WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, March 2, 2013

Rais afunguka kuhusu wachochezi wa kidini





RAIS Jakaya Kikwete  amewaagiza polisi, wakuu wa mikoa na wa wilaya kutofanya ajizi kwenye suala la wachochezi wa kidini, bali wachukue hatua stahiki na kwa haraka ili kuendeleza amani ya nchi.

Kikwete alitoboa hayo kupitia hotuba yake ya mwisho wa mwezi aliyoitoa juzi kwa Taifa  kupitia vyombo vya habari Dar es Salaam.
“ Nimewakumbusha polisi na mamlaka husika kote nchini wasifanye ajizi kwenye matukio ya namna hiyo. 
Wawachukulie hatua stahiki wale wote wanaohusika.  Nimewataka wazingatie msemo wa Kiswahili usemao ajizi nyumba ya njaa”, alisema. 

Alisema kuwa wachochezi wa mifarakano  na chuki za kidini wasipodhibitiwa ipasavyo wataleta maafa kwa Watanzania wasiokuwa na hatia akiwataka wakuu wa wilaya na mikoa kutimiza ipasavyo wajibu wao kama walinzi wa amani.

Alisema wakati wote Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote wanaochochea chuki za kidini, wanaodharau vitabu vitakatifu vya dini nyingine na wanaokejeli dini nyingine

Kuhusu matokeo mabovu ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012, Rais Kikwete alitaka utafiti ufanyike ili kujua chanzo  na kusisitiza kwamba   bila utafiti wa kina kufanyika , tatizo hilo linaweza kuwa kubwa na kuligharimu taifa.

“Wanafunzi 397,132 walifanya mtihani huo na kati yao, waliofaulu ni 126,851 sawa na asilimia 34.5,  wanafunzi  240,903 ambao ni asilimia 65.5 hawakufaulu. Kwa ulinganifu, matokeo hayo ni mabaya kuliko matokeo mengine ya mtihani huo ya miaka ya hivi karibuni. 

Ni suala muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu, hivyo lazima ukweli wake ujulikane kwa uhakika,”alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2012, yameshtua na kufadhaisha watu wengi nchini na kwa sababu stahiki kabisa. 
Kwanza, kwamba kiwango cha kufaulu kimeporomoka sana, tena ghafla, kutoka asilimia 53.6 mwaka 2011 hadi asilimia 34.5 mwaka 2012.  Hili ni anguko la asilimia 19.1 ambalo, kwa kila hali, ni kubwa sana.” 

Rais Kikwete alisema kuwa mambo hayo, ndiyo msingi wa uamuzi wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuamua kuunda Tume ya kuliangalia suala zima la mitihani ya mwaka 2012 na matokeo yake.

“Hii itawezesha Serikali na wadau wengine kuchukua hatua stahiki kurekebisha mambo mapema iwezekanavyo ili hatimaye mambo yawe mazuri siku za usoni. 

Tusipofanya hivyo mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi na lawama zinaweza kuwa kubwa zaidi kwa Serikali,”alisema Kikwete.
Rais katika hotuba yake pia alizungumzia suala la amani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ambapo alifafanua kwamba nchi Wanachama wa  Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) walikubaliana kupeleka vikosi vya kulinda usalama nchini humo wakiungwa mkono na Umoja wa Mataifa utakaolifanya jeshi hilo kuwa sehemu ya vikosi vyake vya kulinda amani DRC (MONUSCO)

“Tumepeleka walinzi wa amani Darfur, Sudan na Lebanon, kwa nini tusipeleke Kingo...: Kama nchi jirani, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yenye amani, usalama na utulivu ni jambo lenye maslahi makubwa kwetu. 

Ina maana ya kutokuwa na wakimbizi kutoka nchi hiyo, uharamia katika Ziwa Tanganyika kutokuwapo na ustawi wa shughuli za kiuchumi na kibiashara kwa upande wetu,” alisema Rais Kikwete.

Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment