WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, March 8, 2013

Sumu ya udini imeanza kutuua



HOFU ya udini imetamalaki. Ni hofu ya kweli, maana, udini umeanza kuvuna roho zetu.
Kupitia safu hii nimepata kuandika mwaka mmoja uliopita, kuwa nchi yetu muda si mrefu itaingia katika mparaganyiko wa  kijamii utakaotokana na siasa kuchanganyika na dini. Tayari tumeshafika hapo. Inasikitisha.

Ndugu zangu, mbegu za chuki za kidini zimeshapandwa. Zimeanza sasa kuchipua. Kama tutatanguliza busara na hekima, basi, hatujachelewa. Tuna lazima ya kuing’oa na mizizi yake, miche yote ya udini iliyochipua, na ambayo, kuna hata baadhi ya wanasiasa, wanadiriki kuimwagilia maji ili isinyauke, kwamba ina manufaa kwao. Ni manufaa ya kisiasa.

Na hakika, ni busara na hekima, kwa mwanadamu kutambua na kuheshimu mamlaka iliyopo na zaidi, inayotokana na watu. Kutambua na kuheshimu  mamlaka inayotokana na sheria, kanuni na taratibu za  mahali husika, hivyo basi, mamlaka inayotokana na Katiba ya wakati huo. Na mwanadamu huyo,  midhari amefanya mawili hayo, ana lazima ya kufanya jambo la tatu; kuyaenzi mamlaka hayo.
Yawezekana  kabisa, kuwa katika kuyapata mamlaka hayo kukawa na mapungufu ya sheria, kanuni na taratibu. Lakini, hayo yasipewe nafasi ya kufanya mchakato wa kisiasa katika jamii ukakwama. Maana, siasa ina maana ya majadiliano endelevu. Ni majadiliano yasiyo koma. Muhimu katika siasa ni kubaki katika meza ya majadiliano.

Tunapokandamiza kwa makusudi mkondo wa siasa usichukue nafasi yake, na hapa pia kwa maana ya kukandamiza siasa za upinzani, basi, tunaruhusu uwepo wa ombwe la kisiasa. Hivyo, nguvu hasi za kijamii hupenya kwa urahisi kuziba ombwe hilo. Ni pamoja na makundi ya kidini yenye misimamo mikali na ya hatari kwa amani ya taifa.

Maana, katika nchi yetu tumeanza kuziona dalili mbaya za siasa kuchanganyika na dini. Na Uchaguzi Mkuu uliopita umetoa ishara mbaya. Ishara za nchi yetu kukumbwa na siasa zilizochanganyika na  udini .
Watanzania tuliwashuhudi baadhi ya viongozi wa kidini; Uislamu na Ukristo, wakitumia nyumba za ibada, si kwa kazi ya kiroho, kazi ya kuhubiri yaliyo mema kwa mwanadamu, bali viongozi hao wa kidini wamefanya kazi ya siasa. Kazi ya kuhutubia mambo ya siasa na kutoa maelekezo ya kisiasa ya moja kwa moja. 
Hayo yamefanyika misikitini na makanisani, ni hatari. Jambo hili linaiweka rehani amani ya nchi yetu. Linahatarisha Umoja wetu wa Kitaifa. Maana, makanisani na misikitini wanakusanyika Watanzania wa itikadi tofauti za kisiasa, na wengine ni watoto, hawajawa tayari kupokea hotuba za kisiasa, bali watoto wako tayari kupokea mahubiri na mafundisho ya kiroho.

Tumefika mahala, kiongozi wa kidini anatamka kwenye nyumba ya ibada;  “Msiwachague wale wenye kutoa kofia na fulana”. Mwingine anatamka; “ Msiwachue watakaotuletea vita”.   Katika mifano hiyo miwili ya kauli ni dhahiri, kuwa bila kutaja ni akina nani wenye kutoa  kofia na fulana waumini wameshawajua ni akina nani. Na bila kuwataja hao ‘watakaotuletea vita’ waumini wameshawajua ni akina nani. Hayo mawili hayawezekani yakawa ni mafumbo magumu kwa waumini kutoka kwa viongozi wa dini.

Hapo inapandikizwa sumu ya chuki miongoni mwa waumini, maana, waumini  hawana itikadi zinazofanana. Hapo  viongozi wa dini wanashiriki kutenda maovu. Kuwagawa wananchi katika misingi ya udini.  Maana, nao , kwa mgongo wa imani, wanashiriki kutoa hukumu bila ya wenye kuhukumiwa kupewa nafasi ya kujitetetea.

 Wahenga wetu walisema” Kamba ukatikia pabovu”. Kamwe huwezi kuwavuruga Watanzania na kuwafanya wachinjane kwa sababu za kudai kuna upendeleo wa ukabila au wa kisiasa. Nchi hii ina makabila zaidi ya 125 na utitiri wa vyama vya siasa.

Mahala ambapo unaweza  kuwagawa Watanzania na hata kufanikiwa wachinjane ni kwenye masuala ya imani, ni kwenye dini. Tusikubali dini iwe ndiwe penye ubovu kwenye kamba inayotuunganisha Watanzania.
Hakika, ni wajibu wetu wa kizalendo kuyazungumza  haya kinagaubaga, kuwa hapa kuna tatizo linalotunyemelea. Tatizo la udini. Maana, Watanzania sisi tuna hulka ya ajabu kidogo. Wakati mwingine tunaamini kuwa kama jambo unalinyamazia, basi halipo hata kama lipo. Tatizo unaliona, lakini unachofanya ni kunyamaza kimya tu. Kinachofanyika hapo ni kufagilia tatizo chini ya jamvi badala ya kufanya jitihada ya kuliondoa.

Na waumini wanaamini, kuwa Shehe haongopi na Padri au Mchungaji vivyo hivyo.  Inakuwaje basi, pale Shehe, Mchungaji au Padri anapotenda dhambi ya kusema uongo? Dhambi ya kufanya maonevu? Waumini, kama vile wanakondoo, watakuwa wamekosa  wachungaji.  Na hao viongozi wa kidini watakuwa ni  sehemu ya kuchochea machafuko katika jamii.
Naam, sasa ni dhahiri, kuwa dini imejichanganya na siasa. Na huu si mseto mwema kwa nchi yetu.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

No comments:

Post a Comment