WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, November 18, 2012

Ukosefu wa ajira unatisha - Prof Lipumba


 Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika Wilayani Kasulu, Mkoa wa Kigoma.

 Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika Wilayani Kasulu, Mkoa wa Kigoma.


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimiana na wanachama wa CCM na CUF mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kigoma kuanza ziara ya siku mbili ya kichama Mkoani humo.

Na Hassan Hamad OMKR

Tanzania inahitaji mabadiliko kwa kuwekeza katika kilimo cha kisasa sambamba na kutoa elimu na huduma bora kwa wakulima ili waweze kuendeleza kilimo chenye tija.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi CUF Profesa Ibrahim Lipumba alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma.

Amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na ardhi yenye rutba inayokubali kuotesha mazao mbali mbali, lakini bado hakujakuwepo na mikakati imara ya kuendeleza kilimo, jambo ambalo linapaswa kufanyiwa kazi kwa maslahi ya wananchi.

Prof. Lipumba amefahamisha kuwa Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa Mikoa inayoweza kufanya vizuri katika kilimo kutokana na kuwepo kwa maziwa na mito ya kudumu ambayo inaweza kutumika kwa kilimo cha mboga mboga na umwagiliaji, na kusaidia kukuza kipato cha wakulima.

Sambamba na hilo Prof. Lipumba amewataka wakulima kutilia mkazo mazao ya nafaka yakiwemo mahindi na maharage, kutoka na kuongezeka kwa bei ya mazao hayo katika soko la dunia.

 Mwenyekiti huyo wa CUF Taifa pia amesisitiza haja ya kuwepo kwa mikakati ya makusudi ya kuongeza ajira kwa vijana ili kuwanusuru kujiingiza katika vitendo viovu.

“Ukosefu wa ajira unatisha, na ikiwa vijana hawana ajira wanaweza kushawishika kufanya jambo lolote ambalo linaweza kuliletea madhara Taifa”, alifafanua Prof. Lipumba.

Akizungumzia kuhusu mchakato wa katiba, Prof. Lipumba ametaka katiba mpya ijayo itamke wazi kuwa maliasili za Tanzania na mali ya Watanzania na iweke itaratibu ambao Watanzania wataweza kunufaika na rasilimali hizo.

Amesema iwapo wananchi watanufaika moja kwa moja na rasilimali zao za nchi wataweza kuzilinda na kuziendeleza, lakini vyenginevyo rasilimali hizo zinaweza kuleta maafa badala ya neema kama zilivyo baadhi ya nchi za Afrika zikiwemo Nigeria na Equatorial Guinea.
 Kwa mujibu wa Prof. Lipumba Tanzania ina utajiri wa rasilimali mbali mbali zikiwemo madini, mafuta na gesi asilia ambapo katika siku za hivi karibuni Kampuni moja ya Norway iligundua gesi yenye futi za ujazo trilioni 5 katika kisima kimoja pekee, ambapo jumla inakisiwa kuwepo na gesi trilioni 30 futi za ujazo.

Amesema rasilimaji zipo nyingi lakini zinahitaji kuwepo na uongozi wenye dira utakaozingatia mgawanyo wa rasilimali hizo kwa wananchi na kuimarisha miundombinu ya kiuchumi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad amesema CUF kitasimamia sera yake ya haki na usawa, ili kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata haki zake za msingi zikiwemo za kisiasa, kiuchumi na huduma za jamii.

Amesema tatizo kubwa la Tanzania ni mipango duni ya kiuchumi, na kuwashauri wananchi kukiunga mkono chama hicho ili kiweze kurekebisha kasoro zilizopo na kuimarisha uchumi wa nchi.

Kabla ya mkutano huo, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, aliupongeza uongozi wa Mkoa huo kutokana na ushirikiano mzuri wanaoutoa kwa vyama vya siasa, na kwamba kufanya hivyo ni kuonesha ukomavu wa kisiasa.

Katika uwanja wa ndege wa Kigoma Maalim Seif alipokelewa na viongozi wa mkoa huo pamoja na wafuasi wa CUF na Chama Cha Mapinduzi.

Mkutano huo ni sehemu ya Operesheni mchakamchaka hadi 2015 iliyozinduliwa na chama hicho kwa ajili ya kutembelea mikoa mbali mbali ya Tanzania kutoa uelewa kwa wananchi ili hatimaye waweze kujiunga na chama hicho.

Imewekwa na MAPARA

No comments:

Post a Comment