WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, March 27, 2013

Njiani Kwenda Kwa Rais!"


581402 10200289233726253 1382026267 n 5ffb3

Ndugu zangu,
Leo mchana wakati nikipata kikombe changu cha chai na andazi pale Tea Room ya kona ya Jamhuri na Morogoro nilipitia kitabu cha mwandishi wa Kisweden Stig Holmqvist kiitwacho; Pa Vag Till Presidenten- Njiani kwenda kwa Rais. Mwandishi kwa lugha ya Kisweden anaipitia historia yetu huku mwenyewe akiwa mshiriki kwenye simulizi yake. Wakati nikimsoma Holmqvist nikatafakari ujio wa Xi Jinping, Rais wa China hapa kwetu Tanzania.Mwandishi anatukumbusha pia mahusiano ya Tanzania na China na Soviet Union wakati ule wa
Vita Baridi ( Kiitikadi) vya Dunia. Mahusiano ambayo yalimweka Julius Nyerere kwenye wakati mgumu sana.
Naam, Wachina wamerudi tena, safari hii si kiitikadi, bali kiuchumi zaidi. Wakati ule wa kiitikadi Tanzania ilikuwa mshiriki muhimu kwenye harakati. Na sasa kwenye Vita Baridi ya Kiuchumi, ujio wa Wachina Afrika unaofuatiliwa kwa karibu na Marekani na Uingereza.
Si ajabu nilimwona Balozi wa Marekani siku ile Xi Jinping alipotoa hotuba ya mwelekeo wa sera za China kwa Afrika akiwa Dar. Naam, Wamarekani wanafuatilia.

Na nPyo ilivyokuwa miaka ya 60 hadi 70. Mwaka 1964 ulikuwa ni mwaka mgumu sana kwa uongozi wa Julius Nyerere kuliko wakati mwingine wowote. Kulikuwa na matukio makubwa yaliyomtikisa Julius Nyerere na Tanzania kama taifa changa.

Mapinduzi ya Januari 12, Zanzibar na Army Mutiny ( Uasi wa jeshi) wa Januari 20, 1964.

Wachina na WaCuba waliingia kwa kasi Zanzibar mara baada ya Mapinduzi. Hali hii iliwatisha Wamarekani. Ikaja taarifa ya kupandikizwa ya kiintelijensia. Ni katika miezi hiyo hiyo. Kwamba Marekani na Uingereza wanapanga njama za kumwangusha Karume. Nyerere akaridhia Karume amfukuze Balozi Mdogo wa Marekani kutoka Unguja.

Julius Nyerere akagundua baadae kuwa alikosea. Akaenda mwenyewe kwa Balozi wa Marekani kufafanua kilichotokea.

Kwenye telegramu ambayo Balozi wa Marekani aliituma White House na CIA Januari 1965 , Balozi huyo, Bw. Leonhart anauelezea mkutano wake na Julius kwa kusema, " Haukuwa mzuri...."

" Nyerere bekglagade djupt att han kunde inte andra sitt beslut"- ( Swedish) Kwamba Nyerere alisikitika lakini hakuwa tayari kubadili uamuzi wake ( Kumfukuza Balozi mdogo wa USA) ( Pa Vag Mot Presidenten, Ukurasa wa 196)

Mengine yaliyojiri kwenye mkutano wa Julius Nyerere na Balozi Leonhart ni vema yakabaki kwenye maandishi ya mwandishi Holmqvist na kwa lugha yake, maana, kuyaweka bayana hapa haiwezi kuwa ni kwa maslahi ya taifa letu.

Nikipata muda nitawasimulia mengine kutoka kwenye kitabu hiki.

Maggid Mjengwa,
Dar es salaam
0788 111 765
http://mjengwablog.co.tz/

No comments:

Post a Comment