WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, November 18, 2012

Neno La Leo: Maisha Yetu Na Falsafa Ya Mtungi...




Ndugu zangu, 

Asubuhi hii nikitoka kwenye mchakamchaka ( jogging) nilimsikia mchungaji wa kanisa akiwatamkia waumini wake; 

“ Angalieni upepo, nguvu ya upepo. Duniani upepo unaweza kutingisha miti, ukavunja matawi na hata ukaangusha miti....!” Sikusimama nikasikiliza alichotaka kusema Mchungaji yule juu ya upepo na nguvu zake. Lakini, nami nikaanza kutafakari na kujiuliza; Matatizo yetu wanadamu na hasa sisi Watanzania ni nini? 

Nikafikiri, kuwa mara nyingi Watanzania hatutaki kuyajua matatizo yetu. Tunataka kuyajua ya wenzetu. Na tukiyajua yetu, hatutaki kuyaweka wazi. Tu mahodari wa kusiliba matatizo yetu. Nje hayaonekani, yamesilibiwa, lakini, ndani hali iko vile vile. 

Tuliokaa vijijini tunajua, kuwa nyumba ya kijijini haijakamilika bila kuwa na mtungi. Afrika hakuna tu siri ya mtungi, kuna falsafa ya mtungi pia. Ninapoingia kwenye nyumba kijijini huangalia kwanza ulipo mtungi. 

Kwenye mtungi yawezekana ndimo yalimo maji ya kunywa. Na ukiinamia mtungi wa maji, usiaangalie sana, chota maji yako, kunywa. Lakini, mtungi pia hutumika kuhifadhia vyakula; iwe unga au maharage. Mara nyingi mtungi huwekwa kwenye kona ya chumba. Na mtungi ukikaa sana, basi, siku ukiinuliwa, hutaacha alama.

 Na unafanye basi mtungi wa maji unapoonyesha kuwa na nyufa, kuwa maji yameanza kuvuja? Kuna mawili; la kwanza si la busara sana. Ni jawabu la muda mfupi, la pili ni la busara zaidi, ni suluhisho la muda mrefu. 

Afrika mtungi wenye nyufa unaweza kuzibwa kwa kusaga vipande vya mtungi wa zamani, kisha ukachanganya na nta. Baada ya hapo utasiliba kwenye nyufa za mtungi. Hiyo ni njia ya kwanza, ni suluhisho la muda mfupi. Maana, tabu inakuja, siku mtungi utakapohitajika kuchemshia ‘ komba’- togwa la pombe. Basi, kwenye moto mkali wa kuni nyufa zile, pamoja na kusilibwa na nta, hazitahimili nguvu ya moto. Mtungi utamegeka vipande vipande. ‘ Komba’, ama togwa la pombe litamwagika. 

Naam, dawa ya mtungi wenye nyufa si kusiliba kwa nta, ni kufinyanga mtungi mpya, basi. Na jamii yetu imekuwa ni kama ya ‘ Super- glo’, ile gundi inayoaminiwa inaweza kusiliba , ama kuunga chochote kile. Kila jambo tunakimbilia kuitafuta ‘ Super-glo’. Kama nta, Super-glo nayo haihimili kwa muda mrefu joto la moto, au hata la jua. 

Wanadamu tuwe na ujasiri wa kuyatambua matatizo yetu kama yalivyo. Tusiwe wepesi wa kukimbilia ‘ kusiliba’ kwa nta ua super-glo. Mengine ni ya kuyafanyia mabadiliko ya jumla. 

Natamani nikutane na Mchungaji yule wa Kanisa, aniambie, kuwa kwake alikuwa na maana gani aliposema kuwa upepo ni tatizo. Tafakari

Maggid Mjengwa, 

Iringa.

No comments:

Post a Comment