WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, November 17, 2012

Safu ya Mkapa yarejea CCM


KUNA kila dalili kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amekirejesha chama hicho katika mikono ya Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, baada ya kuwateua katika nafasi za juu za CCM waliokuwa wasaidizi wa mtangulizi wake huyo.

Wasaidizi hao ni pamoja na Makamu Wenyeviti, Philip Mangula (Tanzania Bara) na Dk Ali Mohamed Shein (Tanzania Zanzibar) pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana, ambao walichaguliwa na kuteuliwa katika vikao vya juu vya CCM vilivyomalizika hivi karibuni mjini Dodoma.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kwamba lengo la mabadiliko yaliyofanywa ni kujaribu kurejesha utaratibu wa CCM kuisimamia Serikali, utamaduni ambao ni kama ulikuwa umekufa, tangu Serikali ya awamu ya nne ilipoingia madarakani.

Mhadhiri wa zamani wa Chuo cha Ushirika Moshi, Akwiline Kinabo anasema kwamba kuna kila dalili kuwa Mkapa ana ushawishi katika uteuzi wa safu mpya katika sekretarieti ya chama hicho.
“Inawezekana Mangula, Kinana na Dk Shein walifanya vizuri sana enzi za Mkapa hadi akashawishi waingizwe kwenye sekretarieti ya sasa, lakini enzi za Mkapa na sasa ni kama mlima na kichuguu,” alisema.
Kinabo ambaye katika uchaguzi wa CCM uliomalizika mwezi uliopita aligombea Nec kupitia Moshi Mjini na kushindwa, alisema viongozi hao hawawezi kwenda na kasi ya siasa za vijana wa sasa.

Kada huyo wa CCM alihoji, ”Hivi Kinana au Mangula wataweza kushindana na hoja za Halima Mdee na Zitto Kabwe majukwaani? Kuna vijana wengi wameshinda Nec kwa nini wasiingizwe huko?”
Naye mwasisi wa CCM na kada wa siku nyingi wa chama hicho, Steven Mashishanga alisema kuwa viongozi waliochaguliwa waliwahi kufanya vizuri siku zilizopita, hivyo hakuna shaka kwamba watarejesha utaratibu wa kutekeleza mwongozo wa chama wa 1981.

“Ukisoma mwongozo huo kuanzia ibara ya 81 utabaini kwamba kazi ya chama ni kuisimamia Serikali, hili lilikuwa halifanyiki kwa muda mrefu katika awamu ya nne, sasa hawa waliochaguliwa lazima waturejeshe katika msingi huo,” alisema Mashishanga ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Mikoa ya Mwanza, Tabora na Morogoro.

Hata hivyo, alisema wasiwasi wake ni iwapo uongozi mpya utaweza kuleta mabadiliko kutokana na Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho kujaa wabunge na mawaziri ambao hawawezi kuwa na ujasiri wa kuukosoa uongozi wa juu wa chama.
“Mimi kwangu msimamo unabaki kwamba chama ni chama na Serikali ni Serikali, huwezi kuwa chama na Serikali kwa wakati huohuo.

Sasa wewe jiulize, hivi waziri anaweza kukaa kwenye NEC akamkosoa mwenyekiti ambaye ni Rais wake? Hapo kuna kasoro ambayo tunapaswa kuirekebisha,” alisema Mashishanga.
Mangula, alikuwa Katibu Mkuu wa CCM takriban kwa miaka 10 ya utawala wa Mkapa, huku Kinana ambaye akiwa amefanya kazi za chama kwa muda mrefu awamu ya Mkapa.
Kwa upande wake Dk Shein aliibuliwa kuwa kiongozi wa juu serikalini na Mkapa, wakati alipomteua kuwa  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Julai 13, 2001 kutokana na kifo cha ghafla cha mtangulizi wake, Dk Omar Ali Juma kilichotokea Julai 4, mwaka huo.

