WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, March 27, 2013

Kwa nini watudanganye kwamba watoto wanapata elimu huku wakipata mimba au UKIMWI badala yake?


                                               Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
                                                                          Uzitoni Street,
                                                                                     Bongo.

Mpenzi wangu, mpenzi wangu,

Mbona uko mbali nami?  Nakuhitaji sana mpenzi, nakuwazia sana, sina raha tukiwa mbalimbali hivi.  Napenda kujua kama u mzima kila wakati na kusikia sauti yako nzito ikinijali kama unavyonijali kila siku.  Nakumiss mpenzi wangu ... mpaka namwaga hata ung’eng’e kwa ajili yako.

Pili, mwandani wangu wa maisha, naomba unisaidie kitu kimoja.  Si kuna yule binamu yangu anasoma shule moja ya ukata huko.  Na ili asome amelazimika kupanga karibu na shule.  Sasa baada ya kumsikiliza mgeni wa bosi wiki hii, nashindwa hata kulala, na nikilala naamka natoa jasho kutokana na jinamizi zinavyonizonga.

Kisa chenyewe ni hicho.  Wakati bosi anabugia supu yake asubuhi asubuhi kabla ya kujipeleka kazini, tukasikia hodi.  Kumbe ni mama mmoja anayetoka jimboni kwa bosi.  Baada ya kumwamkia bosi kwa heshima anazostahili mheshimiwa, bosi akamwambia ajieleze haraka maana anaenda kwenye mikutano.  Basi mama akaanza.

‘Samahani kukusumbua mheshimiwa lakini nimeshindwa kuvumilia.  Tumesisitiziwa umuhimu wa elimu hadi tunafanyiwa msako wa nyumba hadi nyumba kama vile sisi ni wahalifu.’
‘Ndiyo.  Lazima mpeleke watoto wenyewe shuleni.  Mtukufu Rais amesema’

‘Sijabisha.  Lakini kwa nini tunatakiwa kupeleka watoto wetu shuleni?’
Bosi akajibu kwa dharau.
‘We mama usipoteze muda wangu.  Wanaenda shule ili wapate elimu.’
‘Ahaa.  Sawa kabisa.  Na kama shule haitoi elimu?’
‘Una maana gani?  Kama shule si shule, elimu itapatikana wapi?  Kwa nini nimpeleke mwanangu mdomoni mwa mamba?’
‘Mbona sikuelewi.’

‘Unajua mwanangu ametongozwa na walimu wangapi?  Walimu wenyewe wote ni vodafasta ...’
‘We!  Acha kutumia lugha ya namna hii.  Hata mtukufu Rais ...’

‘Amekataza lakini ndio ukweli wenyewe.  Bila shaka wako wanaojua kufundisha lakini katika shule ya mwanangu hakuna.  Na ufasta wao ni katika kutongoza tu.’
‘Basi ni rahisi sana.  Ni kiasi cha kuwashtaki kwa mwalimu mkuu.’

‘Usinichekeshe mheshimiwa.   Yeye ndiye kiongozi, na kwa mujibu wa mwanangu wanajua wanafunzi watatu ambao anatembea nao.’
Lo, mpenzi, hapo bosi akabaki kimya kidogo.  Kumbe mama ndio kwanza anaanza.

‘Lakini si hivyo tu, mheshimiwa.  Naomba nikupe tu kwa muhtasari nilivyoambiwa na wanafunzi wenyewe nilipoamua kufuatilia nilivyoambiwa na mwanangu.  Kwanza wanafunzi wengi wanalazimika kupanga katika nyumba za watu binafsi hali ambayo ni hatari sana.  Makazi wanayopanga wanafunzi hawa si salama, si bora, si sanifu na wala hayatoi mwanya muafaka kwa wanafunzi kujiendeleza. Mzazi anapompangishia mtoto chumba, kutokana na maisha kuwa magumu anashindwa kumtimizia kila kitu na hivyo ananunua unga, dagaa, mafuta ya taa basi.

Wanafunzi wengi wanalala chini, kwa kutandika mifuko ya ‘salfet’ ama gunia. Shida kubwa inakuja siku za mvua ambapo wakati mwingine nyumba huvuja na maji kuwaingilia, ama maji ya mvua kupenya na kuingia ndani, na kuna kipindi cha sisimizi na wadudu. Nilipoongea nao, wanafunzi walilalamikia sana suala la sisimizi kuwaingilia.

Walisema pia kwamba chakula chao kikuu kilikuwa ugali wa mahindi na dagaa, na wengi wao wanapewa kiasi cha kumaliza mwezi mmoja ama wakati mwingine hakitoshelezi. Inapotokea mahitaji haya yamekwisha kabla ya kuletewa basi inabidi mwanafunzi aishi maisha ya kudandia kwa marafiki wenye chakula japo si wakati wote, ni rahisi maana kila mtu ana hali ngumu na anajitahidi kufikisha mwisho wa mwezi.

Upande wa kusoma jioni, hakuna umeme, hivyo wanafunzi wanatumia zaidi kibatari cha mafuta ya taa ili mradi mafuta yawepo.  Sasa kweli wanasoma kwa misingi hiyo mheshimiwa?’
‘Mbona haya mambo ni ya kawaida, mama.  Hata sisi tulisoma kwa shida.  Kinachohitajika ni ari ya kusoma, watafanikiwa tu.’

