WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, February 18, 2013

MAUAJI YA VIONGOZI WA DINI – TUNA DHAMIRA YA KUYAKOMESHA?



UTANGULIZI

Katika kipindi cha wiki moja tumeshuhudia mauaji ya viongozi wawili wa dini ya kikristo. Mchungaji Matayo wa kanisa la Pentecostal Assemblies of God of Tanzania (PAGT) aliuawa Buseresere, mkoani Geita na baadhi ya waumini wa dini ya kiislam wakati akiwasindikiza jamaa walioenda kumtembelea ndugu yake. Leo tena huko Zanzibar Padre Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki, parokia ya Minara miwili ameuawa.

Sababu ya mauaji ya mchungaji Matayo inaelezwa kuwa ni kutokana na mgogoro ulioanza kipindi cha huko nyuma juu ya nani mwenye haki ya kuchinja.

Inaelezwa kwamba miezi michache iliyopita, kuna wakristo walichinja ng’ombe huko Sengerema kwaajili ya sherehe yao, na baadaye waislam walilalamika kuwa walikuwa wamelishwa nyama ambayo haikuchinjwa kadiri ya imani yao. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo alitoa agizo kuwa ni waislam pekee ndio wenye haki ya kuchinja, uamuzi ambao haukuwaridhisha baadhi ya wakristo.

Tarehe 24/01/2013, Waziri katika ofisi ya Raisi, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wasira alifika Mwanza na kufanya mkutano na viongozi wa dini, na kisha alitoa tamko kuwa ni waislam pekee ndiyo wenye haki ya kuchinja. Kauli hiyo ilichochea zaidi tatizo badala ya kupunguza.

Tarehe 29/01/2013, Umoja wa Makanisa ya Kikristo jijini Mwanza, ukijumuisha TEC (Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania), CCT (Jumuiya Kikristo Tanzania) na CPCT (makanisa ya kipentekoste Tanzania) ulitoa tamko kupinga kauli ya Wazira Wasira na kueleza kuwa ilikuwa inakiuka katiba ya Jamhuri ya Mwungano wa Tanzania ibara ya 19 kifungu cha 1 na 2, na hivyo waliwaagiza waumini wao kutokula nyama iliyochinjwa kinyume na desturi za kikristo, badala yake wanastahili kuchinja wenyewe.

Matokeo ya kauli hiyo ilikuwa ni kupungua sanakwa mauzo ya nyama jijini Mwanza hata kulazimisha nyama ya ng’ombe kushuka bei kutoka shilingi 5,000 mpaka shilingi 3,000 kwa baadhi ya bucha. Ni tamko hili hilo liliwafanya baadhi ya wakristo kutokununua nyama katika bucha nyingine huko Buseresere na badala yake wakaenda kununua nyama katika bucha mojawapo iliyokuwa imeandikwa YESU NI BWANA. Ni katika bucha hiyo ndipo mapigano yalipoanzia baada ya baadhi ya waumini wa dini ya kiislam walipoamua kuwavamia wanunuzi na wauzaji katika bucha hiyo. Mapigano hayo yalienea hadi mtaani mpaka kufikia mauaji ya mchungaji Matayo ambaye hata alikuwa hajui kilichokuwa kikiendelea. Mapigano hayo yamesababisha kifo, majeruhi na upotevu wa maili. Baya kuliko yote, mapigano hayo yameacha chuki kubwa kati ya wakristo na waislam mjini Buseresesre.

Tarehe 17/02/2013 majira ya saa 1 alfajiri, padre Evarist Mushi wa kanisa Katoliki, parokia ya Minara Miwili, Zanzibar ameuawa kwa risasi wakati akishuka kwenye gari yake ili aingie kanisani kuendesha misa ambayo ilitarajiwa kuanza saa 3.30 asubuhi. Inaelezwa kuwa wauaji walikuwa kwenye gari ndogo, na mara baada ya kumwua walitoroka.

Tarehe 25/12/2012, padre Ambrose Mkenda wa kanisa katoliki parokia ya Tomondo, Zanzibar alinusurika kufa  baada ya kupigwa risasi kichwani. Wauaji hao, kisha walikimbia.

Kabla ya shambulio hilo la padre Ambrose, kulikuwa na matukio ya kuwashambulia mapadre huko Zanzibar ambapo mojawapo lilikuwa ni lile la tarehe 18/10/2012 ambalo baadhi ya waumini wa dini ya kiislam walivamia kanisa wakipiga kele kuwa wanataka kichwa cha Askofu Shayo, waliposhindwa kuvunja kanisa walienda kanisa jingine ambalo linaongozwa na padre Emanuel Masoud, nako walidai kuwa wanataka kichwa cha Masoud.

Mwakajana pekee yake, zaidi ya makanisa 30 yalichomwa moto na baadhi ya waumini wa dini ya kiislam. Zaidi ya makanisa 25 yalichomwa moto Zanzibar, 3 yalichomwa moto Dar es salaam, na 3 yalichomwa moto Mwanza.

Nimeyaandika matukio haya kuonesha kuwa haya yanayotokea leo hayajaanza leo, viashiria vyake vimeanza siku nyingi lakini kwa bahati mbaya au hatuna uwezo wa kuyazuia, au hatuna dhamira au hatuna mtu wa kuyazuia.

Ni muhimu sana kujua chanzo cha haya yote ili kuweza kutatua tatizo. Usipojua chanzo, huwezi kumaliza tatizo.

NINI CHANZO CHA MAUAJI HAYA YA KIDINI

Kuna wale watakosema kuwa mauaji ya mchungaji kule Buseresere chanzo chake ni uchinjaji wa wanyama, kule Zanzibar ni Wazanzibari kutaka kujitenga na Tanzania bara, kule Dar es Salaam ni mtoto kukojolea msahafu, na kule Mwanza ni wakristo walokole kuchoma moto maandiko ya dini ya kiislam yaliyokuwa yamebandikwa mlangoni mwa nyumba ya mgonjwa muislam aliyekuwa ameomba aombewe na walokole. Lakini ukweli ni kuwa hata hizo tunaziaminishwa kuwa ni sababu siyo chanzo bali ni sehemu ya matiokeo ya chanzo halisi.

Kuna watu sasa hivi katika jamii yetu, wanahangaika kutafuta mahali pa kuanzia ili wapate sababu ya kuanzisha mapigano ya kidini. Hivyo kwao likipatikana japo jambo hata kama litakuwa ni dogo kiasi gani, wanafanya kila sababu ya kulikuza ili iwe sababu ya kuanza kupigana na kuuana.

Hapa chini naorodhesha chanzo halisi cha vurugu zinazofanywa nyuma ya mwavuli wa udini:

1.    MAFUNDISHO YA CHUKI
Kuna wahubiri ambao kila siku waingiapo kwenye nyumba za ibada kazi yao kubwa imekuwa ni kutoa mafundisho ya chuki kati ya waislam na wakristo, na wengi wa wahubiri hawa ni wahubiri wa dini ya kiislam. Wamekuwa wakihubiri wazi na hata wametoa kanda na CD ambazo zinaeleza kuwa waislam katika nchi hii wanaonewa katika mambo mengi. Wanaonewa katika Elimu, katika ajira na katika mgawanyo wa uongozi. Wamekuwa wakati wote wakiwafundisha na kuwaaminisha waumini wao kuwa matatizo yote waliyo nayo waislam yanatokana na wakristo, na kuwa nchi hii inaongozwa na ‘mfumo kristo’. Wamekuwa wakiwaeleza waumini wao kuwa taasisi mbalimbali za kijamii zilizopo chini ya makanisa kama vile hospitali, shule na vyuo zimekuwa zikistawi kutokana na kupewa ruzuku na serikali chini ya MOU kati ya serikali na makanisa.

Wapo viongozi ambao wamekuwa wakiwahubiria waumini wao kuwa wanatakiwa wawaue mapadre na wachungaji iwe ni kwa kificho au kwa wazi, na kuwa kwao ukiua au ukiuawa hakuna hasara maana vyote vinakupeleka ahera. Mafundisho haya ya chuki yapo mioyoni na vichwani mwa baadhi ya Watanzania. Na hawa ndiyo kila siku wanakaa na kuangalia ni nini kinaweza kuwa sababu ya kuanzisha mapigano.

2.    ULEGELEGE WA SERIKALI
Duniani kote, watu wenye dhamira mbaya dhidi ya binadamu wengine wapo. Hata ungetoa Elimu kwa kiasi gani, ni lazima kutakuwepo na watu ambao hawatasikiliza, nao watatenda kadiri ya nia zao ovu zilizopo vichwani na mioyoni mwao. Watu wa namna hiyo, siku zote hudhibitiwa na dola kwa kutumia sheria. Na uimara na umadhubuti wa serikali yeyote Duniani huangaliwa juu ya uwezo wake wa kusimamia sheria ili kuleta utengamano miongoni mwa watu wenye dhamira na mitizamo tofauti.

Hapa kwetu, serikali yetu katika suala la kudhibiti viashiria na matukio ya udini, imekuwa legelege sana. Mafundisho ya kujenga chuki na kuhimiza mauaji yamekuwa yakifanywa wazi lakini serikali haichukui hatua zozote za msingi na za kuweza kuonekana. Umakini wa uongozi ni kufanyia kazi viashiria na siyo kusubiri mpaka watu wamekufa ndiyo mawaziri na Waziri Mkuu wanajipanga kusafiri kwenda kutoa rambirambi na kuunda kamati. Huo siyo utendaji makini wa serikali iliyo makini. Serikali ina vyombo vingi ikiwa ni pamoja na hiyo ambayo inaitwa ‘intelijensia’, kazi kubwa ya vyombo hivi ni kung’amua matukio yanayoweza kutokea baadaye kabla hayajatokea na kuyafanyia kazi.

Kwa upande mwingine utengamano wa Taifa lolote huchangiwa na umadhubuti wa viongozi wanaoiongoza serikali. Mwalimu Nyerere aliweza kuondoa ukabila na udini katika nchi hii kwa vile alikuwa ni kiongozi madhubuti, aliyekuwa na dira ya umoja, na mwenye dhamira halisi ya kuwaona watanzania wakiwa wamoja. Kwenye hilo mwalimu hakuwa na mzaha na yeyote, alilisimamia kwa nguvu zake zote, kiasi kwamba wanasiasa wenzie, watendaji wa serikali na viongozi wote wa dini walilijua hilo. Na pia aliweza kuchukua hatua kwa yeyote mwenye nia ya kueneza utengano wa kikabila au kidini bila ya kujali cheo chake au nafasi yake katika jamii. Serikali yetu ya leo haina ujasiri huo. Ndiyo maana watu wanaweza kusimama hadharani kuhimiza chuki, mapigano na mauaji, huku serikali ikiwa inaona na kusikia. Serikali inachofanya ni kulalamika badala ya kutenda. Serikali yetu inawaogopa viongozi wa dini hata pale wanapohamisisha chuki. Serikali yetu inaogopa wanasiasa hata pale wanapohamasisha chuki na utengano.

3.    VIONGOZI WA SIASA
Tangu mfumo wa vyama vingi uanze, CCM imekuwa ikitafuta kila njia ili kuendelea kubakia katika madaraka. Vyama vya upinzani kwa muda mrefu vimekuwa ni dhaifu kiasi kwamba CCM daima ilikuwa na uhakika wa kushinda kwa kishindo. Kadiri vyama vya upinzani jinsi vilivyokuwa vikipata nguvu, CCM imekuwa ikibuni njia mbalimbali za kuendelea kuungwa mkono, na njia hizi nyingine zimekuwa ni halali lakini njia nyingine zimekuwa ni chafu na zenye madhara makubwa kwa umoja wa Taifa letu.

Kwenye uchaguzi wa mwaka 2005, chama cha CUF kilionekana kuwa na nguvu sana, na CCM ili kuhakikisha inajipatia kura nyingi dhidi ya CUF ilieneza propaganda nyingi kuwa CUF ni chama cha kidini, chenye kuegemea kwenye uislam. Na mara nyingine kilitajwa kuwa ni chama chenye kupenda vita. Ikafikia mahali mpaka wakati fulani mkuu wa polisi alionesha majambia yaliyotajwa kuwa yaliingizwa nchini na chama cha CUF. Baada ya uchaguzi, CCM ikashinda, habari ya majambia hatukuisikia tena.

Mwaka 2010, CHADEMA kilionekana kuwa ni chama cha upinzani chenye nguvu sana. Mara kadhaa viongozi wa CCM ili kuwakatisha tamaa wapiga kura walisikika wakieleza kuwa CHADEMA ni chama cha wachaga na ni chama cha kikanda, huku kukiwa na kampeni za chini kwa chini zikifanywa na CCM kuonesha kuwa CHADEMA ni chama cha udini, kinaegemea kwenye ukristo. Maneno haya yanaendelea kutamkwa mpaka leo hii na viongozi wa juu kabisa wa CCM. Jambo la kujiuliza ni Je, hawa akina Nape na Mwigulu wanaotamka maneno haya wanafahamu athari yake kwa siku za mbeleni? Sheria ya kuanzisha vyama vya siasa inasema kuwa chama chochote cha kisiasa ili kiweze kusajiliwa ni lazima kiwe cha kitaifa, kisiwe cha kidini wala cha kikabila. Viongozi wakuu wa chama tawala wanatamka hadharani kuwa kuna vyama vya kidini, kikabila na kikanda, msajili yupo kimya, Rais yupo kimya, polisi wapo kimya, wakuu wa mikoa na wilaya nao wapo kimya! Hapo ndipo tunaposema kuwa tuna serikali, viongozi na taasisi za serikali ambazo ni legelege kupindukia ambazo hazina dhamira ya kudumisha umoja wa Taifa letu.

4.    HALI NGUMU YA KIUCHUMI
Uduni wa maisha ya Watanzania kiuchumi imekuwa ni kichocheo cha kupokea mafundisho potofu ya viongozi wa dini na wanasiasa. Mtu aliyekata tamaa ni rahisi sana kudanganywa na hata kushawishiwa. Aliye na njaa ukimwambia kuwa wewe una njaa kwa sababu mwenzio Yule anashiba anaweza kuamini hata bila ya kujiuliza ni kwa namna gani, hata kama huyo mwenzie naye ana njaa pia. Kuna wahubiri wa kiislam wanaoaminishwa waumini wao kuwa wakristo wote nchi hii ni matajiri, wamesoma, wanapendelewa katika ajira na wana maisha mazuri. Kuna watu wanayapokea mahubiri hayo ya uwongo bila hata ya kuyachunguza. Si waislam tu, lakini hata wakristo pia wapo wanaoamini kuwa baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wa kiislam wamekuwa hivyo kwa sababu ya kupendelewa na wakuu wa serikali.

Mwenye hali ngumu ya maisha na ambaye hana hekima, daima hufikiria kuwa lazima hali yake imesababishwa na mtu mwingine, akitokea mwendawazimu akamwambia ni huyo jirani yako, ni rahisi kukubali.

TUNAWEZA KUONDOKA VIPI HAPA TULIPO
1.    SERIKALI
Serikali ina nafasi ya pekee ya kututoa hapa mahali tulipojiingiza ambapo hapana faida yeyote. Ninapoongelea serikali, hasa kabisa namwongelea Rais wa Jamhuri wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete, Waziri Mkuu Mizengo Kayanda Pinda na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzanzibar Ali Mohamed Shein.

Kwa mtazamo wangu ni kuwa viongozi hawa hawajatimiza kikamilifu wajibu wao wa kusimamia umoja wa kitaifa kwa nguvu zao zote lakini kwa sasa haisaidii sana kuwalaumu bali tunawaomba wapokee ushauri wetu watanzania, na watimize wajibu wao kama walivyoapa.

Kinachotushangaza Watanzania, viongozi hawa wakuu nao wamekuwa wakilalamika badala ya kutenda. Watanzania tunajiuliza, Rais, Rais wa SMZ, Waziri Mkuu na Mawaziri mnapolalamika, mnataka nani atatue matatizo haya? Wananchi wa kawaida, kama nilivyo mimi, tuna haki ya kulalamika. Na tunapolalamika, tunamlalamikia Rais, Waziri Mkuu na Mawaziri. Rais, Waziri Mkuu na Mawaziri mnapolalamika, mnamlalamikia nani? Ninyi siyo watu wa kulalamika, ni watu wa kutenda, tunataka mtuambie mmefanya nini kuhakikisha Tanzania haina udini, ukabila wala utengano wowote kwa misingi hiyo.

Juzi wakati akielezea tukio la mauaji ya mchungaji Matayo yaliyofanyika kule Buseresere, Rais alisikika akisema kuwa mauaji hayo ni fedheha, na akaongeza kuwa kwenye vita vya kidini daima huwa hakuna mshindi. Mheshimiwa Rais anatakiwa afahamu kuwa Watanzania tulio wengi, wakristo, waislam, wapagani na hata wasio na dini, tunafahamu kuwa vita vya kidini havina mshindi, tunajua pia kuwa vita vya kidini haviwezi kumfaidisha yeyote au kumwathiri mtu wa dini fulani tu, hayo yote tunyaafahamu na wala hatuhitaji kuambiwa. Tunachotaka kuambiwa na Rais wetu, Waziri Mkuu wetu, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na serikali kwa ujumla, ni wanafanya nini kuhakikisha hakuna mifarakano ya kidini, wanaopalilia na kuweka mizizi ya udini wanafanywa nini, na kisha wanaviambia nini vyombo vya dola, wakuu wa wilaya na mikoa, na pia wanawapa maelekezo/amri gani viongozi wa dini. Rais wetu na serikali yetu, kwenye hili hatuhitaji maneno tunataka vitendo ambavyo vitatoa ujumbe sawia kwa kila anayehusika bila kujali ni kiongozi wa dini, chama cha siasa (hata kama ni kiongozi wa ndani ya chama chako).

Mapendekezo yangu kwa serikali ni kwamba inahitaji kufanya yafuatayo:
a.    Kufuta mihadhara yote ya kidini inayofanyika kwenye maeneo ya wazi. Mahubiri yote yafanyike ndani ya nyumba za ibada, na iwe ni marufuku kwa mhubiri yeyote kuweka vipaza sauti nje ya jengo la ibada
b.    Kila mhubiri ni lazima aidhinishwe na taasisi zinazosimamia dini. Kwa makanisa ni TEC, CCT na CPTC; na kwa waislam ni BAKWATA, BALUKTA, n.k.
c.    Kila mhubiri aliyeidhinishwa na taasisi yake, ahitajike kusaini mwongozo wa mahubiri yake ambapo itamkwe wazi mahubiri anayoruhusiwa kuyafanya ni yale tu yasiyohamasisha chuki dhidi ya dini nyingine bali yanayohamisha umoja wa waumini wake na watanzania wengine. Asiruhusiwe kuendesha mahubiri ya kiwanaharakati, kuhamasisha maandamano dhidi ya dini nyingine au taasisi za serikali
d.    Kila mhubiri ahitajike kupewa kitambulisho, na kusiwepo na yeyote atakayeruhusiwa kuwahubiria watu kama hajasajiliwa
e.    Upelekwe mswada bungeni utakao toa mwongozo wa wahubiri wa dini ili watakaokiuka waweze kuadhibiwa kisheria
f.     Kwa wanasiasa, kiongozi yeyote wa kisiasa atakayethibitika, iwe ni kwa kauli au vitendo akieneza propaganda kuwa chama fulani cha siasa ni cha kidini, kikanda au kikabila akamatwe, na sheria iwekwe wazi ambayo itatamka kuwa kiongozi wa namna hiyo atawekwa jela na kutokuruhusiwa kuwa kiongozi katika chama au taasisi yeyote ya kisiasa. Sheria ya namana hiyo pia iwabane viongozi wa dini watakaowaelekeza waumini wao kukiunga mkono au kutokukiunga mkono chama au mgombea wa chama chochote cha siasa.

