WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, November 22, 2012

Slaa awang`ang`ania madiwani 7 Chadema



Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa
  Huenda wakafukuzwa
  Wadaiwa kukaidi chama

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewaweka kiti moto madiwani wake wote wa Halmashauri ya Jiji la Arusha ili kuwabaini walioshiriki katika mchakato wa maandalizi ya uzinduzi wa Jiji hilo sambamba na kushiriki katika vikao vya baraza la madiwani.
Chama hicho kilichukua hatua hiyo kwa ajili ya kuwabaini waliofanya hivyo kwa kuwa kitendo hicho ni kinyume cha msimamo wa chama hicho.
Mbali na kitendo cha kushiriki katika vikao vya baraza la madiwani, chama hicho kilitaka madiwani hao wajieleze kutokana na kuchukua posho mbalimbali za vikao hivyo na maelezo yao kufikishwa katika ngazi ya juu ya chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema kuwa iwapo itabainika kuwa madiwani hao walijipenyeza na kushiriki mchakato wa uzinduzi wa Jiji hilo pamoja na kuchukua posho za vikao, wataadhibiwa kwa mujibu wa taratibu za chama hicho.
Dk. Slaa alisema kuwa msimamo wa chama hicho ni kutomtambua Meya wa Arusha, Gaudence Lyimo (CCM) kwa maelezo kuwa taratibu za kuchaguliwa kwake hazikufuatwa, na kusisitiza kuwa iwapo madiwani wake wanajipenyeza na kushiriki vikao vya halmashauri vinavyoongozwa na Meya huyo ni utovu wa nidhamu.
“Kitendo cha kushiriki vikao vya halmashauri ni kuhalalisha kumtambua Meya wa Arusha, sasa sisi msimamo wetu ni kutoshiriki vikao na hata madiwani wanalijua hilo, ila kama wanashiriki kinyemela na kuchukua posho tutapambana nao,” alisema Dk. Slaa.
Aidha, Dk. Slaa alionya kuwa kitendo cha madiwani wake kushiriki vikao vya manispaa ni mwanzo mbaya wa kuambikizwa madhambi ya ufisadi yaliyopo ndani ya manispaa hiyo yakiwamo matumizi mabaya ya fedha za wananchi.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa Chadema alipotakiwa kueleza msimamo wa Chadema utaisha lini wakati wananchi wanaendelea kusota kutokana na kukosa wawakilishi kwenye kata zao, alisema kuwa diwani anapaswa kushiriki maendeleo kwenye kata yake na wananchi wake na si kushiriki vikao vya halmashauri.
Aliongeza kuwa diwani anapaswa kumfuata ofisini Mkurugenzi wa Jiji na kumweleza matatizo yaliyopo kwenye kata yake bila kushiriki vikao vya baraza la madiwani.
Alipotafutwa mwenyekiti wa madiwani wa Chadema jijini Arusha, Isaya Doita, ambaye ni Diwani wa Kata ya Ngarenaro, alithibitisha kuhojiwa na Dk. Slaa huku akisema kwamba kwa sasa hawana la kusema kwa kuwa wanasubiri maelekezo kutoka ngazi za juu za chama.
Hata hivyo, alikiri kuwa madiwani wa Chadema walioshiriki mchakato wa uzinduzi wa Jiji la Arusha hivi karibuni na kwamba kushiriki na kupokea posho za vikao ni haki yao.
“Sisi tulishiriki katika sherehe hizi za uzinduzi wa Jiji kama viongozi wa wananchi, hatukushiriki katika kikao cha kupanga bajeti cha baraza la madiwani, bali tuliitwa katika kikao cha ghafla, tulipofika tukaambiwa kuwa ni kikao kwa ajili ya uzinduzi wa Jiji,” alisema Doita na kuongeza:
“Awali tulikaa chini na kuafiki kuwa Jiji lizinduliwe mwezi wa kwanza tarehe moja mwakani, sasa kwa kuwa watu walikaa na ikaamuliwa lizinduliwe, tuliamua kushiriki ila siyo kikao cha baraza.”
Hatua ya Dk. Slaa kuwahoji madiwani hao imekuja siku chache baada ya madiwani wa CCM, TLP na Chadema jijini Arusha kushiriki mchakato wa uzinduzi wa Jiji hilo.
Hatua hiyo imeibua gumzo jijini hapa ikikumbukwa kwamba Chadema kiliweka msimamo wa kutomtatabua Meya wa Jiji la Arusha.
Baadhi ya madiwani wa Chadema walioshiriki mchakato wa uzinduzi wa Jiji hilo hivi karibuni, waliongozwa na Diwani wa Kata ya Levolosi, Efatha Nanyaro, ambaye alichaguliwa kuwa Katibu wa moja ya kamati za maandalizi huku mwenyekiti wake akiwa Diwani wa Kata ya Moshono, Paul Matyhsen (CCM).
Chadema kiliwahi kuwatimua madiwani wake watano mwaka jana kwa kosa la kufikia mwafaka na CCM na kumtambua Meya wa jiji la Arusha, kinyume cha msimamo wa chama.
Waliovuliwa uanachama ni Estomii Mallah wa Kata ya (Kimandolu); Ruben Ngowi (Themi); John Bayo (Elerai); Charles Mpanda (Kaloleni) na Rehema Mohamed (Viti Maalum).
Kwa sasa Chadema wana madiwani saba ambao ni Efatha Nanyaro, Isaya Doita, Prosper Msofe, Chrispin Tarimo, Elbariki Maley, Sabina Francis na Viola Lazaro.
WALIOFUKUZWA MATATANI
Wakati huo huo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imetoa uamuzi dhidi ya madiwani watano wa Chadema waliofungua kesi ya kupinga kufukuzwa uanachama wa chama hicho na kushindwa kwamba wanatakiwa kulipa gharama za kesi hiyo Sh. milioni 15.
Madai dhidi ya madiwani hao yalifunguliwa na Chadema wakitaka walipe Sh. milioni 29, lakini mahakama imewataka walipe Sh. milioni 15. Awali madiwani hao walidai mahakamani kwamba hawana uwezo wa kulipa fedha hizo.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Charles Magesa, ambaye alisema kama madiwani hao watashindwa kulipa kiasi hicho watapelekwa gerezani.
Walioamriwa kulipa fedha hizo ni Rehema Mohamed, Charles Mpanda, Rubeni Ngowi, John Bayo na Estomy Malla.
Hukumu hiyo ilitolewa kufuatia madiwani hao waliotimuliwa kufungua kesi ya kupinga kufukuzwa na kuvuliwa uanachama lakini wakashindwa katika kesi hiyo.
Aliwaamuru walipe kiasi hicho cha fedha kama gharama za kesi hiyo kwa awamu mbili.
“Kwa sasa mnatakiwa mhakikishe mnalipa fedha haraka sana na kama mtashindwa kufanya hivyo, basi Mahakama itachukua hatua na maamuzi makali zaidi ya haya,” alisema Hakimu Magesa.
Wametakiwa kulipa fedha hizo kwa awamu mbili, kwanza katika kipindi cha wiki mbili na kisha miezi miwili.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment