WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, November 14, 2012

Maalim Seif azindua ripoti ya idadi ya watu duniani


 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizindua Ripoti ya Idadi ya Watu Duniani kwa mwaka 2012, huko Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akionnyesha Ripoti ya Idadi ya Watu Duniani kwa mwaka 2012, baada ya kuizindua rasmi huko Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanziba Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na Mwakilishi Mkaazi wa UNFPA Tanzania Mariam Khan baada ya kuzindua Ripoti ya Idadi ya Watu Duniani kwa mwaka 2012, huko Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja

Waziri wa Afya Juma Duni Haji akiungana na kikundi cha Sanaa Zanzibar kutoa burudani ya ngoma ya Msewe wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Idadi ya Watu Duniani kwa mwaka 2012, huko Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.(Picha na Salmin Said, OMKR)

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kuwa jamii inahitaji kuelimishwa zaidi juu ya umuhimu wa uzazi wa mpango kwa maendeleo ya nchi na kutunza afya ya jamii hasa kwa akina mama na watoto.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad katika hafla ya uzinduzi wa Ripoti ya Idadi ya Watu Duniani ya mwaka 2012 iliyofanyika katika viwanja vya skuli ya Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambako alimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohd Shein.

Amesema jamii bado haijatoa umuhimu unaostahiki katika matumizi ya njia za uzazi wa mpango, hali inayopelekea kuwepo kwa ongezeko kubwa la watu ambalo huathiri harakati za maendeleo na afya ya jamii.
“Taarifa zinaonesha kwamba Zanzibar hivi sasa inakadiriwa kuwa na idadi ya watu 1.3 milioni, wanaoongezeka kwa kasi ya asilimia 3.1 kwa mwaka ambapo idadi ya watu katika kila kilomita moja ya mraba imefikia watu 496 mwaka 2011”, ilieleza sehemu ya hotuba hiyo ya Dkt. Shein iliyosomwa na Makamu wa Kwanza wa Rais.
Amefahamisha kuwa bado vifo vya mama wajawazito viko juu duniani lakini vimepungua kwa upande wa Tanzania na Zanzibar hasa kwa kina mama wenye umri mdogo na wanaokabiliwa na tatizo la umaskini.
“Kwa Tanzania katika mwaka 2004/05 idadi ya vifo ilikuwa 578 kwa kila akina mama waja wazito 100,000 na kupungua kidogo hadi kufikia vifo 454 mwaka 2010. Hata hivyo kwa Zanzibar vifo vya akina mama vimepungua kutoka vifo 473 mwaka 2006 hadi vifo 281 mwaka 2011, kwa kila kina mama 100,000 kwa takwimu za hospitali”, alifafanua.
Amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi za serikali katika kuimarisha huduma za afya kwa jamii ikiwa ni pamoja na kutoa chanjo za pepopunda na shurua, sambamba na kuimarisha huduma za afya ya uzazi katika hospitali mbali mbali.
Kwa upande wao wawakilishi wa Umoja wa Mataifa wameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuona umuhimu wa huduma ya uzazi na kuamua kutoa huduma hiyo bila ya malipo.
Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Idadi ya watu (UNFPA) Tanzania bibiMariam Khan amesema bado suala la uzazi wa mpango linakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na wanajamii kuona ugumu juu ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango.
Amefahamisha kuwa uzazi wa mpango ni muhimu katika kusaidia kukuza kipato cha wanafamilia, sambamba na kuwaendeleza watoto katika makuzi bora, na wito kwa jamii kutoa fursa zinazostahiki kwa akina mama na watoto ili kusaidia harakati za maendeleo kwa jamii.
Waziri wa Afya Mhe. Juma Duni Haji amesema wameamua kufanya uzinduzi huo katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, ili kutoa uelewa zaidi kwa wakaazi wa Mkoa huo ambao ni miongoni mwa mikoa inayofanya vibaya katika suala la uzazi wa mpango.
Amesema akinamama na watoto wanahitaji kulindwa kiafya, na kuwataka wazazi kushirikiana katika suala la malezi na makuzi ya watoto.
Mapema akitoa muhtasari wa ripoti hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Khamis Mussa amesema kimsingi ripoti hiyo imeelezea juu ya changamoto, faida na haki za binadamu katika uzazi wa mpango.
Amesema uzazi wa mpango ni miongoni kwa haki za binadamu lakini imeelekezwa zaidi kwenye haki za kifamilia, ili wanafamilia waweze kupanga juu ya idadi na umri wa kupishana kwa watoto, ili kuepuka mimba zisizotarajiwa.
“Inakisiwa kuwa kiasi cha mimba milioni 80 zinapatikana bila ya kutarajiwa duniani, huku nusu ya mimba hizo zikitolewa, jambo ambalo ni hatari nyengine katika uzazi”. Alidokeza Katibu Mkuu huyo.
Imewekwa na MAPARA

No comments:

Post a Comment