‘Bila mwalimu?  Hao wanafunzi wako Kidato cha Nne lakini hawajawahi kuwa na mwalimu wa Kiingereza hata siku moja.  Na hata upande wa walimu wengine, taaluma yao ni haba kiasi kwamba wanawazidi wanafunzi kidogo sana.’
‘Wajisomee basi.  Kazi yenu kungoja serikali ikufanyie kila kitu.’

‘Sawa mheshimiwa. Nakuomba siku moja uje uone kama kweli utasoma katika shule kama hizo. Au bora zaidi, mtume watoto wenu kusoma katika shule hizo za ukata.’

Bosi akaanza kukasirika.
‘Yaani unataka kubadilisha hata jina.  Serikali inahangaika weeee kuwaandalia watoto nafasi ya kusoma sekondari katika kila kata waziita shule za ukata?’

Lakini yule mama hakutaka kurudi nyuma.
‘Kama si za ukata, basi leteni watoto wenu.  Mtaambiwa ukweli.  Mimi mwenyewe nilishtuka sana kuwasikiliza hawa wasichana.  Ndiyo maana nimekuja.  Kwa sababu kama hali ndiyo hiyo, nakuambia bora nifungwe kuliko kumpeleka mwanangu katika shule kama hizo.’
‘Wewe umetumwa nini?’

‘Ndiyo nimetumwa. Nimetumwa na wazazi wenzangu ambao wanaumia, wanalia kila siku bila kusikilizwa.  Ngoja nikupe sehemu ya mwisho ya mazungumzo yangu na wasichana wale. Nilipowauliza wanafanyaje kuhusu gharama zao zingine walinijibu hivyo’

‘Mama, ukweli ni kwamba hakuna uwezo wa kupata mahitaji yetu.  Ukitaka mafuta ya kupaka mwili, unatenga ya kula na kupaka, hakuna mafuta maalumu kwa ajili ya mwili. Nguo za ndani ndo hizo hizo za labda kama una bwana mwenye vihela kidogo ...’
Hapo nilishtuka sana mheshimiwa.  Yaani tunawapeleka watoto wetu kwenye uwanja wa UKIMWI moja kwa moja.  Lakini nilijikaza na kuzidi kuwauliza kuhusu masuala ya Bwana.  Majibu yao yakanikatisha tamaa.

‘Mama kwa nini tukufiche maana inatuumiza na sisi.  Inabidi uwe na wanaume angalau watatu, kila mmoja akikupa shilingi elfu moja kwa wiki uongo, unaweza kununua angalau sabuni au kumaliza kodi  ya pango.’ 
Nikawauliza kama hawa wanaume ndio walimu tu maana niliona walimu ni wanne tu.   Walicheka tu.

‘Mwalimu ndiye bora ndiyo maana mnaweza kujikuta mko zaidi ya wanne na mnajuana na hakuna kitu mtafanyana  bali kuvumilia kila mtu ale kwa wakati wake. Maana anayetembea na mwalimu huyo ni tajiri maana mwalimu anatoa dau kubwa kama elfu tano kwa mwezi na hapa kati akikupa shilingi mia tano si haba. Wanafunzi wanaotembea na walimu wanajiona sana na huwezi kuwafanya chochote. Na ukithubutu kusema shule utaihama mwenyewe maana utakuwa unakula bakora kila kukicha, na usiombe mwalimu akuite ofisini maana utatandikwa kama ng’ombe. Na hapo ukute alishakutongoza ukamkataa, utajuta kuzaliwa. Sasa mama utafanya nini?  Na ukimkosa mwalimu, basi utatafuta hawa wa bei ndogo mitaani.’
Mimi mpenzi wakati nasikiliza maelezo yote hayo, nilikuwa namkumbuka binamu yangu. Yuko salama kweli?  Au yeye naye analazimika kuishi maisha kama hayo.  Mwishoni nilishindwa kujizuia, nikaangua kilio.  ‘Maskini binamu yangu ...’
Bosi akashtuka. 
‘We Hidaya unasema nini?’

Ikabidi nivunge kidogo maana mimi sitakiwi kukaa na kusikiliza mazungumzo na wageni.’
‘Samahani baba, nilipata habari asubuhi kwamba binamu yangu anaumwa sana.  Nikamkumbuka tu.’
‘Basi toka hapa.  Unatusumbua.’

Kwa hiyo mpenzi ilibidi nitoke lakini wakati natoka nikamsikia yule mama akisema kwaamba baada ya kusikia yote hayo, yeye na wenzake wamewatoa watoto wao shule moja kwa moja na kama anataka awaletee polisi kuwakamata maana hawawezi kuwaacha watoto katika mazingira hatarishi kama hayo.’

Na kweli.  Katika hali kama hiyo kuna faida gani kuwa na shule?  Kama serikali haina uwezo wa kuhakikisha kwamba shule zake zinajenga badala ya kubomoa kwa nini watudanganye kwamba watoto wanapata elimu huku wakipata mimba au UKIMWI badala yake?  Nakuomba sana mpenzi wangu uende ukamwone binamu maana sasa roho haitulii.

Akupendaye hata uwe mbali namna gani
 
source raia Mwema: Hidaya

No comments:

Post a Comment