WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, November 18, 2012

Rage avunja kamati zote Simba



Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, amevunja Kamati zote tano za klabu hiyo alizoziunda wakati akiingia madarakani miaka miwili iliyopita  baada ya timu kufanya vibaya kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Bara.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Rage alisema amefikia maamuzi hayo baada ya kukutana na kamati ya utendaji juzi.

Aidha, Rage alisema pia amelifuta tawi la klabu hiyo la 'Mpira Pesa' sambamba na kuwafuta uwanachama wa Simba mwenyekiti wa tawi hilo, Masoud Awadhi na mwanachama mwingine wa klabu hiyo, Ally Bane.



Rage alisema kuwa amefikia hatua ya kuvunja kamati hizo tano kwa sababu ameona hazijafanya kazi yake ipasavyo.

Kamati hizo ni ya Ufundi iliyokuwa ikiiongozwa na Ibrahim Masoud 'Maestro', kamati ya mashindano iliyokuwa chini ya Joseph Itang'ala 'Kinesi' pamoja na kamati ya nidhamu iliyokuwa ikiongozwa na Peter Swai.

Pia Rage, alisema kuwa ameifuta pia kamati ya fedha iliyokuwa ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu', na kamati ya usajili iliyokuwa chini ya Zacharia Hanspope.

"Nimetumia nguvu yangu kikatiba kuzivunja kamati hizi kwa lengo zuri tu la kujipanga upya kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi kuu," alisema Rage.

"Kama ambavyo wanachama wameona, mzunguko wa kwanza hatujafanya vizuri na hii imetuumiza wanasimba wote.

"Naenda nyumbani Tabora kutuliza kichwa na kuchagua watu wengine kuongoza kamati hizi.

"Wanasimba watulie kwa kuwa tunajipanga sasa kwa ajili ya mzunguko wa pili."

Akizungumzia wanachama aliowafukuza, Rage alisema wamekuwa wakitoa taarifa za klabu kwa vyombo vya habari huku wakijua kufanya hivyo ni kosa kikatiba kwani kwa mujibu wa katiba hiyo msemaji mkuu wa Simba ni Mwenyekiti, au Katibu mkuu au Afisa habari wa klabu.

"Huyu Masoud Awadhi tumeshawahi kumpa barua ya onyo kwa tabia hii ya kutoa taarifa za klabu kwa vyombo vya habari na pia amekuwa akiitisha mikutano ya wanachama kinyume na taratibu," alisema na kubainisha kuwa "adhabu yake kwa kutumia katiba ni kumfukuza uanachama yeye pamoja na Ally Bane."

Alisema wanachama hao wanaruhusiwa kuomba upya uwanachama na wengine wanaruhusiwa kuunda tena tawi lao kwa kuomba kwa uongozi wa Simba.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment