WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, March 27, 2013

Hapa kwetu, tunakimbilia wapi?

  • Kila jambo ni kwa masafa mafupi, hata jengo la Bunge
MSOMAJI utakumbuka kwamba nimekuwa nikisisitiza juu ya umuhimu wa kuwa na mipango inayoangalia masafa marefu, kwa sababu hapa ndipo kwetu, tumefika na wala hatuna kwingine tunakoelekea.
Kwa bahati mbaya sana tunendelea kufanya mambo yetu kana kwamba tunapita njia. Nimekuwa nikitoa mifano kadhaa, lakini kila uchao naona mifano mingine ya kufanya mambo yetu kwa haraka haraka kama vile kuna mahali tunakokimbilia.

Majuzi nilikuwa na majadiliano makali yaliyoishia kuwa ubishi badala ya kuwa ni mabadilishano ya mawazo na mashindano ya fikra. Tulikuwa tunajadili hoja yangu kwamba jamii iliyodhamiria kujiletea mabadiliko inajionyesha kwa kila kitu inachofanya, kuanzia ujenzi wa makazi, miundo ya uzalishaji, mifumo ya elimu, misingi ya ulinzi na usalama, na kadhalika.

Nilikuwa natoa rai (na rai hiyo nairejea leo) kwamba tunajenga majumba ambayo hayaonyeshi uimara na umakini unaoashiria kwamba tupo hapa kuishi na kudumu daima -umu. Hatuhami mwaka ujao wala miaka 500 ijayo.

Hili, kimsingi, ni tatizo la Afrika nzima, na linadhihirisha jinsi ambavyo hatuna uwezo wa kuangalia maisha ya taifa letu kwa masafa ya miaka elfu au zaidi ijayo.

Tuangalie majumba tunayojenga, hata majengo ya idara zinazostahili hadhi ya juu, ni majumba yasiyo kuwa na haiba yoyote. Mfano wa moja kwa moja ni jengo la Bunge lililojengwa mjini Dodoma katika miaka ya hivi karibuni, na ambalo halinipi kabisa taswira ya jengo la baraza kuu la utunzi wa sheria na usimamizi juu ya serikali.

Jengo la Bunge lililoko Dodoma lingeweza kabisa kutumika kama jengo la maonyesho ya teknolojia ya kompyuta au maonyesho ya vifaa vya maabara, au hata ukumbi wa disko, lakini siyo jengo la Bunge kwa sababu halionyeshi haiba ya kasri ambalo ndani yake mambo mazito yanajadiliwa na kuamuliwa.

Aidha nashuku kwamba muda hautakuwa mrefu kabla jengo la Dodoma halijahitaji ukarabati mkubwa kutokana na matumizi ya vifaa duni katika ujenzi wake.

Hatuhitaji kwenda mbali kuona kinyume cha jengo la Dodoma, tunapoangalia jengo la Karimjee ambalo ndilo lilikuwa na ukumbi ambamo Bunge lilikuwa likiketi. Tofauti kabisa.

Tumetembea sana bara Ulaya, Marekani, Asia na kwingineko, ambako tumejionea wenyewe jinsi majengo, hata ya shughuli zisizokuwa za dola, yaliyojengwa karne ya 11 bado yamesimama leo hii na yanawafanya kila wanaoyaangalia kutekwa na mastaajabu.

Tumeona jumba la Ikulu ya Marekani, jengo la Congress, jengo la Mahakama Kuu ya Marekani, Westminster, Whitehall (Uingereza), makao makuu ya Serikali ya India na Mahakama Kuu ya nchi hiyo, na kadhalika.

Kwetu Waafrika, majengo yenye hadhi kama hayo niliyoyataja ni yale yaliyoachwa na mkoloni, kwa sababu mkoloni, angalau katika baadhi ya makoloni yake, alikuwa na fikra za kubakia milele, na kwa sababu hiyo alijenga vitu vya kudumu.

Inashangaza, basi, kwamba sisi ambao ndio tungetakiwa tuwe na mwelekeo wa kudumu kwa kuwa hapa ni kwetu, sisi ndio tunaojenga viota vya kujishikiza, kana kwamba tunajibanza kwa muda tukisubiri muda wa kuendelea na safari yetu. Ajabu iliyoje.

Katika miaka ya mwanzo ya sabini baadhi ya majengo adhimu ya Jiji la Dar es Salaam, kama vile Kaiserhoffya zamani na Splendid Hotel, yalivunjwa na badala yake tukasimamisha maboksi yasiyo na sura wala roho. Mwanza pia wakabomoa Mwanza Hotel na kuweka boksi lao mahali pake.

Katika hili sina budi kumshukuru yeyote aliyechukua uamuzi wa kuinusuru iliyokuwa Dar es Salaam Club ya enzi za ukoloni, kasha ikawa Fordhani Hotel na sasa ndiyo makao makuu ya Jaji Mkuu wa Tanzania. Jengo lile linafanana kidogo na shughuli inayofanyika humo, lakini mengine mengi ni vichekesho. Kuna wakati katika miaka ya sabini ilizungumzwa kwamba jingo lile livunjwe tuweke boksi jingine.

Mtaalamu mmoja aliandika kitabu kwa jina “The Edifice Complex” ambamo anaeleza uzito wamuonekano wa jengo katika saikolojia ya watu mbalimbali. Kasri kubwa zilizosimikwa kama mahala pa ibada zilijengwa kwa njia ambayo ilimfanya kila aliyeingia humo, au hata alitazame kutoka nje, kufanya heshima, na hata woga.

St Paul’s jijini London, au Kadedraliya Cologne, au Msikiti wa Samawi (Blue Mosque) na Sulaymaniaya Istanbul, ni mahali ambapo kila muumini anayeingia anahisi kwamba yuko mbele ya nguvu kuu, na viwango vya upuuzi na mawazo ya hovyo vinapungua sana.

Hii ni kweli kwa hayo majengo niliyoyataja huko nje, lakini hata hapa kwetu nyumbani tunaona nyumba za ibada zinazozalisha hisia za adabu na heshima.
Majengo ya Warumi wa kale, pamoja na barabara zao, majengo ya Wayunani, pamoja na mahekalu yao, piramidi za Misri kabla ya hapo, vyote vilijengwa na jamii zilizojiona kama za kudumu, jamii zisizoondosheka

Msomaji anaweza akashangaa ni kwa nini nimechukua nafasi kubwa kujadili suala la majengo, lakini napenda kumhakikishia kwamba majengo na usanifu wake, huonyesha umahiri wa jamii husika na umakini katika kufanya mambo yake. Pia ni chanzo cha fahari mbele ya jamii nyingine au mataifa mengine.

Jamii inayoshindwa kusimamisha majengo ya nguvu yaliyosanifiwa na wajuzi wa hisabati zilizopangiliwa wakishirikiana na wana sanaa wanaojua kuuunganisha kilichoimara na kinachopendeza, jamii ya namna hiyo itakuwa ya kubabaisha kila siku, itakuwa inatafuta vitu rahisi, vyepesi na visivyodumu. Vitu vya mpito.

Hata ikiambiwa elimu yake imekufa kabisa, jamii ya aina hiyo itaunda kamati ya haraka haraka ili kutuliza ghadhabu za wanajamii wachache wanaouliza maswali, kutafuta majibu mepesi kwa maswali magumu, magumu mno.

source: Raia Mwema  Jenerali Ulimwengu

No comments:

Post a Comment