2.    UONGOZI WA JUU WA SERIKALI
Uongozi wa juu wa serikali, kwa maana ya Mheshimiwa Rais, Waziri Mkuu na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanziba, ni lazima watoe kauli zilizonyoka, zenye msimamo thabiti, zisizo na unafiki wowote. Kauli kama ile ya Rais kuwa, ‘Kukojolea msahafu haikubaliki na kuchoma makanisa haikubaliki’, hazilisaidii Taifa, Rais mwenyewe, waumini wa dini za Tanzania wala serikali yake. Maana huwezi kulinganisha kosa la mtoto na mtu mzima, na ndiyo maana hata kwenye mahakama zetu, inapodhihirika kuwa mtenda kosa ni mtoto, mwenendo mzima wa kesi unabadilika. Rais alitakiwa kusema wazi, bila ya kuzunguka wala kumung’unya maneno kuwa, ‘Wale waliochoma makanisa kwa kisingizio cha mtoto kukojolea msahafu walitenda kosa la wazi. Aliyekojolea ni mtoto ambaye adhabu yake ni kucharazwa fimbo ili asirudie tena, maana ni mtoto. Pili, mtoto Yule hakutumwa na kanisa wala wazazi wake. Waliochoma makanisa ni watu wazima na hawakuwa na kisingizio chochote cha kufanya hivyo’.

Kauli ile ya Wasira nayo haikustahili kutolewa na kiongozi wa serikali. Wasira alisema kuwa haki ya kuchinja wanyama, kama ilivyozoeleka, ni ya waislam maana ni ibada. Alistahili kutumia hekima zaidi, angesema wazi kuwa serikali yetu haifungamani na dini yeyote lakini inaheshimu dini za watu wake. Mchinjaji wa nyama ni lazima atimize masharti ya leseni na afya lakini hekima ituongoze. Kuna wenzetu ambao dini yao inasema ni lazima mnyama achinjwe kwa masharti fulani, na kuna wengine ambao hakuna msisitizo huo. Na kisha angewauliza viongozi wa kikristo, Je, si busara tukawapa nafasi ya kuchinja wenzetu hawa wanaolazimishwa na matakwa ya dini yao? Kama kuna wengine ambao wanalazimishwa wasile nyama iliyochinjwa kwa masharti fulani wafuate taratibu zitakazowekwa ili nao waweza kuwa na uhuru wa kutimiza imani yao katika uchinjaji wa wanyama.

Serikali ni lazima iwe pro-active, leo hii tunaweza kusema kuwa tuendelee kama ilivyozoeleka lakini tutambue kuwa katiba yetu inatoa uhuru wa imani yeyote kuwepo nchini mwetu, kwa hiyo kuna uwezekano siku moja tukapata dini nyingine inayozuia kabisa waumini wake kula nyama iliyochinjwa kwa desturi ya kiislam au kikristo, tutafanya nini? Ndiyo maana ni vizuri kuwa na mwongozo kuliko kufanya mambo kwa mazoea tu.

3.    UONGOZI WA JUU WA KANISA
Mimi ni mkristo, na miaka yote ya uhai wangu nimekula nyama zilizochinjwa na waislam na wakristo, sijaona na wala siamini kama kuna athari nimepata katika imani yangu kwa sababu ya uchinjaji wa nyama niliyokula. Kwenye hili viongozi wa dini ya kikristo mseme kwa uwazi kabisa kama kweli uchinjaji wa wanyama ni hitajio la imani yetu. Siku zote hatujapewa mafundisho yanayotuelekeza tusile nyama zilizochinjwa na waislam. Siku zote hatujafundishwa hivyo. Nawaombeni mtumie hekima zetu katika hili maana tuwapo tayari kuwapa kitu fulani wale wa dini nyingine ndipo tunapokuwa na haki ya kuwataka wa upande mwingine kutupa sisi kile ambacho ni muhimu kwetu lakini siyo muhimu kwa upande wao.

