WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, March 3, 2013

Ni Ushauri Wangu Tu; Kwenye Masuala Ya Kitaifa Tuwe Na Salaam Za Kitaifa, Si Za Kivyama au kidini...

bur1 bea07

Ndugu zangu,

Moja ya changamoto kubwa katika ujenzi wa Umoja wetu wa Kitaifa ni kuchanganya salamu za kivyama na kidini kwenye masuala ya kitaifa.

Hakuna dhambi ya kutumia salamu za kivyama, lakini, hizo ziwe kwenye shughuli za vyama husika, si za kitaifa.

Hakuna pia dhambi ya kutumia salamu za kidini, lakini, iwe ni kwenye mikusanyiko ya kidini na si ya kitaifa.


Ni makosa na ni kuchangia kuligawa taifa pale Mtanzania anaposimama kwenye kusanyiko lisilo la kidini na kuanza na salamu kama ; " Bwana Yesu Asifiwe! Au Asalaam Aleikum!"

Hizo ni salamu za kidini na zinapaswa zitolewe kwenye kusanyiko la wenye dini husika. Fikiri kama kwenye kusanyiko la Watanzania kuna WaTanzania wenye kufuata imani za jadi, au imani za Kihindu, nao watajisikiaje kutengwa kwenye salamu hiyo.

Tungeweza kabisa kuwa na salamu ya kitaifa, napendekeza ifuatayo; "Udumu Umoja Na Mshikamano Wa Watanzania... Jibu ni Udumu!"

Na ingetosha kabisa, kuwa mwisho wa mazungumzo yetu kutamka tu; " Mungu Ibariki Tanzania". Maana, Mungu huyu ni wa wote.

Hakika, kwa hali ilivyo sasa tunachangia wenyewe kwenye hili la udini. Kwa mambo tunayoyaona ni madogo.

Ningeshauri pia kwa viongozi kuacha kutumia mavazi au alama za kidini kwenye masuala ya kitaifa. Huwa nashangaa kuwaona Wabunge wamevalia kanzu bungeni wakati wakifanya kazi za kitaifa. Ingependeza, na ni katika kudumisha umoja wa kitaifa bila kujali dini, kwa wenye imani husika wangevaa mavazi hayo baada ya kutoka jengo la Bunge. Si kuna vyumba vya kubadilishia mavazi?

Ningeshauri pia, kwa wanasiasa na watendaji , ambao kimsingi ni watumishi wa umma wenye watu wa imani tofauti, waache kutumia milio yenye sauti za kidini kwenye simu zao.

Ni ushauri wangu tu...!

Maggid Mjengwa,
Iringa.

No comments:

Post a Comment