WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, March 8, 2013

Tunakata tawi tulokalia, tukianguka tunashangaa


MARA kadhaa huwa nikifikiria baadhi ya riwaya na hekaya tulizosoma tukiwa wadogo najiuliza iwapo walioziandika walijua wanatuandikia sisi au la, lakini jibu nililolipata hadi sasa, na ambalo lina chembe chembe nyingi zaidi za usahihi ni moja, nalo ni kwamba jamii nyingi duniani, na watu wengi duniani, wamewahi kufanya mambo ya kipuuzi na  ya kijuha  kabla yetu.

Hii inatufanya tukose sifa ya kuwa waanzilishi wa ujuha, kwani walikwisha kutangulia wengine ambao matendo yao ndiyo yaliyozalisha hekaya tulizosoma.

Baadhi ya hekaya hizo ziliibuliwa na matendo halisia ya watu waliowahi kuishi huko zamani, lakini nyingine zilikuwa ni hadithi za kubuni ingawaje zilitokana na matendo ya watu fulani katika jamii au jamii nzima. Lengo la hadithi hizi huwa ni kutoa mafundisho na maonyo kuhusu hasara za kufanya mambo ya hovyo na faida za kutenda mambo yanayopasa.

Hekaya moja imenijia katika kumbukumbu zangu, ingawaje sikumbuki iwapo ilitokana na Abou Nawas (Abunwasi, kama tulivyomjua sisi Waswahili) au Esopo au mtu mwingine aliyeishi kale zaidi.

(Kwa wale wasiomjua Abou Nawas, huyu alikuwa msomi, mwanafalsa, mshairi na mwanasayansi aliyeishi zama za Haroun al Rashid, Khalifa wa Baghdad (miaka 786-809) enzi za mwamko mkuu wa Kiislamu na Kiarabu katika fani nyingi za sayansi na utafiti.  Naye Esopo alikuwa mtumwa wa Uyunani aliyeishi miaka 600 kabla ya Yesu kuzaliwa).

Hadithi yenyewe ninayotaka kuieleza ni ile ya juha aliyekutwa akikata tawi la mti huku amelikalia. Alikuwa anatafuta kuni. Mpita njia mmoja aliyemuona alimtanabahisha kwamba angeanguka, lakini mtema kuni akaendelea na shughuli yake bila kumjali mpita njia.

Mtema kuni alipofanikiwa kulikata lile tawi, naye akadondoka chini, pu! Na kuchunika hapa na pale, lakini hakufa. Na bado akawa na nguvu kuondoka pale chini ya mti na kuelekea mjini kumsaka yule bwana aliyemuonya kwamba angedondoka.

Alipompata alimtaka amueleze ni vipi alijua kwamba angeanguka, na kwa sababu alikuwa amedhihirisha kipaji chake cha utabiri, sasa ni lazima amjulishe siku yake ya kufa itawadia lini.  Sikumbuki ni vipi walimaliza ugomvi wao huo, kwani kulikuwa na kutoelewana kwa aina yake.

Funzo tunalopata hapa, pamoja na kutuasa kwamba tusikate matawi tuliyoyakalia, ni kwamba katika mazingira mengine unaweza kujisababishia matatizo kwa kusema jambo lililo dhahiri ukiwaambia watu wasio na upeo wa kulitambua au wasiotaka kusumbua akili zao kidogo kulitafakari, au walio wavivu mno kulifikiria, au walio na shughuli nyingi muhimu kwao kuliko hilo unalowaambia.

Hivyo ndivyo ilivyotokea kuhusu kisa cha wanafunzi wa kidato cha NNE kushindwa vibaya katika mitihani ya mwaka jana. Wapita njia wengi wamekuwa wakiiambia serikali kwamba imekalia tawi inalolikata na itaanguka, lakini serikali, kwa miaka mingi, imekuwa ikiendelea kutema kuni bila kujali.

Ilipojali ni pale, katika awamu ya tatu, chini ya urais wa Benjamin Mkapa, ilipochukua hatua ya kuiadhibu HakiElimu ambayo ilikuwa ikiitanabahisha serikali kuhusu elimu ya hovyo iliyotolewa kwa watoto wa taifa hili.

Tawi ililokalia serikali lilikwisha kukatika kitambo, na serikali (pamoja na sisi sote) ilikwisha kuchubuka tangu zama, lakini ni safari hii ndipo serikali imetambua kwamba imedondoka, na imekwenda mjini kumtafuta yule aliyeitanabahisha. Sijui ni kwa nini inamtafuta huyu bwana, lakini inawezekana serikali nayo inataka iambiwe siku yake ya kufa, na ndiyo maana ikawafuata watema kuni walioionya.

Serikali imeunda tume ya kuitabiria mustakabali wake, na katika tume hiyo imewaingiza aliyekuwa mkurugenzi wa HakiElimu wakati shirika hilo likiadhibiwa kwa kuiambia serikali isikate tawi ililolikalia, na mbunge mmoja ambaye naye siku za hivi karibuni alitaka kupeleka bungeni hoja ya kuchunguza tabia ya serikali yetu ya kukata matawi iliyoyakalia, lakini akapuuzwa na hoja yake ikatupiliwa mbali siku chache kabla ya tawi kukatika na mti mzima kutikisika.

Masuala mengi ya kitaifa ni magumu, yana miingilio na mitokeo lukuki, yamejificha na yanahitaji weledi mkubwa kuyang’amua na kuyashughulikia kwa kiwango cha kuridhisha, na mara nyingi hukabidhiwa kwa wataalamu wenye weledi wa kiwango cha juu kuyakabili.

Hakuna kilichojificha katika kuporomoka kwa viwango vya elimu nchini humu; kila kitu kiko barabarani, ni sawa na kukalia tawi huku ukilikata;  hakuna sababu ya kuanza kuunda tume ya watu wale wale ambao wamekuwa wakikuambia ukweli ulio wazi nawe ukiwapuuza, kuwabeza na hata kuwaadhibu.
Binafsi, nilikuwa mwenyekiti wa bodi ya HakiElimu wakati ule na nilifadhaishwa sana na mwenendo wa serikali, kwani sikuamini kwamba wakuu wa serikali hawakujua kwamba walimu walikuwa dhaifu katika uwezo wa kufundisha, kwamba walikuwa hawana vitabu na nyenzo nyingine za kufundishia, kwamba walimu walikuwa hawalipwi stahili yao na kwamba malipo yao yalikuwa yanacheleweshwa bila sababu, na kadhalika.

Sikuweza kuamini kwamba watu waliopewa majukumu (tena kwa kuyaomba wenywe) ya kuendesha nchi walikuwa hawaoni matatizo yaliyo bayana kwa kila mwanajamii, kwani sikuelewa dhana ya kipofu kumuongoza mwenye macho. Leo wanashangaa, wanataharuki, wanababaika, wanaunda tume. Ili iweje hasa?

Tumeamua kuifanya elimu iwe ni jambo la kila familia kufanya kadri ya uwezo wake na uelewa wake wa maana ya elimu bora, na kwa maana hii serikali ilikwisha kujitoa katika kuratibu elimu ya watoto wa nchi hii. Kila mtu anajifanyia atakavyo. Basi, tusilalamike, na wala tusipoteze fedha za kodi za watu wetu kuendesha tume zisizokuwa na tija.

Kwa mara nyingine tena, nasema kwamba tumepotea, na tumepotea vibaya mno, na kwamba unapokuwa umepotea, nusura yako ya awali ni kutambua kwamba umepotea. Hili bado hatujalitambua.   

source: Raia Mwema: Jenerali Ulimwengu 

No comments:

Post a Comment