Mimi siamini kuwa maelekezo ya viongozi wa dini ya kikristo kutokula nyama zilizochinjwa na waislam yanatokana na mafundisho ya kiroho bali ni hasira iliyojengeka kwa yale wanayotendewa wakristo. Wakristo wanaamini kuwa baadhi ya waislam wamekuwa wakitenda kila walitakalo hata kama ni kinyume cha sheria bila kukemewa au kuchukuliwa hatua na serikali. Kilio kikubwa cha wakristo ni kuhujumiwa kwa dini yao bila ya kupewa ulinzi wowote na serikali. Mwakajana zaidi ya makanisa 30, nani amekamatwa au kuchukuliwa hatua na vyombo vya serikali? Padre alishambuliwa kule Zanzibar, wangapi wamekamatwa na kuchukuliwa hatua na serikali? Maaskofu, wachungaji na wakristo wanabughudhiwa na kutishwa huko Zanzibar, ni watu wangapi mpaka leo hii wamekamatwa na kuchukuliwa hatua? Kwa nini serikali ilikimbilia haraka sana Mwanza na kutoa kauli kwa sababu tu ya waislam kulalamika kuwa wamelishwa nyama iliyochinjwa na mkristo lakini ikashindwa kuonesha uharaka huo huo kwa jambo kubwa zaidi kama lile la kupigwa risasi padre na kuchomwa makanisa? Mambo haya yamejenga chuki kwa wakristo dhidi ya serikali na kusababisha kukosa kustahimiliana hata katika mambo ambayo yangeweza kuvumilika kwaajili ya utengamano wetu.

Wakristo wanajiuliza, ingekuwaje katika nchi hii kama hayo makanisa yaliyochomwa ingekuwa ni misikiti? Ingekuwaje hao huyo mchungaji aliyechinjwa na mapadre waliopigwa risasi wangekuwa ni mashekhe? Ukipata majibu ya maswali haya, serikali ina kila sababu ya kutoka kwenye usingizi na kutoa kauli itakayowapa matumaini wakristo kuwa serikali inasimaia sheria na wala haiogopi dini fulani wala mtu yeyote.

Kwa viongozi wa kanisa, mnatakiwa kujua kuwa uvumilivu wenu katika madhila haya una faida kubwa zaidi kuliko kisasi cha aina yeyote. Mnatakiwa kuongozwa na roho na mafundisho ya Yesu Kristo. Japo ninafahamu kuwa busara ya kibinadamu inakataa kumvulia na kumsamehe muaji na mtesi wako lakini katika roho inawezekana. Mtambue kuwa kuna mamilioni ya waislam, ambao ni watu wema, ni majirani zetu, ni ndugu zetu na wafanyakazi wenzetu. Wanaoleta maafa haya ni waislam wachache sana, na kama ingekuwa ni waislam japo 1% wanatenda haya, tayari nchi hii isingeweza kukalika.

4.    UONGOZI WA JUU WA DINI YA KIISLAM
Kwa viongozi wa waislam, tafuteni njia ya kuongea na viongozi wa wakristo juu ya jambo hili. Kukutana nao kutaleta faraja kubwa na utengamano. Hiyo itasiaidia kuwapelekea ujumbe watanzania wote kuwa uislam haupo na hao wauaji. Kwa upande mwingine, kwa kufanya hivyo mtakuwa mnawaambia wauaji hao kuwa hawaungwi mkono na mafundisho ya uislam bali wanatumia jina la dini kutenda uovu. Jifunzeni kutoka kwa Rais wa Misri, Anuar El Sadat. Wakati Mehmet Ali Agca alipompiga risasi Papa John Paulo II, Sadat alimwandikia barua papa akisema kuwa anamwomba msamaha kwa kosa la Waislam kutaka kumwua Papa, kwa sababu Mehmet Ali Agca ni muislam mwenzetu.

Lakini pia viongozi wa waislam, wanawafahamu wahubiri wanaohubiri chuki, wawatamke hadharani kuwa hao siyo wahubiri wanaokubalika na taasisi zao za dini ya kiislam. Hiyo itasaidia kuwapa tahadhari waumini wema kutambua kuwa mafundisho wanayopewa na wahubiri hao ni kinyume na imani ya uislam.

