WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, March 14, 2013

Changamoto zinazowakabili Uhuru na Ruto

Rais mteule wa Kenya Uhuru Kenyatta 

TULIAHIDI kwamba wiki hii tutaangalia athari za urais wa Uhuru Kenyatta. Kwa kutangazwa Rais mteule wa Kenya Uhuru na Naibu wake, William Ruto wamefaulu hadi sasa kukikiuka kiunzi kimoja. Kuna vizingiti vingine viwili vinavyowakabili ambavyo lazima wavidakie. Vyote ni vya kisheria. 

Cha kwanza ni kesi mbili zinazofikishwa Jumatano hii mbele ya Mahakama ya Juu ya Kenya (Supreme Court) zenye kuitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iyabatilishe matokeo iliyoyatoa usiku wa kuamkia Jumamosi na yaliyoonyesha kwamba walioshinda uchaguzi wa urais ni Uhuru na Ruto.

Moja ya kesi hizo imefikishwa mahakamani na Muungano wa CORD wenye kuongozwa na Raila Odinga, kiongozi wa ODM, aliyekua mpinzani mkuu wa Uhuru katika uchaguzi wa urais. Ya pili imewasilishwa mahakamani na asasi ya kiraia. Kesi hizo lazima zisikilizwe siku 14 baada ya mashtaka kufunguliwa.

Hizo zitakua kesi za mwanzo zenye uzito kuwahi kusikilizwa na Mahakama ya Juu tangu Mahakama hiyo iundwe miaka miwili iliyopita.

Kesi hizo zitasikilizwa na majaji watano.  Majaji hao wakiamua kwamba kweli palifanyika mizungu na ghiliba nyingine katika uendeshwaji wa uchaguzi na hasa katika kuhesabu kura basi Mahakama ya Juu yanaweza yakaubatilisha uchaguzi wa urais. 
Ukifikiwa uamuzi huo basi uchaguzi wa urais itabidi ufanywe upya katika muda wa  siku 60 kutoka siku itapotolewa hukumu hiyo.

La majaji wakiamua kwamba uchaguzi uliendeshwa kihalali basi Uhuru na Ruto watabidi walishwe viapo vya kuzishika nyadhifa zao katika muda wa siku 14 kutoka siku waliotangazwa kuwa ndio washindi.

Wafuasi wa Raila wamegawika kuhusu kesi hiyo. Kuna wenye kuunga mkono kufunguliwa mashtaka hayo lakini wapo pia wenye kuhisi ya kwamba lau CORD itashindwa mahakamani basi Raila anaweza akajiharibia jina lake. Wengine wanasema kwamba wao wamekwishakubali kwamba upande wao umeshindwa na hawataki taifa ligubikwe na hali ya wasiwasi.

Lakini ilivyo ni kwamba Raila aliyezoea kumpiga madongo Uhuru na kumsengenya kwa mafumbo sasa ameazimia kummaliza mahakamani.

Kizingiti cha pili kinachowakabili akina Uhuru na Ruto ni kesi yao mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) yenye makao yake mjini Hague, Uholanzi.
La ajabu ni kwamba kesi hiyo, kinyume na ilivyotarajiwa, ni moja ya mambo yaliochangia kuwajenga washtakiwa hao wawili waliokua wagombea wenza katika uchaguzi uliopita.

Kesi hiyo pia ndio iliyowafanya wazidi kushirikiana. Chambilecho ubeti mmoja wa kale hivi sasa Uhuru na Ruto wamekua:
‘Ni chanda na pete
Ulimi na mate
Uta na upote…’

Hivi karibuni kuwamekuwako dalili kwamba kesi dhidi ya Uhuru imekua ikidhoufika na ndio maana haikua ajabu kwamba Mahakama ya ICC siku ya Jumatatu iliyafuta mashtaka yote aliokuwa akishtakiwa Bwana Francis Muthaura, katibu wa zamani wa baraza la mawaziri, aliyeshtakiwa pamoja na Uhuru.
Kabla ya uchaguzi wa Machi 4 tulikuwa hatwishi kuambiwa kwamba kesi hizo zilizo mbele ya Mahakama ya ICC zitauhatarisha uchaguzi usiweze hata kufanyika.

Pili tukiambiwa kwamba kesi hizo zitakua suala kuu la kujadiliwa kwenye kampeni za uchaguzi.Yote hayo mawili hayakutokea.

Hata hivyo kwa vile Uhuru na Ruto wameshatangazwa na Tume ya Uchaguzi kuwa ndio washindi wa kinyanganyiro cha urais lazima tukae kitako na kuutafakari mustakbali wa urais wa waheshimiwa hao wawili wanaokabiliwa na mashtaka ya jinai.

Kesi zote hizo mbili hivi sasa zimeahirishwa; ya Ruto inatazamiwa kusikilizwa Mei na ya Uhuru mwezi Julai.
Wawili hao wamekua wakishikilia kuwa hawana nia ya kuzikwepa kesi za Hague.Kwa hivyo wanasema watakua wakifunga safari kwenda Hague kuhudhuria vikao vya kesi kila pale wanapohitajika kwenda huko.
Mji wa Hague uko masafa ya kilomita 10,542.1 kutoka Nairobi kwa safari ya gari au kilomita 6,676 kwa safari ya ndege. Safari ya gari kati ya miji hiyo ni ya muda wa takriban siku sita na saa tano wakati safari ya ndege ni ya saa nane na nusu.

Urais na umakamu wake ni kazi. Ni kazi ya kila siku (haina mapumziko ya kawaida ya Ijumaa au Jumapili) na saa zote wenye  nyadhifa hizo wanatakiwa wawe hadhir na tayari kukabiliana na changamoto yoyote itayozuka wakati wowote ule naiwe mchana naiwe usiku.

Ndipo watu wakawa wanajiuliza:“Uhuru na Ruto watawezaje kutekeleza majukumu ya kazi zao endapo watakua hawapo nchini na wapo mahakamani Hague wakijibu mashtaka?”

Miongoni mwa majukumu ya Rais na naibu wake ni kuhudhuria na kuongoza vikao vya baraza la mawaziri ambalo kwa kawaida linakutana mara moja kwa wiki. Sasa ikiwa Rais na naibu wake watakua wanakosekana mara kwa mara katika vikao hivyo serikali itakua inaendeshwa bila ya viongozi wake wakuu na pingine hata bila ya dira.

Isitoshe, baraza la mawaziri kadhalika huwa na kamati ndogo kadhaa zenye jukumu la kulishauri baraza zima pamoja na Rais.  Bila ya shaka patazuka mushkili katika kazi za kamati hizo endapo Rais atakua anakosekana kwa vipindi vya muda mrefu katika vikao vya baraza la mawaziri.  Tusisahau kwamba yeye Rais ndiye moyo wa baraza hilo, ni kiungo muhimu cha shughuli zote za baraza la mawaziri.

Halafu kuna suala la majeshi.  Rais ni amiri jeshi wa majeshi yote ya Kenya na ndiye mwenye mamlaka ya uongozi wa majeshi hayo.  Kwa sasa majeshi ya Kenya yanakabiliwa na changamoto kubwa za kiusalama isizowahi kuzikabili kabla. 

Hali ya usalama ndani ya nchi ni ya wasiwasi na majeshi ya Kenya yamo vitani kupambana na magaidi wa Al-Shabaab nchini Somalia.

Katika nyanja hiyo ya usalama ni Rais pekee mwenye uwezo wa kikatiba wa kutangaza hali ya hatari nchini.  Na ni yeye pekee mwenye uwezo wa kutangaza vita. Taarifa zote nyeti za usalama wa taifa zinamfikia yeye.
Naibu wa Rais, kwa upande wake, ndiye mwenyekiti wa kamati ya usalama ya baraza la mawaziri.  Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Waziri wa Usalama wa Ndani ya Nchi, Waziri wa Ulinzi, Waziri wa Sheria na Shughuli za Kikatiba, Waziri wa Fedha, Waziri wa Mambo ya Nje na Mkuu wa Idara ya Utumishi wa Umma. 

Kamati hiyo ndio yenye kumshauri Rais kuhusu mambo ya usalama na ndio yenye kujitwika jukumu la kuhakikisha usalama wa taifa.

Hivyo, hali ya usalama nchini huenda ikasambaratika endapo Rais au naibu wake atakua anatakikana awe anakwenda Hague kila mara kwa sababu ya kesi. Wote wanahitajika nchini kwa sababu wote wana majukumu nyeti kuhusika na usalama na ulinzi wa taifa.

