WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, March 8, 2013

Kaburu, Hanspope wajiuzulu Simba

 
Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Goefrey Nyange 'Kaburu'
Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Goefrey Nyange 'Kaburu' pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hanspope wametangaza kujiuzulu nafasi zao ndani ya klabu hiyo kuanzia jana, imefahamika.
 
Akizungumza na NIPASHE jana, Kaburu aliliambia gazeti hili kwamba amefikia maamuzi hayo kutokana na wakati mgumu anaokumbana nao kwenye klabu hiyo licha ya jitihada mbalimbali anazozifanya za kuhakikisha Simba inasonga mbele.
 
Kaburu alisema anaamini kuwa baada ya kukaa pembeni, wanachama wengine wenye uwezo wa kuongoza huenda wakapata mafanikio na kuifikisha mbali klabu yao.
 
"Timu yetu ni ngumu sana kuiongoza, tunatukanwa... nimechoka," alisema Kaburu.
 
Awali, kabla ya Kaburu kufikia uamuzi mgumu wa kubwaga manyaga, Kaburu alikiri kuona barua ya kujiuzulu kwa Hanspope na kueleza kwamba ameiwasilisha kwa mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage kwa njia ya barua pepe kwani hivi sasa (Rage) yuko nje ya nchi kwa matibabu.
 
Katika maelezo yake, Hanspoppe alisema ameamua kujiuzulu kufuatia matokeo mabaya ya timu yao katika mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara na pia kuondolewa kwao katika michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika baada ya kupata kipigo cha jumla ya mabao 5-0 kutoka kwa Recreativo de Libolo ya Angola.
 
"Ni kweli nimejiuzulu nafasi zote nilizokuwa nashikilia ili tuwape wengine nafasi," alisema Hanspope ambaye wiki iliyopita ndiye aliyeongoza msafara wa Simba kwenda kuwavaa Libolo nchini Angola.
 
Hanspope alisema kuwa tayari ameshawasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa uongozi na anawatakia mafanikio Wanasimba wengine watakaochukua nafasi zake.
 
Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, jana jioni alikiri kupokea barua za kujiuzulu kwa Kaburu na Hanspope.
 
Baadhi ya wanachama wa klabu hiyo inayoshikilia ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara wamekuwa wakishinikiza viongozi wao kuachia ngazi kutokana na mfululizo wa sare na vipigo katika ligi kuu na pia kuondolewa kwao mapema katika michuano ya Afrika.
 
Hata hivyo, Rage aliwahi kupuuza rai ya kutakiwa kujiuzulu kutoka kwa baadhi ya wanachama kwa maelezo kwamba yeye siyo mchezaji wala kocha na hivyo, wanaotakiwa kuhojiwa kufuatia matokeo yao mabaya ni watu wao wa benchi la ufundi. 
 
Aidha, uongozi wa Simba ulitangaza wiki iliyopita kupitia kwa msemaji wao, Ezekile Kamwaga kuwa wataitisha mkutano mkuu wa dharura ili kujadili mwenendo wa timu yao. Hata hivyo, Kamwaga hakusema ni lini mkutano huo utafanyika. 
 
Rage, Kaburu na viongozi wengine wa kuchaguliwa wa Simba waliingia madarakani kwa ksihindo mwaka 2010 na kwa mujibu wa katiba ya klabu yao, watamaliza muda wao wa kuongoza mwakani wakati utakapofanyika uchaguzi mkuu mwingine.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment