WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, November 27, 2012

Slaa: CCM haina ubavu wa kuwabana mafisadi


Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Willibrod Slaa amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake hawana ubavu wa kupambana na mafisadi nchini kwa kuwa wao ndiyo waliochangia kuwaweka madarakani.

Kadhalika, viongozi wa CCM na serikali wametakiwa kuacha tabia ya kwenda kwa wananchi na kuwaomba msamaha kwa kushindwa kutekeleza ahadi zao waliozoahidi mwaka 2005 na 2010 huku wakiwa mikono mitupu badala yake wanatakiwa kwenda kuwaambia wamefanya nini.



Dk. Slaa alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho katika Jimbo la Kigamboni.

Alisema Watanzania wataendelea kuona mafisadi wakitanua huku rasilimali za nchi zikiibiwa kwa kuwa serikali ya CCM haina ubavu wa kukemea uchafu huo ingawa inawajua wote kwa majina.

“CCM na serikali yake hawana ubavu wa kupambana na mafisadi kwa sababu hawa hawa ndiyo waliowaingiza madarakani kwa kutumia fedha chafu,” aliwaambia wajumbe hao.

Aliwataja baadhi ya majina  ya watu (tunayahidahi) aliodai kuwa walitumia fedha chafu zilizotokana na rushwa kuhakikisha CCM inashinda chaguzi za mwaka 2005 na 2010.

Aidha, alisema licha ya CCM kuwaogopa mafisadi, lakini pia imeshindwa kudhibiti wizi na vitendo vya utoroshwaji wa wanyama wakubwa wakiwamo Twiga ndani ya ndege na kwenda kuuzwa nje ya nchi.

“Haya ni maajabu kuona Twiga mkubwa namna ile anakunjwa na kuingizwa kwenye ndege huku serikali ya CCM ikishindwa kuchukua hatua za kukomesha wizi huo,” alisema Dk. Slaa akiwa katika ziara yake ya siku nne ya kutembelea majimbo ya Kigamboni, Temeka, Ilala na Kinondoni.

Kuhusu viongozi wa CCM na serikali kwenda kuwaomba msamaha wananchi, Dk. Slaa alisema hayo ni mapungufu makubwa ya utendaji na kwamba wao walitakiwa kwenda kuzungumza na wapiga kura wao wakiwa na kitu mkononi na siyo kuomba wahurumiwe kwa kushindwa kutimiza ahadi walizoahidi kuzitekeleza baada ya kupewa ridhaa ya kuiongoza nchi.

“Kama ni shule kila mwananchi kwa nafasi yake amechangia kuzijenga, sasa wao walizojenga zipo wapi?” alihoji kiongozi huyo na kuongeza kuwa hilo ndilo swali linaloulizwa na Watanzania wengi katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema Chadema kitaendelea kukusanya mapungufu hayo ya CCM na kuyapeleka kwa wananchi ili mwaka 2015 waiweke pembeni kwa kuwa kimeshindwa kutimiza kilichoahidi mwaka 2005 na 2010.

Kwa mujibu wa Dk. Slaa, kwa sasa viongozi wa CCM wanafanya mchezo wa kuigiza kutokana na kurudi  kuomba msamaha kwa wananchi badala ya kutekeleza ilani kwa vitendo.

“CCM kimekuwa kama popo, hakijulikani kwa sasa kinafanya nini kwa wananchi, na wananchi nao hawakielewi uhalisi wake na hii ni hatari, mustakabali wa taifa letu hususani katika kutafuta maendeleo,” alisema Dk. Slaa

 Aidha, Dk. Slaa alisema CCM kiache kuhubiri kwamba Tanzania ni nchi ya Ujamaa na Kujitegemea kwa kuwa baada ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, mashirika yote yameuzwa na kufanya nchi iwe ya kibepari.

“Mkapa (Benjamin) alianza kuuza kila alichoona mbele yake na sasa nchi imejikuta haina shirika ambalo kila Mtanzania anafaidika nalo kama ilivyokuwa wakati wa Mwalimu Nyerere na hii ilitokana na kuvunjwa kwa Azimio la Arusha na kuanzishwa Azimio la Zanzibar,” alisema Dk. Slaa.

AWATETEA WAKAZI KIGAMBONI

Akizungumzia hatma ya wananchi wa Kigamboni wanaotarajiwa kuhamishwa kupisha ujenzi wa mji mpya, Dk. Slaa alisema hajawahi kuona nchi isiyojali watu wake kama Tanzania kwa kuwa inawaondoa watu wake ili kuwafurahisha wawekezaji.

“Mimi nimekaa Canada, pale Canada kuna msitu mkubwa wa hifadhi karibia robo ya nchi ile na mtu haruhusiwi kuugusa kwa kuwa wanasema unatunzwa kwa ajili ya vizazi vijavyo miaka elfu tatu, lakini Tanzania hicho hakuna kila kitu kinakwenda kiholela,” alisema Dk. Slaa.

Kuhusu uhai wa Chadema, Dk. Slaa aliwataka viongozi wa Chama hicho kutumia mbinu mbalimbali kuhakikisha  watu wanakiunga mkono kuanzia ngazi ya chini.

Aliwataka viongozi wa Chadema ambao hawajui wajibu wao kukaa pembeni kwa kuwa hawataweza kukivusha na kuingia Ikulu mwaka 2015.

Aliwakumbusha viongozi na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jimbo la Kigamboni kuendesha chama kwa kuzingatia Katiba yao na badala ya mtu kuibuka kufanya anachoona kinafaa.

CCM YAJITAPA

Wakati Dk. Slaa akisema hayo, CCM kimesema kuwa ziara iliyofanywa na Sekretarieti mpya ya chama hicho katika mikoa ya Rukwa, Mtwara, Geita na Arusha kimepata mafanikio mengi tofauti na walivyotarajia.

 “Kwa sasa tunaendelea vizuri na ziara yetu, mafanikio ni mengi, tukimaliza tutawapa ratiba ni mikoa gani tutakwenda,” alisema Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) wa Itikadi na Uenezi ya CCM, Nape  Nnauye.

Aidha, Nnauye, amesema kuwa hakuna Waziri yeyote aliyezomewa katika ziara hiyo tofauti na ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.

Akizungumza na NIPASHE jana, Nnauye alisema katika ziara hiyo viongozi wote wa CCM walipanda jukwaani kujibu kero mbalimbali za wananchi katika mkutano wa kwanza wa viongozi wapya, ukiongozwa na Katibu Mkuu wake, Abdulrahaman Kinana, na hakuna Waziri yeyote aliyezomewa.

Alisema habari za Mawaziri kuzomewa ni propaganda za vyombo vya habari.

Wiki iliyopita, mawaziri watatu wa CCM, Christopher Chiza wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Hawa Ghasia (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa -Tamisemi) na Naibu wake, Aggrey Mwanri, wakiwa  mkoani Mtwara wanadaiwa kuzomewa baada ya kupanda jukwaani kujibu kero mbalimbali za wananchi katika mkutano wa kwanza wa viongozi wapya wa CCM taifa, ulioongozwa na Kinana.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment