WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, February 12, 2013

Jaji Warioba kukabidhi Katiba Oktoba



 Jaji Joseph Warioba
  •             Kwenda Bunge la Katiba Novemba

TUME ya Mabadiliko ya Katiba, inatarajia kukabidhi rasmi Ripoti yake na Rasimu ya Katiba kwa Marais Jakaya Kikwete wa Jamhuri ya Muungano na Dk. Ali Mohamed Shein wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Oktoba, mwaka huu, imefahamika.
Sambamba na hilo, Tume hiyo itawasilisha rasmi Rasimu ya Katiba hiyo katika kikao cha Bunge Maalumu la Katiba, Novemba 11, mwaka huu, kabla ya Bunge hilo kujadili Rasimu hiyo kuanzia tarehe hiyo hadi Januari 19, mwaka ujao wa 2014 na kuiridhia kuwa Katiba rasmi ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Mpango kazi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba, unaoonyeshwa katika kalenda ya mwaka huu ya Tume hiyo, kukabidhiwa kwa Ripoti na Rasimu ya Katiba Mpya kwa marais, na baadaye Rasimu hiyo kuwasilishwa mbele ya Bunge Maalumu la Katiba, itakuwa ndiyo mwanzo wa upatikanaji wa Katiba Mpya, ambayo uzinduzi wake unatarajiwa kufanyika rasmi katika kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, hapo Aprili 26, 2014.
Akizungumza na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari katika ofisi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba, jijini Dar es Salaam, juzi Jumatatu, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Warioba, alisema Tume yake ilikamilisha mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi mmoja mmoja kupitia mikutano ya wazi Desemba 19, mwaka jana, kabla ya Januari 7 hadi Januari 28 mwaka huu kukusanya maoni ya makundi maalumu ya kijamii wakiwamo viongozi wa sasa, wastaafu na watu mashuhuri.
Aliyataja makundi maalumu hayo kuwa ni pamoja na vyama vya siasa, ambapo Tume ilikutana na vyama 19 vya siasa kati ya 20 vyenye usajili wa kudumu, taasisi 22 za kidini, tasisi 72 za kiraia, taasisi 71 za kiserikali na viongozi na watu mashuhuri takriban 43 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Katika mkutano huo na waandishi wa habari, ambao Tume hiyo iliuitisha kwa lengo la kuelezea utaratibu wa uundwaji wa Mabaraza ya Katiba, Jaji Warioba alisema kabla ya Rasimu ya Katiba Mpya kukabidhiwa kwa marais Kikwete na Dk. Shein na baadaye Bunge Maalumu la Katiba kwa hatua ya mwisho, Rasimu hiyo itajadiliwa kwanza na wananchi kupitia mabaraza yao watakayoyaunda wenyewe kuanzia kwenye ngazi ya Kata kwa Tanzania Bara na Shehia kwa Tanzania Visiwani.
Aidha, alisema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, inataka wananchi wapate kwanza fursa ya kuisoma Rasimu hiyo, ikiwa ni pamoja na kuchapishwa katika magazeti mbalimbali kama sehemu ya kutoa elimu kwa umma, kabla ya kuwasilishwa rasmi katika Mabaraza hayo ya Katiba yatakayoitishwa na kuratibiwa na Tume hiyo.
Wachambuzi kadhaa wa mambo kuhusu mwenendo wa mchakato wa utoaji wa maoni kuhusu Katiba hiyo, wanasema wazi kwamba huenda ukatokea mvutano mkali baina ya vyama vikuu viwili vyenye ushawishi na ufuasi mkubwa kwa Tanzania Bara, Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika upatikanaji wa wajumbe wa Mabaraza hayo, kila chama kikitaka kiwe na uwakilishi mkubwa kwa lengo kulinda na kutetea matakwa na maslahi ya vyama hivyo.
Katika uundaji huo wa Mabaraza ya Katiba, mikoa yote ya Tanzania Bara, isipokuwa Dar es Salaam, kila Kata itatakiwa kuwa na uwakilishi wa wajumbe wanne. Kwa upande wa mkoa wa Dar es Salaam wenye idadi kubwa ya watu ikilinganishwa na mikoa mingine nchini, kila Kata itawakilishwa na wajumbe wanane, wakati kwa upande wa Tanzania Visiwani, kila Shehia itatakiwa kuwa na wajumbe watatu. Diwani wa kila Kata na kila Shehia ataingia moja kwa moja kuwa mjumbe na kufanya idadi hiyo ya wajumbe wanaotakiwa.
Wakati wa mchakato wa awali kabisa wa kuandikwa kwa sheria ya mabadiliko ya Katiba kulitokea mvutano mkali baina ya makada wa CCM na CHADEMA, kila upande ukisimama kidete kuhakikisha kwamba baadhi ya matakwa ya vyama vyao yanaingizwa ndani ya sheria hiyo, kiasi cha baadhi ya wabunge wa CHADEMA kususia upitishwaji wa sheria hiyo kwa kutoka nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.
Hali kama hiyo ndiyo inayotazamiwa na wachambuzi hao wa mambo kujitokeza katika mchakato huu unaofuata wa uundaji wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, yenye jukumu la kupitia na kutolea maoni Rasimu ya Katiba hiyo, kwa kila chama kati ya vyama vikuu hivyo viwili mahasimu kwa Tanzania Bara, lakini pia kwa CUF dhidi ya CCM kwa upande wa Zanzibar, kwa kila kimoja kujaribu kuhakikisha kwamba wajumbe walio wengi wanatokana na vyama hivyo kwa lengo la kutaka kupenyeza matakwa ya kila chama katika Rasimu hiyo kabla ya kuandikwa rasmi.
Kwa mujibu wa ratiba ya mpango kazi huo katika kalenda ya Tume hiyo ya mwaka 2013, kuanzia Jumpili iliyopita ya Februari 3 hadi Machi 4, mwaka huu, Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakuwa na kazi muhimu ya uchambuzi wa maoni mbalimbali yaliyotolewa na wananchi mmoja mmoja, makundi ya kijamii na ya viongozi na watu mashuhuri.
Aidha, kuanzia Machi 5 hadi Aprili 3, Tume itakuwa na kazi ya kuandika Rasimu ya Ripoti ya ukusanyaji wa maoni hayo, wakati kazi ya kuandika Rasimu ya Katiba itaanza Aprili 4 hadi Mei 2, mwaka huu. Kazi hiyo itafuatiwa na uchapwaji wa Rasimu hiyo utakayofanywa kati ya Mei 3 na 8, kabla ya kuingia kwenye hatua ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu Rasimu ya Katiba hiyo, kazi itakayofanyika kuanzia Mei 9 hadi Juni 7, mwaka huu.
Kati ya Juni 10 hadi Agosti 7, mwaka huu, mpango kazi huo unaonyesha kwamba Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakuwa na kibarua kingine kigumu cha kuratibu na kusimamia mikutano ya Mabaraza ya Katiba ya kila wilaya nchini, mabaraza ambayo yatakuwa na jukumu la kupitia, kujadili na kutolea maoni Rasimu hiyo ya Katiba.
Kalenda hiyo ya kazi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba, inaonyesha zaidi kwamba kati ya Agosti 12 na Septemba 10, kutakuwa na kazi ya kuchambua maoni yatakayotokana na Mabaraza ya Katiba, kabla ya Ripoti na Rasimu ya Katiba hiyo kuingizwa mitamboni tena kwa ajili ya kuchapwa, kazi itakayofanyika kuanzia Septemba 11 hadi Septemba 30.
Jumanne ya Oktoba Mosi, mwaka huu, Tume ya Mabaduiliko ya Katiba itakabidhi Ripoti na Rasimu ya Katiba Mpya kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Kikwete, na siku ya Alhamisi ya Oktoba 3, mwaka huu, Tume hiyo itakabidhi Ripoti na Rasimu ya Katiba kwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
Habari zinasema baada ya marais hao kukabidhiwa Ripoti na Rasimu ya Katiba, watalazimika sasa kukutana na kuunda Bunge Maalum la Katiba kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kabla ya Bunge hilo nalo kupokea Rasimu hiyo ya Katiba na kuanza kuijadili katika kikao chake cha kwanza kitakachoanza Novemba 11, mwaka huu hadi Januari 19, 2014.
Akitangaza mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya mapema mwaka jana, Rais Kikwete aliiagiza Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuhakikisha inakamilisha kazi hiyo mapema iwezekanavyo ili Katiba Mpya iweze kuzinduliwa rasmi katika kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ulioasisiwa rasmi na waasisi wa Taifa hili, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, Aprili 26, 1964.
Source: Raia Mwema

No comments:

Post a Comment