WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, November 14, 2012

Chadema yampa ushindi Wassira


Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akipiga kura ya kupitishwa kuendelea kushika wadhifa huo wa chama katika mkutano mkuu wa chama hicho mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi MCL

Julius Magodi na Habel
Chidawali, Dodoma
USHINDI wa kishindo ambao ameupata Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira katika nafasi kumi za ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, unaelezwa kuwa unatokana na yeye kutokuwa katika kambi yoyote iliyopo katika chama hicho.

Vilevile, ushindi wa Wassira ambaye aliibuka kidedea kwa kuzoa kura 2,135,unatokana kumudu jukwaa wakati wa kujieleza na kuonyesha kuwa yeye ni mwarobaini kwa wapinzani hususan Chadema.

Wakati akijinadi mbele ya wajumbe kabla ya kupigiwa kura, Wassira aliomba apewe nafasi hiyo ya ujumbe wa Nec, ili apeleke kilio Chadema.

“Nipeni kura nipate nafasi ili nipeleke kilio Chadema,” alisema Wassira huku akishangiliwa wakati akiomba kura na Rais Jakaya Kikwete akimwita kwa jina la utani, Tyson.

Baadhi ya makada wa CCM waliliambia gazeti hili kwamba kete ya kuwashughulikia Chadema, ‘ilimbeba’ Wassira ikizingatiwa kwamba chama hicho cha upinzani ndicho kinachowakosesha CCM usingizi.

Wassira ambaye aliwahi kuwa mbunge wa upinzani kupitia Chama cha NCCR-Mageuzi, hivi sasa ni mmoja kati ya makada tegemeo wa CCM na katika siku za karibuni amekuwa mstari wa mbele katika shughuli zote za chama hicho hasa za utatuzi wa migogoro na pale chama chake kinapohitaji utetezi  mbele ya vyama vya upinzani.

Miongoni mwa shughuli hizo ni kuwa mmoja wa walioongoza kampeni za CCM katika chaguzi ndogo za Igunga na Arumeru Mashariki, ambako alitumia muda mrefu kukishambulia Chadema na viongozi wake. Pia kushughulikia mgogoro ndani ya CCM mkoani Arusha na bungeni amekuwa akiongoza kujibu hoja za wapinzani, ingawa umma umekuwa ukikosoa kauli zake za mara kwa mara.

Habari zilizopatikana zinaeleza kwamba sababu nyingine ya Wassira kupata kura nyingi ni kutokana na yeye kutokuwa katika kambi ya makundi ya kuusaka urais wa 2015  yaliyopo ndani ya CCM.

Pia nafasi yake ya uwaziri anayehusika na mambo ya siasa, inatajwa kwamba imempa nafasi ya kuwa karibu na viongozi wengi wa CCM kuanzia ngazi ya taifa hadi wilayani.

Mjumbe wa Mkutano Mkuu, kutoka Mkoa wa Morogoro, Semindu Pawa alisema  kuwa ushindi wa kishindo wa Wassira unatokana na yeye wakati wa kiujieleza kumudu jukwaa.

Semindu Pawa ambaye ni Mbunge wa zamani wa Morogoro Kusini Mashariki alisema, Wassira alijua namna ya kutumia muda kwani alikuja na kauli ambayo iliwafurahisha wajumbe ya kueleza kuwa apewe nafasi hiyo ili apeleke kilio kwa Chadema.

Kauli ya Wassira
Alipoulizwa siri ya ushindi wake mkubwa ndani ya chama hicho, Wassira alisema: “Kilichonipa ushindi ni msimamo wangu wa kutotegemea kundi lolote na ukweli wangu ndani ya chama.”

Wassira alijinasibu kuwa yeye ni lulu ndani ya CCM na wakati wote amekuwa ni muumini wa ukweli huo bila ya kuyumba na kila mara amekuwa ni mjenga hoja za ukweli.

Alisema kuwa hata pale ambapo CCM kimekuwa kikitukanwa na wapinzani huwa anapeleka majibu ya hoja siyo matusi kama ambavyo wengine hufanya.

“Niliamini kuwa lazima nishinde na kweli ninawashukuru wajumbe kwa kuwa mimi ndiyo mwarobaini wa chama kwa wapinzani wetu, lazima tuwe pamoja na tutaendelea kuwa pamoja,” alisisitiza.