Philip Mangula
Mangula ambaye ametumikia nyadhifa mbalimbali za chama na Serikali kwa miaka mingi, aliteuliwa na Mkapa kuongoza chama hicho, kuanzia mwaka 1997 hadi mwaka 2007.
Katika uongozi wake, Mangula anasifika kwamba alikijenga chama na kuwa imara na kwamba wakati wa utawala wake hapakuwa na makundi yaliyotishia uhai wa CCM kama ambavyo imejitokeza kwa siku za karibuni.
Mangula ambaye ni mmoja wa makada wakongwe ndani ya CCM, mbali ya kuwa Katibu Mkuu, amewahi kuwa mwalimu wa Chuo cha Chama Kivukoni kwa muda mrefu.
Pia amewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Mkuu wa Mikoa ya Kagera, Tabora na Mwanza na baadaye kuingia katika utendaji wa chama.
Hata hivyo, alipata pigo la kisiasa baada ya Rais Kikwete kuingia madarakani alipounda safu mpya ya uongozi wa chama hicho mwaka 2007 na kumwacha.
Mkongwe huyo wa siasa nchini, aliamua kurejea nyumbani kwake Kijiji cha Imalinyi, Wilaya ya Njombe na kujikita katika kilimo cha nyanya.
Mangula wakati akiwa katibu mkuu, ndiye aliyesimamia mchakato wa kumpata mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na Rais Kikwete kufanikiwa kugombea.

Kinana na Dk SheinKwa upande wake, Kinana, alikuwa msimamizi mkuu wa kampeni za urais za Rais Mkapa wakati anaingia madarakani 1995 na baadaye akaongoza kampeni yake ya kuwania kuongoza ngwe ya pili 2000.
Mbali ya kuongoza kampeni yake Rais Mkapa alikuwa akimtumia Kinana katika mambo ya kisiasa mengi ikiwamo kumteua katika Kamati Kuu ya chama kwa muda mrefu.
Uhusiano huo mkubwa wa Mkapa na Kinana ndiyo ambao umemfanya Rais huyo mstaafu kuendelea kufanya naye kazi, kwani hivi sasa ni mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya Mkapa (Mkapa Foundation).
Kinana aliingia katika bodi hiyo inayoogozwa na Meja Jenerali Mstaafu, Herman Lupogo mwishoni mwa mwaka jana. Baadhi ya wajumbe wenzake katika bodi hiyo ni Dk Gilbert Mliga, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia, Dk Yahya Ipuge, Eileen Swain a Profesa  Eden Maro.

Kwa upande wa Dk Shein wakati alipoteuliwa na Mkapa hakuwa mtu ambaye alikuwa akifikiriwa katika nafasi ya Makamu wa Rais, kwani hakuwa na jina kubwa miongoni mwa wanasiasa wa Zanzibar.
Rais Mkapa aliyaweka kando majina makubwa ambayo yalikuwa yakitarajiwa wakati huo, hatua ambayo inamfanya Dk Shein kuikumbuka Julai 13, 2001 kuwa siku ya pekee katika maisha yake.
Akitoa shukrani baada ya kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM mjini Dodoma wiki iliyopita, Dk Shein alisema tarehe 13 ni siku maalumu katika maisha yake, kwani ndiyo siku alipoteuliwa kushika wadhifa wa makamu wa rais, wakati huo akiwa hajui pa kuanzia.
“Leo hii ni tarehe 13, lakini si mwezi Julai bali mwezi Novemba, nachaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, lakini tofauti na wakati ule, leo ninafahamu pahala pa kuanzia,” alisema Dk Shein.

Wasemavyo wanaCCM
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM kutoka Wilaya ya Nzega, Hussein Bashe akizungumzia uteuzi huo alisema, ni mzuri kwa sababu umechanganya wazee na vijana.
Alisema safu hiyo mpya ya chama inaonyesha taswira ya mwelekeo wa chama, kwani uzoefu wa Mangula na Kinana ambao wametumikia chama tangu enzi ya utawala wa Rais Mkapa utasaidia sana kukifanya kiendelee kuongoza nchi hii.

Bashe alisema uteuzi wa safu hii ndiyo suluhisho la migogoro iliyopo ndani ya chama hicho.
“Migogoro na mpasuko ndani ya chama chetu sasa basi,” alisema.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja alimpongeza Rais Kikwete kwa kuteua watu wanaofaa katika uongozi wa chama hicho.
Alisema uzoefu wa muda mrefu wa Kinana na Mangula ambao wametumikia hata awamu nyingine ya uongozi wa nchi, unatosha kukifanya chama hicho kuwa na safu ya uongozi ambayo ni ya ushindi.
Mgeja alisema anaamini safu hiyo imefungua ukurasa mpya wa matumaini katika chama hicho ambacho kilikuwa kimekumbwa na migogoro mingi.

CHANZO: www.mwananchi.co.tz/habari/Siasa

No comments:

Post a Comment