Pamoja na hayo niliyokwishayataja kuna shughuli nyingi nyingine ambazo pia zinamhitaji Rais na naibu wake wawe watu wasiobabaishwa na mambo kama ya kesi ya ICC.

Safari za mara kwa mara za kwenda Hague kuhudhuria vikao vya kesi bila ya shaka zitaziathiri vibaya kazi za Rais na naibu wake. 

Aidha, kazi hizo zitazidi kutatanika kwa vile viongozi hao wawili watakua si makini.   Wanatakiwa wawe na akili zilizotulia kushughulikia mambo ya kitaifa na sio mara kwa mara wawe wana wahka kuhusu yanayotokea katika mahakama ya ICC na nini yatakuwa matokeo ya kesi yao na majaaliwa yao. 

Jambo jingine litaloweza kuwatia mtegoni ni msimamo wa nchi nyingine. Nchi jirani za Kenya kwa jumla hazina tatizo na kuchaguliwa kwa Uhuru. Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari Uhuru anakubalika zaidi miongoni mwa marais wa Afrika ya Mashariki na wa nchi za Maziwa Makuu kushinda Raila. 

Tunajua kwamba kuna kiongozi mmoja mkuu wa eneo hili ambaye hata kumuona Raila hataki seuze kuwa na maingiliano naye.  Na hawa ni watu ambao zamani walikuwa wakisikilizana.  Kwa hivyo, kwa upande wa majirani Uhuru hatokuwa na tatizo.

Tatizo atalipata kutoka kwa baadhi ya nchi za Magharibi — hasa Uingereza, Marekani na Jumuiya ya Ulaya. Nchi hizi zimedhamiria kumtia adabu kwa msimamo wake wa kutokubali kuyumbishwa asisimame katika uchaguzi uliopita.  Hii ndio sababu inayowafanya wengi watie shaka kwamba nchi hizo zikitaka Raila asipambane na mgombea atayeweza kumshinda.

Na haya ndio yanayowafanya baadhi ya wachanganuzi wa siasa za Kenya waamini kwamba madola ya Magharibi tangu mwanzo yakimtaka Raila awe rais mpya wa Kenya.  Wengine wamefika hadi hata ya kumuelezea Raila kuwa ni ‘kibaraka’ wa madola ya Magharibi yakiwa pamoja na Israel.Swali linalozidi kuulizwa ni: ‘Nini ambacho Raila ameiziahidi nchi za Magharibi na kwa nini?’

Tunavyoelewa ni kwamba katika miaka miwili mitatu hivi iliyopita mahusiano kati ya nchi za Magharibi na Kenya yaliporomoka wakati serikali ya Rais Mwai Kibaki ilipoigeukia China kwa misaada, hasa katika ujenzi wa miundombinu.Ilifika hadi hata balozi wa Ufaransa akabidi alalamike hadharani kwamba anapata shida kubwa kupangiwa muda wa kuonana na Kibaki.

Kabla ya uchaguzi baadhi ya madola ya Magharibi yalitoa vitisho vilivyotafsiriwa kuwa ni jaribio lao la kuwataka wapigaji kura wa Kenya wasimchague Uhuru na mwenza wake. Hayakusema kama yataiwekea Kenya vikwazo lakini wengi walichukulia kwamba hayo ndio yaliokusudiwa.
Mfano wa Sudan na wa Rais wake Omar Hassan al Bashir ulitolewa.  Kwa mtazamo wangu hizo ni ndaro tu za madola ya Magharibi.  Kenya si Sudan.

Nchi za Magharibi na hasa Uingereza zina maslahi makubwa ya kiuchumi nchini Kenya na hazitotaka rasilmali zao na maslahi yao yadhurike kwa hatua zao dhidi ya Kenya kwa sababu viongozi wake ni Uhuru na Ruto.

Wala Kenya si Iran kwani tunajua sababu hasa inayoyafanya madola ya Magharibi yaziandame nchi hizo mbili.  Serikali ya Kenya haina Uislamu unaoyataabisha madola hayo katika Iran na Sudan.

source: Raia Mwema:  Ahmed Rajab

No comments:

Post a Comment