswisi ni kielelezo chao cha kutojali wenzao, hawana uzalendo.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

source vijimambo blog

No comments:

Post a Comment