WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, February 8, 2013

Vitambulisho vya taifa vyatoka


NA MUHIBU SAID

Rais Jakaya Kikwete na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Professa Ibrahim Lipumba, wakifurahia jambo wakati Rais akimkabidhi Kitambulisho cha Taifa Mwenyekiti huyo kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam jana.

Hatimaye Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) imefanikiwa kuanza kutoa vitambulisho hivyo na Vitambulisho vya taifa vyatoka raia 46 waliokabidhiwa vitambulisho hivyo jana jijini Dar es Salaam. 

Kabla ya Rais Kikwete kupokea kita kitambulisho chake chenye namba 19501007-1110100001-26, ambacho mwisho wa matumizi yake ni Februari 7, 2023, kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, alizindua mfumo wa usajili na utambuzi wa watu kitaifa na utoaji wa vitambulisho vya taifa. 

Waliopewa vitambulisho hivyo jana ni viongozi wakuu wa serikali wastaafu, walioko madarakani, taasisi za umma, kiraia, dini, vyama vya siasa pamoja na wananchi wa kawaida wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Amani Abeid Karume pamoja na mawaziri wakuu wastaafu, Dk. Salim Ahmed Salim na Jaji Joseph Warioba, Rais Kikwete alibeba jukumu la kuwakabidhi vitambulisho raia 44.

Wengine waliohudhuria hafla hiyo, ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad; mawaziri, makatibu wakuu, viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa, vyombo vya ulinzi na usalama, dini, taasisi za kiserikali, kiraia na wananchi wa kawaida kutoka Tanzania Bara na Zanzibar. 

Wa pili kupewa kitambulisho alikuwa ni Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete, alichokabidhiwa na Waziri Nchimbi, katika hafla hiyo. Rais Kikwete alianza kwa kumkabidhi kitambulisho Mwinyi, kisha Mkapa, Karume na Maalim Seif.

Wengine, ambao Rais Kikwete aliwakabidhi vitambulisho vyao kwa nyakati tofauti katika hafla hiyo jana, ni Dk. Salim na Jaji Warioba. Wengine ni mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale-Mwiru, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi; Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki na Mjane wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, marehemu Abeid Aman Karume, Fatuma Karume. 

Wengine ni Mke wa Rais mstaafu Mkapa, Anna Mkapa; Mke wa Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Ester Sumaye; Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo  na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbaraka Abdulwakil. Wengine ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema; Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Othman Rashid na Naibu wake, Jack Zoka na Kamishna Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Tanzania, Magnus Ulungi. 

Wengine ni  Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna Jenerali (CGP) John Minja; Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Pius Nyambacha; Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa, Mkuu wa Madhehebu ya Bohora nchini, Sheikh Seif Jamal na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaad Mussa.

Pia walikuwapo Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba; Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk. Ramadhan Dau na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Mfuko wa Pensheni ya Mashirika ya Umma (PPF), William Erio.

Wengine ni Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat), ambaye pia ni Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Limited, Reginald Mengi; Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda na Evod Mmanga kutoka Tango.

Wengine ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata), Lupi Mwaswanya; pamoja na wawakilishi na wananchi wa kawaida kutoka Wilaya za Ilala, Kinondoni, Temeke, mkoani Dar es Salaam, Kilombero, mkoani Morogoro na visiwani Zanzibar.

 Katika orodha hiyo pia alikuwapo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Janerali Devis Mwamunyange ambao hawakuhudhuria. Taarifa pia zinasema Mama Maria Nyerere alikuwa apewe lakini alitoa udhuru mapema kwa kuwa yuko nje ya Dar es Salaam. Pia waliotoa udhuru ni mawaziri wakuu wastaafu. 

Rais Kikwete alisema uzinduzi huo umetimiza ndoto ya Watanzania kuwa na vitambulisho vya taifa iliyokuwapo muda mrefu, ambalo lilianza kushughulikiwa na marais waliomtangulia kwa namna yake.

 Alisema kuchelewa kwa vitambulisho hivyo, kumechangiwa na ukosefu wa fedha za kugharimia mradi na changamoto zilizoukumba mchakato, ikiwamo baadhi ya watu kuuzuia mahakamani. 

Hata hivyo, alisema tayari serikali Nida imeshajili wafanyakazi wake kwa ajili ya kuingizwa kwenye mfumo huo na kupata kitambulisho na kwamba, watu wengine watasajiliwa baadaye baada ya kuchukuliwa alama za vidole, saini na picha zao.

Rais Kikwete alisema suala hilo si la hiari, kwani liko duniani kote na kwamba, watu wote wakitambuliwa, pamoja na faida nyingine watakazozipata katika shughuli zao, pia itakuwa rahisi kwa mabenki kutoa mikopo na kupata pembejeo za kilimo na kusisitiza kuwa hakuna mtu atakayeachwa.

Alisema serikali itasaidia kukabili changamoto zote zinazoukabili mradi, ikiwamo kuhakikisha fedha za kuukamilisha zinapatikana ili Watanzania wote wawe wamepata kitambulisho ifikapo mwaka 2015 na wakitumie kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo.

Alisema tayari amekwisha kuongea na Waziri wa Fedha na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, ambao wamemuhakikishia kuwa fedha hizo zitapatikana na kusisitiza kuwa mwaka huu hakuna ujanja, bali lazima zipatikane na kwamba, atashangaa kama waziri na katibu mkuu wa wizara hiyo hawatatimiza ahadi waliyotoa. 

Awali, Waziri Nchimbi na Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Dickson Maimu, walisema kwa nyakati tofauti kuwa mradi huo unakabiliwa na changamoto kubwa, ambayo ni upatikanaji wa fedha za kuendeshea mradi, hasa kwa kuzingatia zoezi hilo linatakiwa kutekelezwa sambamba na zoezi la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuhuisha Daftari la Kudumu la Wapigakura ili vitambulisho vitumike katika kura ya maoni ya katiba mwakani, pamoja na kusaidia katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

Rais aliwataka watumishi wa Nida kuwa waadilifu katika utoaji wa vitambulisho na kuepuka kuwapa watu wasiokuwa raia wa Tanzania. “Mkimbizi asipate cha mgeni mkazi na mgeni mkazi asipate cha raia. Epukeni kuwapa wasiokuwa raia. Matatizo yanayokuwapo kwenye pasipoti yasiwapo kwenye vitambulisho vya taifa. 

Pasipoti zetu zinakamatwa kwa sababu mtu kapewa pesa. Tutafuatilia kwa karibu na atakayekiuka tutakula naye sahani moja,” alisema Rais Kikwete na kuongeza: “Ukimpa kitambulisho cha taifa asiyekuwa raia umefanya kosa kubwa sana.”

Pia alisema Dar es Salaam kuna baadhi ya watu walitoa fomu za kuingia kwenye mfumo huo na ili kupata kitambulisho kwa kutoza pesa na kuagiza wenye tabia hiyo wakamatwe mara moja hata akiwa ni mwenyeviti wa serikali ya mtaa.

Aliwataka Watanzania kutokutoa taarifa za uongo na kuonya kuwa atakayebainika hatua za kisheria zitafuata mkondo wake. Aliwataka Watanzania kuwa wazalendo na kuzitaka pia taasisi za serikali zinazoshughulika na nyaraka zinazohusu uraia, kama vile Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (Rita), kuwa makini katika kutoa vyeti vya kuzaliwa ili kuepuka kuwapa watu wasiostahili. 
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment