WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, November 19, 2012

Taarifa ya Skagit yataka wahusika wafikishwe mahakamani



Tume iliyoundwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
kuchunguza ajali ya meli ya MV. Skagit iliyotokea tarehe 18.7.2012
ilipokuwa ikitokea Dare s Salaam kwenda Zanzibar imependekeza kuchukuliwa
hatua za kisheria na kinidhamu watu saba kwa makosa mbali mbali
yaliyochangia kutokea kwa ajali hiyo ili kuhakikisha kunakuwepo uwajibikaji
kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri wa baharini na watendaji wa Taasisi
zinazosimamia suala hilo na kuepusha ajali za mara kwa mara.

 
Akitoa taarifa ya Tume hiyo kwa Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Idara
ya Habari Maelezo Mnazimmoja, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu
Kiongozi Abdulhamid Yahya Mzee amewataja watu waliopendekezwa kuchukuliwa
hatua za kisheria ni mmiliki wa MV.Skagit ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni
ya Seagull Sea Transport Said Abdul-rahman Juma, Nahodha wa meli hiyo
Makame Mussa Makame na Meneja wa Kampuni hiyo tawi la Dar es salaam Omar
Hassan Mkonje.
 
Amesema kutokana na matendo yao ya kuwa karibu mno na sababu zilizopelekea
kutokea kwa ajali hiyo, Tume imependekeza watu hao washtakiwe kwa kosa la
kusababisha vifo kutokana na uzembe.

Mmiliki wa kampuni hiyo amefanya kosa la  kufanya biashara ya usafiri wa
baharini kwa kutumia chombo ambacho hakikusajiliwa kwa mujibu wa sheria na
kutumia chombo ambacho hakikutimiza masharti ya ukaguzi kwa mujibu wa
sheria ya usafiri wa baharini Zanzibar namba 5 ya mwaka 2006, kumuajiri
nahodha bila ya kuwa na cheti cha umahiri cha daraja la tano  na kuruhusu
meli kupakia idadi kubwa ya abiria kinyume na uwezo wake.
 
Abdulhamid amesema taarifa hiyo imesema Nahodha Makame Mussa ametenda kosa
la kuendesha meli akiwa hana cheti, kushindwa kuwaandaa abiria  kujiokoa
wala kutoa taarifa ya dharura, kuendesha meli hali ya kuwa si salama na
kuruhusu kupakia abiria 431 badala ya 250 iliyoainishwa kwenye cheti cha
abiria.

Watu  waliopendekezwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu ni  aliekuwa Mkaguzi
wa meli na Kaimu Mrajisi wa meli kutoka Mamlaka ya usafiri wa baharini
Zanzibar Juma Seif Juma, Mkaguzi wa kujitegemea Capt. Saad Shafi Adam na
Maafisa wa usalama wa bandari ya Dar es Salaam Johari Mikidadi  Ndumbati na
Peter Ndimbwa Mwasi kwa kushindwa kudhibiti uingizaji wa abiria katika meli
ya MV. Skagit siku iliyopata ajali ikiwa ni kinyume na majukumu yao ya kazi.

 
Taarifa hiyo imetoa mapendekezo ya kuimarisha Sheria na kanuni za usafiri
wa baharini namba 5 ya 2006 kwa kuvifanyia marekebisho baadhi ya vifungu
ikiwemo kuweka utaratibu wa kisheria utakaowalazimisha wafanyabiashara wa
usafiri wa baharini kuwa na utaratibu wa kuuza tiket za safari pamoja na
kutengeneza urodha ya wasafiri kwa njia ya electroniki na kuweka utaratibu
wa kisheria unaowalazimisha uongozi wa kampuni unaoendesha biashara ya
usafiri wa baharini kuwa na taaluma ya masuala ya usafiri wa baharini.


Aidha Abdulhamid amesema Tume hiyo imependekeza Kampuni kuwalipa fidia
abiria wote waliokuwemo ndani ya meli.  Kwa  waliofariki walipwe thamani ya
kiwango cha mshahara wa chini cha muda wa miezi 80 na walionusurika na
kupata ulemavu walipwe asilima 75 ya kiwango cha waliofariki na watu
wengine walionusurika bila ya kupata majeraha yoyote walipwe asilimia 50 ya
kiwango   walicholipwa waliofariki.

Katika ajali hiyo watu 81 wakiwemo raia watatu wa kigeni walifariki na
maiti zao zilipatikana na kuzikwa,  212 walipotea na 154 waliokolewa wakiwa
hai wakiwemo raia 15 wa kigeni.

 
Katibu Mkuu Kiongozi amesema Tume imeeleza sababu za kutokea ajali hiyo
kuwa ni upepo mkali, muundo wa meli ilioruhusu abiria wengi kukaa juu,
mwendo wa kasi, nahodha kukosa ujuzi na umahiri na abiria kuwa wengi kupita
kiwango chake.

Amesmea Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekubaliana na mapendekezo yote
yaliyotolewa na Tume hiyo iliyokuwa na wajumbe 10 chini ya mwenyekiti wake
Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar Abdulhakim Ameir Issa.


IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment