WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, March 13, 2013

Kikwete kawa muumini wa historia mpya Tanganyika?

Hayo ndiyo maisha ya Watanzania na hiyo ndiyo Tanzania yenye amani na utulivu tuliyozaliwa, kukua na kuishi.  Nawasihi sana Watanzania wenzangu, tuienzi na kuidumisha tunu hii waliyotujengea mababu zetu. – Kikwete (Hotuba ya Mwisho wa Mwezi Februari, 2013)

KUNA kila dalili kuwa Rais Jakaya Kikwete amekuwa muumini wa propaganda ya historia mpya ya Tanganyika ambayo imekuwa ikienezwa chini kwa chini na ambayo imepata mashabiki.

Kwa muda mrefu sasa katika hotuba zake mbalimbali Rais Kikwete amekuwa akijitahidi ama kujilinganisha na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na kumuonesha kuwa yeye Kikwete amefanya mengi kuliko Nyerere au kwa namna moja au nyingine kuanza taratibu kulifuta jina la Nyerere na mchango wake wa pekee.
 
Anaamini kafanya mengi kuliko Nyerere
Mojawapo ya mambo ambayo yanatokea kwenye utawala wowote ambao umebakia na muhula mmoja tu wa kuongoza ni kujaribu kutengeneza kumbukumbu (legacy).

Karibu marais wote katika nchi za kidemokrasia wanapofikia miaka michache kabla ya muhula wao kwisha hujaribu kufanya mambo ambayo jamii zinazokuja nyuma zitawakumbuka. Sasa hivi Rais Kikwete yuko katika wakati kama huo ambapo anajaribu sana kuhakikisha kuwa vizazi vijavyo vitamkumbuka kwa mengi.

Yeye mwenyewe anaamini kuwa amefanya mambo mengi sana ya maendeleo na amejitamba hivyo mara kadhaa akijilinganisha na viongozi waliotangulia.
Katika hotuba yake wakati wa maadhimisho ya kuzaliwa CCM yaliyofanyika kitaifa mkoani Kigoma mwezi mmoja uliopita Rais Kikwete alitangaza kuwa anataka pale atakapoondoka madarakani akumbukwe kama “bwana maendeleo”. Sababu ni kuwa anaamini kuwa utawala wake umeleta maendeleo mengi kuliko wengine waliomtangulia.

Ukimuuliza mtu anayeamini nadharia hii utaona kuwa wote watakuonesha ‘wingi’ wa vitu ambavyo vimefanywa na utawala wa RaisKikwete. Mrundikano wa magari, majengo mapya, barabara, hospitali, vyuo, shule na vingine vingi. Watu wanaoamini maendeleo kama ‘ongezeko la kiasi’ watakimbia kwa haraka kuonesha “vitu” kama dalili ya maendeleo. Hawa husema “mbona wakati wa Nyerere hatukuwa na x, y, na z” na kwa vile hivyo “x, y, na z” vipo chini ya utawala wa Kikwete basi Kikwete kafanya mengi kuliko Nyerere.

Sasa kuna ukweli wa aina yake na usiopingika katika hili. Hata hivyo ni ukweli ambao unavutia watu wasiofikiri. Nyerere ameanza kuongoza Tanzania akiwa na madaktari 12 na wahandisi wawili wazalendo. Nyerere alipoanza kuongoza hakukuwa na chuo kikuu cha Tanganyika, walitegemea Chuo Kikuu cha Makerere ambacho sehemu ya Tanzania ilikuwa ni tawi lake.

Wakati Nyerere anaanza hivyo hakuna rasilimali watu ambazo Kikwete leo anazo. Lakini matokeo yake ni tofauti. Wakati Nyerere anaondoka madarakani uwezo wa kujua kusoma na kuandika ulikuwa umefikia asilimia 91 hivi; leo Kikwete pamoja na shule, vyuo, walimu na misaada lukuki wanaojua kusoma na kuandika ni kama asilimia 69 hivi! Na cha kuudhi zaidi (kama kuna namna ya kuudhika zaidi) ni kuwa pamoja na mabilioni yote ambayo Kikwete ameyatumia kwenye elimu leo hii watoto wetu wanafeli vibaya zaidi kuliko wakati wowote tangu tupate uhuru! Ati bwana maendeleo!

Lakini kubwa zaidi ni hili la historia mpya ya Tanganyika. Katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Februari ambayo seemu yake nimeinukuu hapo juu Kikwete anajaribu kufanya kiile ambacho kimekuwa kinafanywa na baadhi ya watu sasa hivi cha kuandika upya historiaya Tanganyika ambayo inapunguza, kudharau na kwa namna Fulani kukejeli mchango wa kipekee wa Baba waTaifa MwalimuNyerere.
 
Je, amani yetu ililetwa na mababu?
Katika simulizi hii mpya amani tunayoiona sasa hivi haikutokana na juhudi za kipekee na mchango wa kipekee wa Nyerere.

Kumhusisha Nyerere na amani hii ni kumpa sifa asiyostahili. Hivyo, katika simulizi hili jipya Nyerere “aliikuta” amani hii na hakufanya lolote lile la kipekee la kuhakikisha kuwa katika Tanganyika mpya amani itamalaki. Na wapo wenye kuamini hili.
 
Uamuzi wa busara
Bahati mbaya sana historia ina ushahidi wa tofauti sana. Matukio makubwa kadhaa wakati wa uongozi wa Mwalimu yalichangia sana kuhakikisha kuwa amani katika Tanzania inadumu. Kwanza ni ule uamuzi wa kura tatu wa mwaka 1958.

Huu ulikuwa ni mmoja wa uamuzi wa kimkakati ambao ulibadilisha kabisa mwelekeo wa siasa za nchi yetu. Uamuzi huu wa busara ulihakikisha kuwa TANU inakuwa na nafasi ya pekee ya kushinda uchaguzi ule.
Hata hivyo nyuma ya mkakati ule ilikuwapo nia ya wazi ya kuvuruga mpango wa kundi dogo la baadhi ya viongozi ambao walikuwa wanataka kuingiza udini katika siasa.
 
Kujiuzulu waziri mkuu
Mojawapo ya uamuzi wa kijasiri kabisa wa Baba wa Taifa na ambao ulichangia sana kuongeza umoja, amani na utulivu wa nchini pale alipoamua kujiuzulu uwaziri mkuu ili vkuijenga TANU.

Ikumbukwe kuwa Nyerere alishazunguka karibu Tanganyika yote kabla ya Uhuru kueneza TANU lakini mara hii ya pili Nyerere alikuwa anazunguka kuwapa Watanganyika nafasi ya kujitambua kama taifa moja na watu wamoja chini ya TANU. Ilikuwa ni muda wa kujenga utaifa zaidi – wakoloni hawakutuachia hisia ya utaifa bali nchi moja yenye makabila mbalimbali na hali mbalimbali za maisha.
 
Misukosuko ya miaka kumi ya kwanza
Kama kuna wakati mgumu katika historia ya nchi yetu ni hii miaka 10 ya kwanza. Wanaosema Nyerere hakuwa na nafasi ya pekee katika kuleta na kudumisha amani yetu hawajui historia yetu. Wamezoea mazungumzo ya barazani. Ndani ya miaka 10 ya kwanza ya Uhuru, Nyerere alikumbana na changamoto ambazo hakuna rais mwingine baada yake amekutana nazo. HAKUNA. Baadhi ya changamoto hizo:
  • Baa la Njaa (mara tu baada ya Uhuru)
  • Mvurugano wa kidini na kuvunjika kwa EAMWS
  • Kuvunja baraza la machifu wa kikabila
  • Maasi ya jeshi
  • Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano
  • Siasa za kimataifa za vita baridi
  • Kuendelea kwa ukoloni kusini mwa Afrika
  • Njama za kuipindua serikali
  • Mgongano ndani ya TANU
Lakini ni kutokana uongozi hodari wa hekima wa Baba wa Taifa Tanzania ikapita salama. Wapo waliojeruhiwa, wapo walioumizwa lakini taifa letu likapita salama. Na hoja inaweza kujengwa kuwa hata miaka kumi ya pili (1971-1981) ilikuja na changamoto za aina yake ambazo Kikwete hajazipitia na zote zilikuwa zinahusiana na amani na utulivu na usalama wa Tanzania. Leo hii wengine tunajiuliza hivi Kikwete angekuwa rais katika kipindi cha kwanza au cha pili cha miaka kumi, mtu ambaye hata hajui kwa nini Tanzania ni masikini kweli Tanzania ingekuwapo?

Ni kwa sababu hiyo Watanzania wanapaswa kuangalia upya jaribio la viongozi wachache kuficha udhaifu wao kwa kuubeza na kuukejeli kiaina uongozi adimu wa Baba wa Taifa. Watanzania wawasikilize jinsi wanavyojaribu kupuuzia mchango huo wakiamini kwa kufanya hivyo wanawaridhisha (appease) mashabiki wao.

Uzuri ni kuwa historia itasimama kamili kuonesha mchango wa pekee, uliotukuka, na usiona mfano wa Baba wa Taifa katika kuleta, kulinda, na kudumisha amani.

Amani hii inapovunjwa leo hii, wakulaumiwa ni hawa hawa. Hawawezi kukwepa kwani walipewa nchi salama salmini sasa inaweza kuvunjika mikononi mwao, na wananchi wake wakibaki majeruhi wa siasa dhaifu zilizoshindwa.

source: Raia Mwema: Lula wa Ndali Mwananzela

No comments:

Post a Comment