WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, February 8, 2013

Halali mtoto kufanya mambo ya kitoto, marufuku kwa mtu mzima


HALALI mtoto kufanya mambo ya kitoto, marufuku kwa mtu mzima.
Tofauti kati ya udogo na ukubwa haielezeki kwa umbile wala ‘saizi.’ Wapo watu wadogo wa mwili ambao ni wakubwa na pia wapo watu wenye miili mikubwa ambao bado ni wadogo, kwa umri, tabia na jinsi wanavyotenda mambo yao.
Tunapokuwa wadogo tunakuwa na haki ya kutenda mambo madogo, mambo ya kitoto, na wazazi na wakubwa zetu wanatuvumilia huku wakituelekeza kwa sababu wanajua kwamba bado tu wadogo, bado tunakua na tutaachana na tabia hizo tutakapokuwa tumefikia utu uzima.
Dalili za kusogea mbele na kukua, kutoka hali ya utoto na kuelekea utu uzima, pia huonekana. Mtoto hufikia umri wa kutumwa dukani, kuchunga mbuzi, kwenda shule ya karibu, kwenda shule ya mbali, na hatimaye kuondoka nyumbani kwa wazazi wake kabisa.
Utoto una raha zake, na hizi hazipatikani kwingineko isipokuwa utotoni. Tulifundishwa tukiwa wadogo kwamba “Watoto hucheza ni sentenso” kwa maana kwamba inajitosheleza kwa nomino na kitendo lakini pia kwa sababu ina mantiki kwamba ada ya watoto ni kucheza. Mtoto asiyecheza ni chanzo cha shauku kubwa kwa wazazi wake ( anaweza kuwa anaumwa) na mtu mzima asiyeisha kucheza anawafanya wanaomuangalia wajiulize kama akili yake iko sawa.
Katika utoto, hata matendo yanayojithibitisha kwamba si ya haki yanaelezeka kwa sababu ni ya utotoni na utotoni watoto hutenda kama watoto watendavyo utotoni. Kwa mfano, ipo tabia ya kunyang’anyana wakati wa mlo, mara nyingi ukiwa ni mlo wa pamoja, watoto wakilizunguka sinia la wali au ugali, huku macho yote yakiiangalia minofu michache ya nyama iliyopo.
Kwa sababu nyama inakuwa ni tunu katika mazingira yetu halisi, kila mtoto anaweka ‘akiba’ yake ya nyama ili aile pale wali au ugali utakapokuwa umeisha na aweze kuwaringia wenzake waliomaliza kitoweo chao mapema. Zahma inayompata mtoto ‘mjanja’ kama huyo ni kwamba mlo unapokaribia mwisho hutokea binamu mkubwa miongoni mwa watoto wale, akalikumba sinia, pamoja na wali au ugali uliosalia, na nyama zote zilizowekwa ‘akiba’ kisha akakimbia na kwenda kula peke yake.
Zogo linalotokea pale huishia pale pale, na hakuna mtu mzima atakayeshughulishwa mno na tukio hili, kwa sababu ni mambo ya kitoto, na watoto wakikua wataachana na michezo hiyo.
Watoto hucheza michezo ya “baba na mama,” wakiigiza ndoa na harusi, mara nyingi wakiwa faragha, kwa maana kwamba hakuna mtu mzima anayewaona. Mchezo kama huo hauna madhara kwa sababu watoto wanafikiria ni nini baba na mama huwa wanafanya wanapokuwa faragha. Wakigundulika wanachapwa, lakini wasipogundulika ni raha tupu.
Na michezo hii nayo ina ukomo wake. Ni marufuku kwa kijana aliyebalehe kucheza mchezo huu, kwa sababu umri wake haumruhusu kucheza michezo ya kitoto, na sasa anatakiwa ajiandae kucheza michezo ya kikweli ya “baba na mama.” Kadhalika, michezo ya kutega ndege, kurusha tiara (kishada) na “mchezo wa kalinge kanyama”. Ni michezo wafanyayo watoto wakati wanakua kuelekea utu uzima.
Utoto pia hujumuisha adha mbali mbali ambazo ukubwani hutoweka. Watoto wengi hukumbwa na tatizo la kukojoa kitandani, na huchapwa na wazazi wao kwa sababu ni tabia inayoudhi na inayosababishwa na uvivu wa kuamka inapobidi kwenda haja ndogo. Tatizo hili nalo hutoweka mtoto anapokuwa kijana, na ni zahma kubwa iwapo mtoto ataendelea kulowesha matandiko baada ya kuwa amebalehe.
Hata kuangukaanguka ni sehemu ya utoto. Mtoto anahitaji muda wa kuyajua mazingira yake, tokea ndani ya nyumba ya wazazi wake hadi viwanja anakokwenda kucheza. Uwezo wa kutambua mazingira hatarishi, kama vile utelezi, bado ni mdogo. Inabidi aanguke mara nyingi kabla hajatambua ni wapi kuna utelezi, ili afanye hadhari kila anapokanyaga sehemu hiyo.
Baada ya muda tatizo hili pia huisha, na mtu mzima anayeonekana akidondoka hovyo anajulikana kama aliyelewa au mgonjwa. Binafsi nakumbuka kwamba kwenye umri fulani nilisema kimoyomoyo, " Lo, siku hizi sianguki tena !" Ilikuwa ni ishara ya kukua.
Si watoto wote hunyonya kidole, lakini wale wanaofanya hivyo huwapa shauku kubwa wazazi wao, ambao hufanya jitihada za kila aina kuwafanya waache tabia hiyo. Ni tabia ya utoto ambayo ikionekana kwa mtu mzima itakuwa ni kioja, ni balaa.
Matamanio ya watoto nayo pia huendana na hali ya utoto. Utamu wa peremende, soda, keki, andazi, kitumbua na ‘shikilimu’ ni utamu wa utotoni. Nilipokuwa mtoto niliweka nadhiri kwamba nikikua na nikapata fedha ningenunua peremende, mandazi, keki na vitumbua, nile hadi nivimbiwe. Hamu hii ilinitoka kabla hata sijapata mshahara wangu wa kwanza. Utu uzima ulileta matamanio mapya, tofauti kabisa.
Kupenda kubembea pia ni tamanio la utotoni. Tunapokuwa wadogo mama zetu hutubelembeza kwa kuturusharusha. Siku hizi bembea zinatengenezwa China na zinapata soko kubwa kwetu, kwa sababu mtoto anaona raha kubwa anapobembea. Akiisha kuwa mkubwa atakutukana ukimwambia apande kwenye bembea, jambo la kitoto. Mtu mzima anayependa kubembea anasumbuliwa na taahira ya akili.
Yapo mambo mengi ambayo yanajulikana kwamba yanahusiana na utoto, na watoto wengi huyapitia bila kupata lawama kubwa, kwa sababu yanatambulika kama sehemu ya awamu mahsusi ya makuzi. Kadri mtoto anavyobadilika na kuwa kijana, na kisha kijana akawa mtu mzima ndivyo tabia hizi zinavyotakiwa kupungua, kufifia na mwisho kutoweka kabisa, ili mtu mzima atende mambo ya utu uzima. Hili lisipotokea, jamii itajua kwamba mtu huyo, pamoja na utu uzima wake, amevia. Vivyo hivyo kwa taifa pia.
SOURCE: RAIA MWEMA: Jenerali Ulimwengu

No comments:

Post a Comment