WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, February 8, 2013

Haya yanaweza kuikwamisha Chadema 2015



 SIKU zinazidi kusogea huku tambo za kisiasa zikizidi kuhusu nafasi ya vyama vya siasa katika uchaguzi mkuu wa 2015. Tambo hizo hasa ni kwa vyama vikubwa – CCM na Chadema.
Chadema kimeanza kuandaa mashambulizi ya kuchukua madaraka ya nchi kutoka mikononi mwa CCM, lakini hiyo haitakuwa kazi rahisi kwa kuwa CCM nayo inaelekeza mashambulizi kwa Chadema kama chama, na wanachama binafsi, hasa Dk Willibrod Slaa ambaye jina lake limeendelea kusimama kama alama ya chama hicho.
Chama hicho kimetokea kuwa ni mwiba mkali kwa CCM, na kuwa kivutio kwa idadi kubwa ya vijana kutokana na ushawishi unaojidhihirisha kutoka kwa wabunge na makamanda wa chama hicho.
Mbali na ushawishi huo, pia chama hicho kimekuwa kikijivunia mipango yake mahususi, kama operesheni za ujenzi wa chama, kurudisha madaraka kwa wanachama kupitia Sera yake ya majimbo na shughuli zingine.
Januari 27 na 28, mwaka huu chama hicho kimefanya vikao vyake vya juu – Kamati Kuu na Baraza Kuu – na kujadili ajenda mbalimbali ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha kinashinda Uchaguzi Mkuu 2015.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika hatua iliyopo ni kuzingatia uamuzi ya kuwapata viongozi na kuweka mpango kazi wa kuongeza nguvu ya umma.
“Tunaanza ujenzi wa chama ili kujiimarisha zaidi katika harakati za kushinda uchaguzi mkuu ujao, lakini pia tunajiweka sawa kwa namna tutakavyosimamia ahadi zetu za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kwa kuishinikiza Serikali kutekeleza,” anasema Mnyika. Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ametangaza vita ya kisiasa, akisisitiza kuwa “Mwaka 2013 ni mwaka wa nguvu ya umma.”
Anasema chama hicho kimeweka mikakati ya kujijenga kuanzia matawi hadi taifa na kutawashughulikia wanachama wanaodaiwa kutumiwa na CCM kuanzisha migogoro ndani ya chama.
Kauli hiyo ya mwenyekiti, ni kinaashiria kuwa ndani ya chama hicho kuna migogoro ambayo isipoangaliwa na kutatuliwa katika kipindi hiki, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema inaweza kuwa kikwazo kwa harakati na mipango yake ya kushika dola.
Uamuzi kufuata Katiba
Profesa Chris Maina wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema Chadema inapaswa kuhakikisha inafanya uamuzi na kutekeleza mipango yake kwa kufuata Katiba, ili kuhakikisha inaendelea kuimarika zaidi mpaka kufikia uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Anasema endapo migogoro inayodaiwa kuwamo itaendelea ndani ya chama hicho, na chenyewe kikafanya uamuzi bila kufuata katiba yake, basi hakutakuwa na mafanikio ndani ya chama hicho.
“Ninachoamini mimi wanatakiwa kutekeleza mipango yao kwa kufuata katiba, ndio inayoweza kuwaongoza wakasimamia misingi yao, hata migogoro na mivutano haitaweza kujitokeza, mhimili wa chama ni makubaliano ya kufuata misingi na kanuni ya katiba,” anasema Profesa Maina.
Uteuzi usio wa haki
Jambo lingine ambalo anasisitiza Profesa Maina linalotakiwa kuepukwa ni makosa katika uteuzi wa wagombea katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika, ili kujenga dhana ya uaminifu kwa Watanzania wanaotakiwa kutenda haki katika uchaguzi huo.
Profesa Maina anasema endapo chama hicho kinahitaji kufanikiwa katika uchaguzi mkuu ujao, kinapaswa kumchagua kwa umakini kiongozi wanayeamini kuwa atastahili kusimama katika uchaguzi mkuu.
“Waangalie mfano wa Kenya na vyama vingine, utakuta mgombea mwingine hakubaliki kwa wananchi lakini anakubalika ndani ya chama, na mwingine hakubaliki kwenye chama chake lakini ndio anayeonekana kipenzi cha wananchi, anasema Profesa Maina bila kutaja majina.
Mbinu za CCM
Mkazi na mfanyabiashara wa Dar es Salaam, Alfani Mohamed anasema chama hicho kinapaswa kuwa makini na mbinu mbalimbali zinazotoka upande Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwani kumbukumbu zinaonyesha kuwepo kwa vyama vilivyowahi kuwa na nguvu na baadaye kudhoofishwa.
“Kuna vyama viliundiwa njama mpaka leo vimeshakosa nguvu tena, kulikuwa na NCCR- Mageuzi baadaye kikafuata CUF, lakini viko wapi kwa sasa, kuna utekelezwaji wa mbinu kabambe za kuvidhoofisha kwa hali na namna yoyote,” anasema Mohamed.
Mfumo wa uchaguzi
Moja ya vikwazo vinavyoweza kukwamisha ndoto za Chadema ni kutokuwapo uhuru kwa Tume ya uchaguzi iliyopo sasa, ambayo mwenyekiti, watendaji na makamishna wake wanateuliwa na Rais ambaye ni mwenyekiti wa chama shindani.
Kiongozi wa kituo cha madereva wa taksi, Tabata, Kanaluza Abdi anasema mfumo huo ni tatizo linaloweza kuondoa imani ya wapigakura kwa kuona haki haiwezi kutendeka.
“Kama mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi amechaguliwa na Rais ambaye pia ni mhusika katika uchaguzi, sio rahisi kupata matokeo mazuri, labda Katiba ibadilishe suala hilo kabla ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu wa 2015, vinginevyo Chadema haitaweza kuchukua nchi,” anasema Abdi.
Muundo wa chama
Mfanyabiashara na mkazi wa Buguruni, Dar es Salaam, Mohamed Salim (27) anasema kuna uwezekano mkubwa wa Chadema kushindwa kwenda Ikulu kutokana na muundo wake kwa sasa.
Anasema chama hicho bado hakijashuka hadi chini kwa wananchi, kipo mijini tofauti na CCM ambacho kimejikita zaidi katika mashina ya vijijini.
“CCM bado wana mashina mengi vijijini ukienda mpaka leo kuna watu wanaamini na kusema CCM ikiondolewa madarakani kuna vita itatokea, dhana hiyo ni kwa sababu ya kukosa elimu, unadhani mpaka kizazi hicho kitoweke ni lini,”anahoji Abdi.
Idadi ya wapiga kura
Kwa mujibu wa Alfani Mohamed, asilimia kubwa ya wapigakura wanaoiunga mkono Chadema wengi ni vijana, wakiwamo walio na sifa na wasio na sifa ya kupiga kura.
Anasema kumbukumbu zinaonyesha kuwa wanawake na wazee ndio hujitokeza katika kipindi cha uchaguzi kupiga kura, tofauti na vijana ambao huonekana mstari wa mbele katika mikutano ya kampeni.
“Uchaguzi uliopita kulikuwa na watu karibu milioni 19 waliojiandikisha, lakini kwenye matokeo ikabainika ni asilimia 42 tu kati hao ndio walijitokeza, sasa ukiuliza unaambiwa vijana ndio wengi hapa nchini, sasa sijui huwa wanakwenda wapi wakati wa kupiga kura,”anahoji Mohamed.
“Endapo vijana watahamasika kupiga kura, Chadema wakasimika matawi vijiji vyote nchi nzima na elimu ikatolewa juu ya umuhimu wa kura ya Mtanzania, katika uchaguzi huo wa 2015, Chadema itachukua nchi, ila naona muda uliobakia si haba,” anasema Abdi.
Ahadi zisizotekelezeka
Hata hivyo, kada mmoja wa CCM, Paul Makonda anasema chama hicho kina tatizo la kutangaza ahadi zenye matumaini hafifu ya kutekelezeka na kuwafanya watu wajenge hofu katika utekelezaji wake.
Makonda anasema ahadi hizo zinajenga tafasili ya Chadema kuonyesha shauku ya kutamanani kuingia madarakani badala ya kuangalia njia mbalimbali za kuisaidia jamii kabla ya kuingia madarakani ili kujijengea uaminifu zaidi. “Angalia mfano, utaona mara nyingi wao wanatumia mianya ya changamoto kama daraja la kujijengea umaarufu, utakumbuka, migomo ya walimu, madaktari na sasa hivi wamehamia Mtwara, haijawahi kutokea Chadema wakahamisha wananchi kutii sheria za nchi au kuandaa makundi ya kuelimisha kwa mambo mbalimbali,” anasema Makonda. 
SOURCE: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment