WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, February 22, 2013

Elimu tofauti zitazaa mataifa tofauti, na hayataiva chungu kimoja


NIMEELEZA kwamba elimu ndicho kiungo kinachowaunganisha wanajamii waliopo leo na pia ni kiungo kinachowaunganisha wanajamii waliopo na wanaokuja kwa maana ya mapokeo na hazina ya utambuzi wa jamii endelevu.
Jamii isiyokuwa na elimu inayotambulika kama elimu ya jamii hiyo ni jamii ya wapita njia, kwa maana wako pamoja kwa muda lakini kila mmoja ana safari  yake mwenyewe, na safari zao hazihusiani sana.
Nikiangalia mataifa makubwa yaliyopata maendeleo ya kiufundi, kiteknolojia na kiviwanda, naona mifumo ya elimu iliyoasisiwa karne kadhaa zilizopita, na ambayo imekuwa ikiboreshwa kila mara kukidhi mahitaji mapya katika mazingira mapya. Lakini, hata inapobadilishwa katika kuiboresha, elimu hiyo haiachi misingi ya awali inayoitambulisha kama elimu ya taifa fulani.
Nchi hizo nazo zinasikikika zikilalama kuhusu viwango duni vya elimu yake. Tofauti na wetu, wakuu wa nchi hizo hawapiti wakijisifu tu kwa uwekezaji waliofanya katika uwanja wa elimu, bali huendelea kutia mkazo katika umuhimu wa kuboresha elimu yao ili iweze kuendana na mabadiliko duniani.
Kwa mfano, viongozi wa Uingereza, Ufaransa na Marekani wamekuwa wakilalama kuhusu kushuka kwa elimu yao dhidi ya nchi kama Singapore na Korea, hususan katika elimu ya sayansi na teknolojia.
Lakini, pamoja na maboresho yote yanayofanywa mara kwa mara, pamoja na kufuata nyendo mpya za sayansi na teknolojia,  misingi ya elimu inayojenga utambulisho wa taifa na uzalendo wa raia haibadiliki. Hakuna shule ya Waingereza inayofundisha hisabati na kemia bila kufundisha Magna Carta, Elizabeth wa Kwanza, William Shakespeare na Oliver Cromwell.
Hakuna shule ya Marekani itakayofundisha teknolojia ya dijitali bila kufundisha Boston Tea Party, George Washington na Benjamin Franklin.
Wafaransa hawatambui elimu itakayowapa watoto wao ujuzi wa kurusha satelaiti iwapo watoto hao hawatafundishwa kuhusu 1789 na kutekwa kwa gereza la Bastille, na maana hasa ya maneno “Liberte, Egalite, Fraternite” pamoja na historia ya Kardinali Richelieu.
Pamoja na maendeleo makubwa ya viwanda na uvumbuzi, hakuna mtoto wa Kijerumani atakayepita shuleni bila kufundishwa kuhusu Martin Luther, Goethe na Beethoven.
Ndivyo yanavyofanya mataifa yanayojali utambulisho wake kama mataifa. Wahindi wanafanya hivyo ; Wajapani wanafanya hivyo ; Warusi wanafanya hivyo ; mataifa yote yanafanya hivyo. Tumebaki Waafrika.
Tumebaki hivyo kimsingi kwa sababu hatujawa mataifa. Tulipokusanywa pamoja na mkoloni ili tumtumikie, na akatupachika jina la Tanganyika, au Mali, au Angola, au Kenya, au Kongo, alituumba jinsi alivyotaka, kama vyombo vyake vya kumfanyia kazi. Hakuwa na nia ya kutufanya tuwe mataifa.
Ni katika kudai Uhuru wetu ndipo tulianza kujitambulisha kama taifa kutokana na kutawaliwa kwa pamoja, si kutokana na uhalisia wetu wa zama kabla ya wakoloni.
Baada ya Uhuru, wapo waliodhamiria kujenga mataifa kutokana na kile kilichoachwa na mkoloni, Julius Nyerere akiwa mmoja wao. Wapo pia waliorudi katika mataifa yao ya asili, yaani makabila, kama Jomo Kenyatta. Leo hii tunaona matunda ya mitazamo hii miwili tofauti : Nyerere alianza kujenga taifa moja baina ya makabila kadhaa kupitia elimu, lakini kwa sababu warithi wake wameitelekeza elimu, taifa hilo limeanza kumomonyoka ; Kenyatta alijenga kabila lake, si taifa, na kabila lake linaendelea kujiimarisha, na Kenya imeshindwa kabisa kuwa taifa.
Hakuna muujiza katika hili. Taifa hujengwa na watu walio pamoja na waliodhamiria kujenga taifa ; halizuki hivi hivi tu. Kuwa na watu wengi mahali pamoja, katika eneo la ardhi yenye mipaka iliyochorwa kwa umahiri mkubwa, haina maana ya taifa. Huo ni mkusanyiko mkubwa wa watu katika eneo fulani, lakini si taifa.
Kinachojenga taifa ni elimu, ni maadili yanayochangiwa na kila mmoja ndani ya jamii ; ni mitazamo inayoshabihiana miongoni mwa wanajamii ; ni tabia na haiba. Yote haya hufundishwa kupitia elimu iliyoasisiwa na kuendelezwa na jamii husika, si na waziri wala rais, bali na wanajamii walioafikiana juu ya aina ya elimu ya kuwapa watoto wao na aina ya elimu ya kuirithisha toka kizazi hadi kizazi.
Tukishindwa kulielewa hili, kama ambavyo naona tumeshindwa, basi tuelewe kwamba hatujengi taifa moja. Iwapo tumekubali kwamba kila anayeweza ana hiari ya kuwafundisha wanawe kadri anavyojua, basi tuelewe kwamba tunajenga mataifa mengi ndani ya nchi moja, na tutambue kwamba iko siku mataifa haya hayataiva ndani ya chungu kimoja. Nitalieleza hili mbele ya safari.
Nimekuwa nikisema kwamba tumekuwa tukienenda kama vile jamii ya mpito, kama vile hapa tulipo tuko ‘transit’ na tunakokwenda ni kwingine. Kila kitu tunachofanya kinaashiria ‘uharaka’ fulani.
Hatutulizani, tukatafakari kwa pamoja. Ni kama vile hatuna pumzi ya kuketi na kufikiri kwa muda mrefu, tukabadilishana mawazo, tukajenga hoja na kuzipambanisha, tukapima uzito wa fikra na kuzichambua, tukahojiana kwa undani, tukapata kujua kila mmoja anafikiri nini na kwa nini.
Tunakimbilia wapi, na hapa ni kwetu ? Nimekuwa nikisema kwamba tunahitaji kutambua kwamba tupo hapa tulipo kwa miaka milioni kadhaa ijayo, na zaidi ya hapo tutaendelea kuwapo, si kwa sababu sisi tunaoishi leo hatutakufa, bali kwa sababu kila anayezaa hafi akapotea. Muendelezo wa uhai wake hujitokeza katika uzao wake.
Kama hivyo ndivyo, basi, hatuna budi kujenga vitu vya kudumu, hasa miundombinu yote, ikiwa ni pamoja na makazi yetu, miji ya kudumu na vijiji vya kupendeza, barabara na njia za reli, bandari, mikondo na mifereji ya maji ya kudumu, na kadhalika.
Katika miundombinu hiyo yote, muhimu zaidi ni miundombinu iliyojengwa katika akili za watu wetu : Elimu.
Source: Raia Mwema: Jenerali Ulimwengu

No comments:

Post a Comment