WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, November 30, 2012

Palestina Yazidi Kukubalika




 Na Mwandishi Maalum
 Palestina jana ( alhamisi) imeibuka kidedea baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kuweka historia kwa kupiga kura Azimio lililoipandisha hadhi ya kutambuliwa kama Nchi Muangalizi asiye Mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Azimio hilo lilipitishwa kwa kura 138 za ndiyo , kura tisa za hapana na 41 za kutofungamana na upande wowote. Kati ya nchi zilizopiga kura ya hapana na ambazo zilitegemewa ni Marekani, Israel na Canada huku Ujerumani na Uingereza zikipiga kura ya kutofungamana na upande wowote Ukumbi Mkuu wa Mikutano wa Baraza hilo ulifurika wajumbe wa katika tukio hilo la kihistoria lililokuwa na sura ya mchuano mkali wa mpira wa miguu ambapo kila upande ulikuwa ukijitahidi kushangilia kwa nguvu kila msemaji wa upade fulani aliposimama kujenga hoja ya kutaka Azimio liungwe mkono au akijenga hoja ya kupinga Azimio hilo. 

Azimio hilo limeungwa mkono na mataifa mengi kutoka pande zote yaani mataifa yale makubwa kama vile Ufaransa, China, na Urusi nchi ambazo ni wajumbe wa kudumu wa Baraza Kuu la Usalama. Zikiwamo pia nchi nyingi za Jumuiya ya Ulaya, Afrika,Asia na Visiwa vya Karibian Tukio hilo pia lilishuhudiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ambaye alisema, kura ya kupitisha azimio hilo ilikuwa ikisisitiza umuhimu wa kutoa msukumo mpya wa kuanza mazungumzo na akazisihi pande hizo mbili kuonyesha dhamira ya kurejea kwenye meza ya mazungumzo. Licha ya ukweli kwamba bado Palestina ina safari ndefu ya kuweza kukubaliwa kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa, lakini kwa kukubaliwa kwake kuwa na hadhi ya kuwa nchi muangalizi asiye mwanachama, kunaifungulia milango ya kujiunga na taasisi nyingine za kimataifa, ikiwamo Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai( ICC) kama ikitaka kufanya hivyo. 

Akizungumza kabla ya kupiga kura, Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, aliwataka wajumbe wa Baraza hilo kuchukua hatua muhimu ya kurekebisha dhuluma ambayo wametendewa wananchi wa palestina kwa muda mrefu. Kwamba alikuwa anaitaka jumuiya ya kimataifa kuliunga mkono azimio hilo na hivyo kupeleka ujumbe wa matumaini kwa wananchi wa Palestina ambao amewaelezea kama walioteseka kwa muda mrefu na waliokuwa wakielekea kukata tamaa. Katika hotuba yake iliyokuwa ikikatishwa mara kwa mara kwa makofi na miluzi kutoka kwa wajumbe wa mkutano huo. Kiongozi huyo wa Palestina, akabainisha kwamba walikuwa wameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuona mazungumzo ya kutafuta amani kati yake na Israeli ni kama vile yalikuwa yamekufa. 

Hata hivyo akasisitiza kwamba wamefikia hatua hiyo ya kupita Baraza Kuu kuomba kupandishwa hadhi na kutambuliwa kuwa nchi muangalizi asiye mwanachama hasa baada ya ombi lao kupitia Baraza Kuu la Usalama kutofanyiwa kazi. Lakini pia wamechukua hatua hiyo kama kielelezo cha kuthamini amani na haki yao ya msingi kama raia wengine ya kuwa na uhuru wa si tu kuwa na taifa lao linalotambuliwa bali pia haki na fursa ya kujiamulia mambo yao wenyewe. “ Hatukuja hapa kutaka kufuta uhalali wa taifa fulani yaani Israeli, lakini tuko hapa kutafuta uhalali wa taifa jingine yaani Palestina,kwamba lazima sasa iijipatie uhuru wake” akasema Mahmoud Abbas Na kuongeza “ Tunawaomba leo hii mtupatie cheti chetu cha kuzaliwa”. Akasama Abbas na kuongeza kwamba uamuzi huo hauna maana kwamba wanaachana na mchakato wa kurejea kwenye meza ya mazugumzo. Wala haukuwa na nia ya kutaka Azimio la kuipandisha hadhi Palestina limepigiwa kura katika tarehe ( Novemba 29) ambayo Baraza hilo lilikuwa likiadhimisha miaka 65 tangu lililopitisha azimio namba 181 lililoigawa Palestina kuwa mataifa mawili lile la Kiyahudi na la Kiarabu. 

Aidha Tarehe hiyo pia huadhimishwa siku ya kimataifa ya mshikamano na wananchi wa Palestina. Siku ambayo ilipitishwa mwaka 1977 Kwa upande wake Balozi wa Israeli katika Umoja wa Mataifa, Ron Prosor yenyewe imesema nchi yake haikubaliani na azimio hilo na kwamba Palestine ilikuwa inafanya kosa kubwa na itakuja kujuta hapo baaaye. Aidha Israel inasema haliitambui Azimio hilo kwa sababu lilikuwa limeegemea upande mmoja na lilikuwa haliitambua taifa la Kiyahudi. Mjumbe huyo wa Israeli akiongea kwa kejeli alieleza baya kwamba, azimio hilo haliwezi kwa namna yoyote ile kuleta amani bali lilikuwa linarejesha nyuma mchakato wote wa kuleta amani, na kwamba yenyewe ilikuwa inamini katika majadiliano badala ya njia za mkato mkato kama iliyofanya Palestina hiyo jana. 

Nayo Marekani kupitia Balozi wake Susan Rice imeeleza bayana kwamba haikubaliani na azimio hilo ambalo kwao ilikuwa ni kama kupoteza muda. Hata pamoja na kukandia na kuzikejeli nchi zilizopiga kura ya kuunga mkono azimio hiyo, Marekani inasema itaendelea na juhudi zake za kuhakikisha kwamba mazungumzo ya kutafuta suluhu ya kudumu kati ya pande hizo mbili yanaendelea. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikuwa ni kati ya nchi zilizopiga kura ya kuunga mkono azimio hilo, na Balozi Tuvako Manongi alielezea ni kwa nini Tanzania iliamua kupiga kura ya ndiyo. 

Baadhi ya sababu alizotoa ni kwamba Tanzania ilishaitambua Palestina kama nchi huru tangu mwaka 1961 na imekuwa na uhusiano wa kidiplomasia na nchi hiyo kwa miaka mingi. Aidha akasema kwa kupishwa kwa azimio hilo jumuia ya kimataifa ilikuwa inalitambua taifa huru la wapalestina kama vile ilivyoitambua Israel na kwa Tanzania mataifa yote mawili yana uhalali wake. Akaongeza pia kwamba Tanzania inaamini Palestina ilikuwa na kila sababu ya siyo tu kutambuliwa lakini pia kuwa na uhuru wa kujiamulia mambo yake. Akasisitiza kuwa Tanzania inaamini katika makubaliano na majadiliano yanayolenga kufika suluhu ya kuwa na mataifa mawili yakiishi sambamba na kwa amani kulingana na makubaliano ya mwaka 1947;

source:mjengwa blog

No comments:

Post a Comment