WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, November 18, 2012

Chadema yatoa tamko dhidi ya polisi


Chama  cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema ) kumetoa tamko kumtaka  Rais Jakaya  Kikwete kuonyesha  dhamira ya  kushughulikia malalamiko waliyotoa kwake dhidi ya matumizi ya polisi kupambana na wakosoaji wa CCM na serikali.

Tamko hilo limo kwenye  taarifa ya Chadema iliyotolewa na Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama Wilfred Lwakatare, iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam.

Katika andiko hilo, walimtaka Rais Kikwete atekeleze mambo yaliyoandikwa kwenye barua ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliyetaka serikali ifanye uchunguzi wa matukio ya utesaji yaliyofanywa na vyombo vya dola dhidi ya wanaoipinga serikali.

Waraka huo  ulitaka uchunguzi ufanyike dhidi ya polisi waliotumika kuteka, kutesa na kuua kwa malengo ya kisiasa ya kupambana na wakosoaji wa chama tawala na serikali yake.

Katika taarifa yake, Chadema ilisema walimwandikia Rais wakitaka kufanyike uchunguzi huru kwa kuunda Tume ya Kimahakama/Kijaji ili ukweli ujulikane na haki ionekane ikitendeka badala ya kutoa lugha ya kisiasa kwa nia ya kujikosha mbele ya umma, wakati  CCM na polisi, wanakaa na kupanga mikakati inayopelekea kudhulumu haki na roho za Watanzania.

Aidha, wakati uchunguzi huo ukifanyika, watuhumiwa wote, wakiwemo viongozi wa CCM, serikali na watendaji wa Jeshi la Polisi waliokubali kutumika, hata kuvunja haki za binadamu, katiba na sheria, wanawajibika kwa wao kujiuzulu au kufukuzwa kazi.


Rwakatare alisema kauli  iliyotolewa na Mwenyekiti wa CCM, Rais  Kikwete kuwataka viongozi na wanachama wa chama hicho waache kutegemea Jeshi la Polisi katika kukabiliana na wapinzani ni ushahidi wa tuhuma ambazo Chadema imekuwa ikitoa dhidi ya chama hicho.

Hivi karibuni Rais Kikwete, alikitahadharisha chama hicho kuwa kikitegemea zaidi polisi kwamba ndiyo msaada kwake katika kujibu mapigo ya wapinzani kitashindwa.

Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Nane CCM baada ya kuchaguliwa kwa mara nyingine kuwa Mwenyekiti kwa miaka mingine mitano, alisema viongozi wa CCM lazima wajipange na kuwa wepesi wa kujibu mapigo ya wapinzani.

Alisema jawabu la siasa siyo polisi bali ni wanasiasa wenyewe na kwamba polisi hawawezi kuwa jibu la suala la siasa lazima kila kiongozi ajitambue yeye mwenyewe ndiyo mwenezi katika eneo lake.

Chadema ilisema Watanzania wanajua kuwa matukio ya vyombo vya dola kuhujumu wapinzani na wakosoaji wa serikali ya CCM, kwa nia ya kuilinda CCM, yamekwenda kwa sababu watu na makundi ya kijamii pia wameanza kuandamwa.

“Mtu, watu au makundi mbalimbali ya kijamii ambayo yanaonekana kutoa mawazo mbadala, kudai haki na uwajibikaji yameanza kuandamwa. Mifano mizuri hapa ni kufungiwa kwa Gazeti la Mwanahalisi na kutekwa na kuteswa kwa kiongozi wa madaktari, Dk. Steven Ulimboka. “  ilisema taarifa ya Rwakatare.

 Chadema ilisema ukweli huo umesaidia kumaliza fumbo lililokuwepo juu ya madai ya muda mrefu kuwa Jeshi la Polisi linatumika kisiasa na viongozi wa CCM na watendaji wa serikali.

“Kauli hiyo ya Kikwete imetufikisha kwenye kilele cha ushahidi kuwa Jeshi la Polisi linatumika kisiasa kukabiliana na hoja na shughuli halali za kisiasa zinazofanywa na Chadema ,  chama mbadala kwa sasa kinacholenga kuiondoa CCM madarakani”.

Aidha imesaidia kufumbua fumbo la kwa nini Jeshi la Polisi Mkoani Iringa  lilitumia nguvu kubwa kuingilia shughuli halalli za  Chadema kufanya mikutano ya ndani, ikiwemo ufunguzi wa matawi katika Kijiji cha Nyololo, mkoani Iringa, na hatimaye kusababisha kifo cha Mwanandishi wa Habari, Daudi Mwangosi, Septemba  mwaka huu.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment