WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, March 27, 2013

Mafuriko: Tutaacha lini kumsingizia Mungu

 
 
Na Fredy Azzah, Mwananchi  
Dar es Salaam. Kila wakati mtu anapopoteza maisha au kupatwa na jambo lolote baya, iwe kwa ugonjwa, ajali ama kuuawa kwa makusudi na watu, kauli ya kuwa kazi ya Mungu haina makosa utaisikia kutoka kwa ndugu na waombolezaji mbalimbali.

Kwa maana hiyo basi, nikisema Watanzania tuna kilema cha kumsingizia Mungu  kwa kila jambo linalotupata nitakuwa sijakosea.

Usiku wa kuamkia Disemba 21 mwaka 2011, ilinyesha mvua kubwa jijini Dar es Salaam ambayo ilisababisha mafuriko yaliyopoteza maisha ya zaidi ya watu 40  na wengine zaidi ya 5,000 kukosa makazi.

Wengi walioathiriwa na mafuriko haya ni wakazi wa mabondeni hususani eneo la Jangwani, mto Msimbazi na Kigogo.

Ikiwa ni miaka miwili, miezi mitatu na siku tatu tangu kutokea kwa mafuriko hayo Dar es Salaam, juzi ilikumbwa tena na mafuriko mengine yaliyotokana na mvua zilizonyesha katika maeneo mbalimbali ya Jiji.
Wakati wa mvua za mwaka 2011 Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), walitabiri kutokea kwa mvua hizo na kuwataka watu wa mabondeni wachukue hatua ikiwa ni pamoja na kuhama.

Viongozi mbalimbali wa mkoa pia waliwataka watu wanaoishi kwenye maeneo hatari kuhama, lakini kwao maelezo yote yalikuwa ni kama kelele za chura ambazo Waswahili wanasema hazimnyimi usingizi mwenye nyumba.

Madhara hayo yametokea  siku moja  baada ya dunia kuadhimisha  siku ya hali ya hewa (23 Machi), iliyokuwa na kauli mbiu ya “Ufuatiliaji wa hali ya hewa ili kulinda maisha na mali”
Vivyo hivyo mvua za juzi zimetokea wakati ambapo TMA walishatabiri kuwapo kwa mvua kubwa.

Utamaduni wetu ni kukaa kimya bila kusikiliza ni nini utabiri wa hali ya hewa unasema, baada ya ndugu zetu kupoteza maisha kutokana na mafuriko tunabaki kusema kazi ya Mungu haina makosa, siyo kweli tunamsingizia Mungu.

Siku chache baada ya mafuriko ya mwaka 2011, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, iliazimia kubomoa nyumba zote zilizojengwa mabondeni, katika kipindi cha mwezi mmoja, ukiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Kikwete.
Siku tatu kabla ya kauli hiyo ya Halmashauri,  Rais Jakaya Kikwete, alitembelea Shule ya Msingi Mchikichini kwa lengo la kuwapa pole watu walioathiriwa na mafuriko hayo na kuwataka wanaoishi mabondeni kuhama mara moja, ili kuepuka kupoteza maisha na mali zao.

 Kufuatia agizo hilo, halmashauri ya Ilala, iliitisha kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani, kutathmini athari zilizotokana na mafuriko na kutoa maazimio ya namna ya kubaliana na athari hizo katika siku zijazo.

Waliazimia kubomoa nyumba zote zilizojengwa mabondeni na kwamba utekelezaji wa mpango huo ulitakiwa kuanza ndani ya mwezi mmoja.
Wakati Halmashauri ikijipanga hivyo, baadhi ya wakazi wa Msimbazi na Jangwani, walisema licha ya agizo hilo hawawezi kuhama katika makazi yao kwa sababu hawana maeneo mengine ambayo wanaweza kwenda.
Athumani Mohamed Mkazi wa Msimbazi, alisema hata kama Serikali inawataka wahame katika maeneo hayo hawawezi kuhama mpaka watakapotafutiwa maeneo ya kwenda.

“Mimi nimepanga hapa Msimbazi kwa zaidi ya miaka 10, sasa leo ninapoambiwa nihame huku nikiwa sijui wapi nitakwenda, sitaweza kufanya hivyo zaidi ya kufanya usafi nyumbani kwangu na kuendelea kuishi na familia yangu,” alisema Mohamed.

Hata baada ya serikali kuwataka watu hawa kwenda kuishi katika eneo la Magwepande lilipo Manispaa ya Kinondoni, wengi hawakwenda na matokeo yake juzi yamewakumba tena.







Kwa nini serikali haikubomoa nyumba za mabondeni?
Baada ya serikali kutaka kuwahamisha kwa nguvu, wakazi hawa walikimbilia mahakamani hivyo mipango yote ikasimama.

Mwaka jana mwishoni baada ya TMA kutangaza kuwapo kwa mvua za El-nino kwa mikoa ya Pwani ya Bahari ya Hindi ikiwa ni pamoja na Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa Said Meck Sadiki, alinukuliwa na vyombo vya habari akionya wale wote waishio mabondeni.
 
“Asiyesikia la mkuu huvunjika guu. Efforts (jitihada) zote zimeshatumika. Hatuwezi kuwachapa viboko watu kama hao. Karibu viongozi wote wameshalizungumzia ikiwa ni pamoja na mimi mwenyewe, wabunge na rais, lakini hawasikii, yatakayowapata watajua wao wenyewe.”

“Hatuwezi kuvunja sheria za nchi, tumefungwa mikono na mahakama, kusingekuwa na kesi mahakamani tungeweza kuwaondoa kwa nguvu...mahakama ikituruhusu tutawaondoa kwa nguvu,” alifafanua Sadiki.
 
“Unajua hao wanaodaiwa kukaidi ni kwa sababu wanajua kesi yao iko mahakamani, hivyo natumia nafasi hii kuzungumza mambo mawili; kuwataka wakazi hao kuondoka mara moja, pili tunaiomba mahakama itoe tamko  ili tuwaondoe  kwa nguvu za dola,” alisisitiza.

TMA na Mwakyembe
Katika taarifa yake kwa umma, Mkurugenzi wa TMA Dk Agnes Kijazi anasema kuwa, anawataka wananchi kuhakikisha wanatumia vyema taarifa za mamlaka hiyo.
“Nawataka wananchi kujenga tabia ya kutumia taarifa za hali hewa katika kupanga shughuli zao za maendeleo,” anasema Dk Kijazi.

Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi Dk Harisson Mwakyembe ambaye TMA ipo chini ya wizara yake, anasema kuwa Serikali itaendelea kuijengea uwezo mamlaka hiyo ili itoe taarifa za uhakika.

Katika taarifa yake aliyoitoa kwenye siku ya hali ya hewa duniani, anasema kuwa TMA itaendelea kutoa taarifa kwa umma ili waweze kutumia taarifa zake.
Swali la msingi hapa, ni je wananchi kama hawa wa mabondeni huwa hawapati hizi taarifa? Ama hupata na kusema ‘wao (TMA) ni nani mpaka wajue kuwa mvua zitanyesha, wao wamekuwa Mungu’.

Yakitokea majanga ya mafuriko wakati wa kujiokoa kila mtu utasikia akitaja jina la Mungu kwa lugha yake, ukweli ni kuwa watu wakiwa wasikivu hali hii inaepukika, tuache kumsingizia Mungu kila jambo.
 
source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment