WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, November 3, 2012

Vurugu zimeigharimu Zanzibar - Maalim Seif

 
 
Na Hassan Hamad OMKR
 
 
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad ameelezea kuchukizwa kwake na vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani vilivyotokea hivi karibuni visiwani Zanzibar.
 
Amesema vitendo hivyo vimeigharimu Zanzibar katika Nyanja mbali mbali zikiwemo za kiuchumi, kisiasa na kijamii, sambamba na kuitia doa katika jamii ya kimataifa. 
 
Akihutubia mkutano wa hadhara wa chama hicho katika viwanja vya demokrasia Kibandamaiti mjini Zanzibar, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amevilaumu vyombo vya dola kwa kutochukuwa hatua zinazostahiki katika kudhibiti vitendo hivyo.
 
Amesema hatua zilizochukuliwa katika kurejesha amani baada ya kutokea kwa vurugu hizo hazikuwa muafaka, kwani zimekuwa zikiwadhalilisha na kuwanyanyasa wananchi wasiokuwa na hatia pamoja na kuhujumu mali zao.

Amesema yeye binafsi amechukizwa na kitendo cha kuuliwa kwa askari polisi katika eneo la Bububu, Koplo Said Abrahmani lakini bado serikali na vyombo vya dola vina jukumu la kulinda haki za raia kwa kuwasaka wanaohusika na tukio hilo, na sio kuwanyanyasa raia wasiokuwa na hatia.
 
“Nazungumza haya kwa unyonge sana leo, sikufikiria kuwa vitendo hivi vingetokea Zanzibar katika wakati huu tunaotekeleza maridhiano ndani ya serikali ya umoja wa kitaifa”,alieleza Maalim Seif na kuongeza,
“Sipendi kuisema serikali yangu na Rais wangu hadharani, lakini inanibidi niseme ‘Rais wangu Dkt Shein unatuangusha’ kwa kuwa wewe ndiye mwenye jukumu kubwa zaidi la kulinda amani ya nchi hii” alieleza.
 
Ametahadharisha kuwa huenda vitendo hivyo vimepangwa kuvuruga umoja wa Wazanzibari ambao umeiletea sifa kubwa Zanzibar, na kuwataka wananchi kutokubali kuingizwa katika mtego utakaopelekea kuvunjika kwa umoja na mshikamano uliopo miongoni mwa wananchi.
 
Katibu Mkuu huyo wa CUF alienda mbali zaidi kwa kudai kuwa vikundi vinavyolalamikiwa kufanya vurugu vikiwemo vya ‘Ubaya ubaya, Mbwa mwitu na Janjawid vilikuwepo kabla ya tukio hilo na kwamba vimetokana na kundi kubwa la vijana la JANJAWID lililoahidiwa kupewa ajira na Serikali.
 
Katika hatua nyengine Maalim Seif ameitaka Tume ya mabadiliko ya katiba kufanya kazi kwa uadilifu na kuheshimu mawazo ya wananchi wanayoyatoa bila ya kuonyesha upendeleo kwa baadhi ya watu au makundi fulani.
 
“Tume hii inaonekana kuanza kuwa na ‘bias’ kwa baadhi ya watu na makundi fulani, lakini tunamwambia Jaji Warioba tume yake iheshimu mawazo ya wananchi”, alitanabahisha.
 
Katika risala ya wanachama wa chama hicho kwa wilaya sita za Unguja iliyosomwa na Katibu Mtendaji wa vijana CUF taifa Khalifa Abdallah walitahadharisha juu ya uwezekano wa kuwepo kwa ajenda ya siri ya kuvuruga Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
 
Amesisitiza kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa bado inahitajika katika kupata ukombozi wa kweli wa Zanzibar, sambamba na kuendeleza umoja na mshikamano wa Wazanzibari.
 
Nae Kaimu wa Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bw. Salim Bimani amewasisitiza wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao juu ya mabadiliko ya katiba, na kuiomba Tume inayohusika na ukusanyaji wa maoni kuwapa fursa wananchi kutoa maoni yao kwa uwazi.
 
“Wananchi msikubali kuchokozeka, nendeni mkatoe maoni kwani hii ni fursa pekee ya kupata katiba tuitakayo” alisisitiza Bimani.

No comments:

Post a Comment