WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, November 24, 2012

Neno Fupi La Usiku Huu: Ng'ombe Hanenepi Siku Ya Mnada...!


Ndugu zangu, 

Kila jambo linahitaji maandalizi. Kuna kisa cha mbweha na mbwa mwitu. Mbweha alishangaa sana kumwona mbwa mwitu  akiwa na mazoea ya kunoa meno yake hata kama haendi mawindoni. 

Mbweha akamwuliza mbwitu; " Iweje unahangaika kunoa meno yako wakati hutayatumia kuwindia kwa muda huu?"

Mbwa mwitu akajibu: " Kama nitasubiri kunoa meno yangu mpaka siku ya kuwinda ifike, basi, nitashindwa hata kukabiliana na ninayemwinda!"

Naam, ni wachache sana humu duniani waliofuzu mitihani migumu bila maandalizi. Aliyejiandaa vema hupata wepesi katika afanyalo. Tumekuwa tu wavivu sana wa kufanya maandalizi kwa tuyafanyayo. 

Hatuna mipango. Wengi wetu tumekuwa tu watu wa kukurupuka asubuhi na kuitazama siku kama ilivyokuja. Tupo tupo tu. Unakutana na mtu mtaani atakwambia; ” Nashuka chini kidogo”. 

Yawezekana kabisa huko chini hajui anakwenda kufanya nini. Ukikutana nae tena baadae atakwambia; ” Napandisha juu kidogo”. Usimwulize huko juu anakopandisha anakwenda kufanya nini. 

Ndio maana ukisikia kelele ya kibaka mtaani, ghafla watatokea watu kutoka kila kona kumfukuza kibaka huyo. Wengi wa watu hao hawana mipango ya kuifuata katika siku hiyo. Kelele za mwizi huyoo zimewapa kazi ya kufanya. 

Ndio, hatuna mazoea ya kufanya maandalizi. Utamkuta  Kijana wa Kitanzania  amemaliza kidato cha sita au Chuo Kikuu. Hajiweki katika hali ya siku moja anaweza akaitwa kusailiwa kwa nafasi ya kazi. Na ikifika siku hiyo ya kuitwa kwenda kufanya intavyuu, basi, hatolala usiku. Atakesha akijiandaa kwa intavyuu. Kesho yake ataingia kwenye chumba cha usaili akiwa amechoka sana. Yumkini atashindwa.

Ni kama  mwenye ng’ombe,  ambaye siku ya mnada, ndipo anapokumbuka kumlisha majani ng’ombe wake aliyekonda ili apate bei nzuri mnadani. 

Naam, ng’ombe hanenepi siku ya mnada. 
Na hilo ni neno fupi la usiku huu.

Maggid,
Iringa

No comments:

Post a Comment