Makundi ndani ya chama hicho yanaelezwa kuwa yanatokana na mbio za kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Makundi haya ambayo tayari yamekigawa chama hicho, yamemfanya Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete kuonya kuwa yanaweza kukimaliza chama hicho ikiwa hayataondoshwa.

Wassira aliongoza katika uchaguzi huo na kuwashinda baadhi ya vigogo wakiwamo Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama.

CCM walipuana
Katika hatua nyingine, suala la ufisadi ndani ya CCM limeendelea kutikisa chama hicho, baada ya wajumbe wa mkutano mkuu kupendekeza kuwa makada wanaotuhumiwa kwa kashfa hiyo wavuliwe uanachama.

Vilevile, wanachama hao wamependekeza viongozi wanaotoa hadharani siri za Baraza la Mawaziri na kuikosoa hadharani Serikali waadhibiwe, wakieleza kuwa matendo hayo yanakiuka maadili ya kazi zao.

Wakitoa maazimio yaliyopatikana kutoka katika makundi yaliyokuwa yakijadili taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, iliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Wilson Mukama na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda juzi mchana, wajumbe hao walisema kuendelea kuwapo ndani ya chama hicho watu hao kunahatarisha usalama.

Akiwasilisha mapendekezo ya kundi la tatu, lililokuwa la Mikoa ya Dodoma, Iringa, Kilimanjaro, Tanga, Rukwa na Mjini Magharibi, Dk Damas Mkasa katika kundi lao wamependekeza makada wa CCM ambao wamekuwa wakikivuruga kwa kuendelea kupandikiza mpasuko waondoke.

“Wenye ndimi mbili wanaotengeneza migogoro ndani ya chama chetu waondolewe, ili CCM iendelee kushika hatamu ya nchi,” alisema Dk Mkasa, huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano ukumbi mzima.

Emmanuel Lwegenyeza akiwasilisha mapendekezo ya Mikoa ya Kigoma, Dar es Salaam, Kusini Unguja, Geita, Manyara na Shinyanga, alisema wajumbe katika kundi hilo wametaka wanachama wa CCM wanaotuhumiwa kwa kujihusisha na rushwa waondolewe.

“Wale ambao wanajihusisha na rushwa ndani ya chama wafukuzwe,” alisema.

Awali juzi jioni, wakichangia katika makundi wajumbe kutoka Mikoa ya Arusha, Tabora, Singida, Kusini Magharibi na Ruvuma, ambao walikuwa katika Ukumbi wa Kizota, kama wazee ndani ya chama hicho, walishindwa kuwadhibiti waachie ngazi na kuwakabidhi majukumu hayo vijana.

Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangala alisema, haiwezekani wazee waendelee kuitafuna nchi, huku Watanzania wakiendelea kuwa maskini.
“Haiwezekani wazee waendelee kuitafuna nchi na kujinufaisha wao wenyewe, kama wamechoka waondoke,” alisema.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa, mbunge huyo alishangaa kuona ndani ya chama hicho kuna makanda wanaotuhumiwa kwa ufisadi, lakini wamekuwa wakijitetea kuwa wasafi, huku wakiendelea kukigawa chama.

Mwakilishi wa kundi namba nne, Balozi Ali Mchumo alipendekeza kuwa ni wakati mwafaka kwa CCM kuwafagia watu wote ambao wamekuwa wakikihangaisha chama na kuwafanya wajumbe kuwa na makundi.

“Wanaomomonyoa chama watoswe kwa faida ya wengi, tumependekeza hata wale wanaovujisha siri za chama watoswe pia kuliko kuendelea kuwa nao,” alisema Mchumo.

Charles Mwakipesile ambaye alikuwa ni mwakilishi wa kundi namba tano alipendekeza kuwa watu wote ambao wamekuwa ni tatizo ndani ya chama waanze kwa kuonywa na wakirudia tena ndipo wafukuzwe.

Mwakipesile alisema ili chama kionekana kuwa ni bora, hakina budi kujipambanua kwa kuwafukuza pale itakapobidi wale ambao wanakipaka matope chama hicho.

Mwananchi

No comments:

Post a Comment