5.    VYAMA VYA SIASA
 Msajili wa vyama vya siasa akutane na viongozi wa vyama vyote vya siasa. Vyama vyote vya siasa vielekezwe kuwa ni marufuku na ni kosa kwa kiongozi au mhutubiaji yeyote wa chama cha siasa kuwatangazia watu  kuwa chama fulani ni cha kidini, kikabila au kikanda. Kama kutakuwa na mtu yeyote ambaye anajua au anahisi kuwa chama fulani kinaendeshwa kwa misingi ya dini, kabila au kikanda, awasilishe taarifa hiyo kwa msajili wa vyama vya siasa. Msajili wa vyama vya siasa ataunda kamati ya kuchunguza tuhuma hizo, ikidhihirika kwa uhakika kuwa chama hicho siyo cha umoja wa kitaifa, kitafutwa. Hii ni baada ya kuwekwe vigezo vya wazi, vinavyoweza kuelezea kwa ufasaha chama kikikosa nini kitatamkwa kuwa siyo cha umoja wa kitaifa.

Kiongozi yeyote wa chama cha siasa ambaye atakituhumu chama cha kingine cha siasa kwenye majukwaa ya mikutano kuwa ni cha kidini, kikabila au kikanda, ashitakiwe, ikidhihirika alitamka apelekwe jela, na akitoka huko asiruhusiwe kuwa kiongozi wa chama chochote cha siasa.

HITIMISHO
Rais na serikali yake ndiyo wanategemewa na kila mtanzania kuwa kama walivyolipokea Taifa hili likiwa na umoja walikabidhi hivyo hivyo kwa wale watakaokuja kupokea uongozi. Hata kama kutakuwa na jema gani lililotendwa na serikali ya awamu ya nne, kama Taifa hili litaingia kwenye vita ya kidini, viongozi wa sasa watambue wataingia kwenye historia mbaya kabisa ya Taifa letu. Mna nafasi na uwezo upo, kama mkiwa na dhamira ya kuwafanya Watanzania waendelea kuwa wamoja zaidi. Rais Jakaya Kikwete akiweza kulisimamia hili, atakuwa ametenda jambo la faraja kubwa sana kwa kizazi cha sasa na vingi vijavyo. Ifahamike wazi kuwa, wakristo wengi wa Zanzibar hawaamini hata kidogo kuwa serikali ya Zanzibar na jeshi la polisi visiwani humo, wana dhamira ya dhati, ya kuona wakristo wanakuwa na haki ya kuishi Zanzibar na kuwa na haki ya kuabudu. Ndiyo maana hata baadhi ya waumini waliohojiwa leo, wamesema wazi kuwa hawawaamini viongozi wa SMZ, hawawaamini polisi wa Zanzibar, hawawaamini hata madaktari wa Zanzibar.

Kuendeleza umoja, mshikamano, upendo na umoja wa Watanzania inawezekana kama tukiwa na dhamira. Viongozi wetu, na hasa Rais wetu, anatakiwa kutambua kuwa zaidi ya 99.99%, waislam kwa wakristo, na hata wale wasio na dini wanataka amani. Je, unawaogopa na kutaka kuwafurahisha <0.01% ya watanzania huku ukiwasikitisha na kuwakatisha tama watanzania zaidi ya 99.99%?
Mpaka sasa, serikali ya awamu ya nne ndiyo imekuwa ya kwanza kushuhudia mauaji ya kidini. Hii siyo rekodi nzuri kwa serikali na kwa Rais Kikwete. Ukiona haya yanatendeka ni lazima kuna mahali serikali kama msimamizi mkuu wa kila kitu, haikutimiza wajibu wake. Serikali inatakiwa kusimama sasa na kutimiza wajibu wake, la sivyo Watanzania kwa kupitia bunge ni lazima iihoji serikali kama bado ina uwezo wa kuongoza nchi yetu au imeshindwa. Na kama serikali ikiona haiwezi kuyamaliza mambo haya, isione shida kwa kupitia utaratibu wa kisheria, kujiuzulu maana ikisubiri mpaka mambo yaharibike kabisa itakuwa ni kazi ngumu sana kuurudisha umoja wetu.

Chama cha Mapinduzi, ambacho ndiyo chenye serikali, kiihoji serikali ili kuwa na uhakika kama kweli serikali bado ina uwezo wa kuliongoza Taifa kwa kuwahakikishia watanzania amani, umoja na mshikamano.

Source: Bart Mkinga

MWANZA

No comments:

Post a Comment