WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, November 21, 2012

Mwakyembe azuia watumishi wizara yake kupanda daraja la kwanza kwenye ndege



WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amewapiga marufuku wafanyakazi wote walio chini ya wizara yake kusafiri kwa ndege katika daraja la kwanza, akieleza kuwa huo ni ubadhirifu wa fedha za umma.Akizungumza na waandishi wa habari mkoani  Tanga jana, Mwakyembe alisema atakayekaidi  agizo hilo, atakatwa fedha katika mshahara wake.
Mwakyembe ambaye tangu ateuliwe kuwa Waziri wa Uchukuzi amekuwa akifanya uamuzi magumu, alisema hawezi kuvumilia mtu yeyote ambaye atatumia hovyo fedha za walipa kodi, huku akiwataka wafanyakazi wa wizara yake kufanya kazi kwa maadili na kuwatumikia wananchi.
“Kulingana na hali halisi ya maisha ya baadhi ya ya  Watanzania, wizara yangu haitakuwa tayari kuona fedha zikitafunwa na watu wachache kwa njia za kifisadi. Matumizi yafanyike kulingana na hali halisi ya Watanzania,” alisema Mwakyembe na kuongeza;

“Kuanzia leo nawapiga marufuku watendaji wote wa wizara yangu kusafiri na ndege kwa kutumia daraja la kwanza.”

Akizungumzia hali za Mamlaka za Bandari Tanzania (TPA), Dk Mwakyembe alisema, Wizara yake imeunda bodi ya watu wanane ambao wataanza kazi Januari mwakani. Alisema kikosi kazi hicho, kitaleta mapinduzi ya utendaji wa kazi katika mamlaka hiyo.
 
Alisema bodi hiyo itatambulishwa mara baada ya kukamilika kwa baadhi ya mambo muhimu na hivyo kuwataka wananchi kuwa wavumilivu.

Alisema kwa sasa bodi hiyo imeanza mikakati ya kuhakikisha Tanzania inaingia kwa nguvu zote katika soko la ushindani la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Alisema Wizara yake inakusudia kuleta mageuzi katika sekta ya usafirishaji katika bandari zake (PTA) ili kuweza kuleta ushindani wa kibiashara na nchi jirani na  kuweza kuwavutia wafanyabiashara watakaoweza kushusha shehena zao katika  bandari zake.

‘Baada ya kuunda  bodi mpya ya watu wanane ya (PTA), tumedhamiria kwa dhati kuondoa madudu ambayo yalikuwa yanatusumbua katika bandari zetu na kuonekana kama tumeshindwa,” alisema Dk Mwakyembe.
Akizungumzia kuhusu Bandari Mpya ya Mwambani ambayo ujenzi wake bado haujaanza, Waziri Mwakyembe, alisema wale ambao wana ubeza mradi huo mwisho wake wataumbuka kwani ndani ya miezi sita ijayo utaanza.

Alisema mradi huo wa kujenga bandari mpya utaanza ndani ya miezi sita ijayo,  hivyo wale ambao wamekuwa wakiubeza na kuleta  upinzani watambue kuwa mradi huo upo na utaendelea kuwepo na Serikali itahakiksha inatekeleza azma yake.

“ Hao wapinzani wanaoubeza mradi huu wajue kuwa mwisho wake wataumbuka kwani mradi upo na ndani ya miezi sita tutaanza kwani kila kitu kiko tayari na bado utekelezaji wake tu” alisema Dk Mwakyembe.

Kuhusu bandari ya nchi kavu Mwakyembe alisema itajengwa Wilayani Korogwe sambamba na mradi wa reli ambao utakuwa mkombozi kwa watu Korogwe na maeneo ya jirani husasuani kwa wafanyabiashara.

Alisema bandari hiyo ambayo itajengwa sambamba na mradi wa reli utaweza kuwanufaisha wananchi wa Tanga na mikoa jirani kwani mbali ya ajira pia wataweza kujitafutia masoko katika nchi jirani.

chanzo vijimambo.blog

No comments:

Post a Comment