WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, February 9, 2013

Mbunge asema ipo siku watavunja viti


VURUGU BUNGENI

 Naibu Spika Job Ndugai akizozana na Tundu Lissu nje ya ukumbi wa Bunge
  • Ni Peter Msigwa wa Iringa Mjini-CHADEMA
  • Siri zafichuka, Tundu Lissu achafuliwa
  •  Mnyika, Nassari kuhojiwa Kamati ya Maadili

WAKATI Spika wa Bunge, Anne Makinda akiahirisha hoja binafsi za wabunge kutokana na vurugu za bungeni Jumatatu wiki hii, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, amesema upendeleo wa Spika ukizidi, kuna siku watavunja viti vya Ukumbi wa Bunge.
Msigwa alitoa onyo hilo alipozungumza na mwandishi wetu aliyeko Dodoma kwa ajili ya vikao vya Bunge, akionekana kukerwa na kile wanachokiita; “Upendeleo wa Spika kwa wabunge wa CCM.”
“Tumekwishakata rufaa nyingi hata dhidi ya Spika mwenyewe hakuna hatua zinazochukuliwa. Hoja zetu zinatupwa bungeni...kuna upendeleo wa wazi, achana na vurugu zile, mimi nasema ipo siku kama hali hii itaendelea tutavunja viti bungeni,” alisema Msigwa.
Kutokana na uzito wa kauli hiyo, mwandishi wetu alimuuliza; “..nikunukuu kuhusu kauli hii gazetini? Naye akajibu; “Nukuu, wala usiwe na wasiwasi ndiyo hali halisi, uonevu ukizidi watu hujitetea kwa taratibu zao. Hatupendi kufika huko, wajirekebishe. Wasitusukume kwenda huko.”
Maelezo ya Spika
Jumanne wiki hii, Spika Makinda alitoa maelezo bungeni kuhusu vurugu hizo za Jumatatu wiki hii, wakati Naibu Spika Job Ndugai, alipoongoza mjadala wa hoja binafsi kuhusu maji safi na maji taka ya Mbunge wa Ubungo- Dar es Salaam, John Mnyika.
Katika kikao hicho, wabunge wa upinzani walisimama na baadhi kuanza kuzomea hovyo, wakiashiria kutokukubaliana na uamuzi wa kumruhusu Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, kutoa hoja ya kuondoa hoja ya awali ya Mnyika, kwa maelezo kuwa, Dar es Salaam imepewa bajeti kubwa na fedha nyingi za maji kuliko mikoa mingine na zaidi ya hapo, miradi mingi ya maji inafanyika kwa hiyo hoja iwe ni tatizo la maji nchi nzima.
Kwa mujibu wa maelezo yake kuhusu vurugu hizo, Spika Makinda alisema Kamati ya Uongozi ya Bunge imekemea utovu wa nidhamu wa wabunge waliozomea, lakini pia imeahirisha hoja binafsi zilizopangwa kujadiliwa katika mkutano wa sasa wa Bunge, unaokwisha mwishoni mwa wiki hii.
Mbali na hayo, Spika alisema waliohusika katika fujo hizo watafikishwa katika Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge kwa hatua zaidi. Kwa kadiri ya picha za televisheni zilioonyeshwa moja kwa moja na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) wakati wa fujo hizo, wabunge John Mnyika, Tundu Lissu, Peter Msigwa, Moses Machali na wengine wengi wa kambi ya upinzani walionekana wakziomea na mwandishi wetu aliyeko Dodoma alishuhudia hali hiyo moja kwa moja bungeni.
Lakini katika kambi hiyo ya upinzani, wapo wabunge ambao walisimama kuungana na wenzao bila kupiga kelele ambao ni pamoja na Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, James Mbatia, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, wabunge wa CUF wengi hawakusimama wala kuzomea.
Kwa hiyo, kwa maelezo ya Spika, wabunge Mnyika, Lissu, Machali ni kati ya watakaofikishwa Kamati ya Maadili kwa ajili ya mahojiano. Baadhi ya wabunge ambao hawakufanya fujo nao pia wataitwa kama sehemu ya ushahidi.
Siri za mtikisiko
Siri za mtikisiko huo bungeni wenye taswira ya upendeleo kwa wabunge wa CCM dhidi ya wabunge wa upinzani msingi wake unatajwa ni kanuni kuu ya kidemokrasia; “wachache wasikilizwe, wengi waamue.
Ndani ya siri hizo inaelezwa kwamba kukwama kwa hoja binafsi za wabunge wa upinzani msingi wake ni kushindwa kufanya ushawishi (lobbying) kabla ya hoja hizo hazijawasilishwa bungeni, lakini pia ushindani wa kutumia Bunge kama jukwaa la kukuza siasa za vyama ni tatizo jingine.
Katika mabunge mengi duniani, na hasa yanayofuata mfumo wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola, wabunge wenye idadi ndogo bungeni wamekuwa wakifanya ushawishi kwa wenzao walio wengi nje ya Bunge, ili hoja zao zenye maslahi mapana kwa sekta au nchi kwa ujumla zifanikiwe.
Mjumbe mmoja wa Kamati ya Uongozi ya Bunge inayoundwa na wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge, pamoja na Spika, Naibu wake na Waziri Mkuu, amesema; “Siri ya hiki kinachoonekana upendeleo ni kambi ya upinzani kushindwa kutumia mbinu za mabunge ya Jumuiya ya Madola. Kanuni kuu ya kufanya uamuzi bungeni ni kuhoji pande mbili zinazogongana katika hoja husika.”
“Kwa mfano, Mnyika (John Mnyika- Mbunge wa Ubungo Dar es Salaam) ameleta hoja kuhusu kuboreshwa kwa huduma ya maji safi na maji taka Dar es Salaam, Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe ameleta hoja ya kutaka hoja hiyo iondolewa kwa sababu kwanza Dar es Salaam imepewa bajeti kubwa ya kutatua tatizo hilo kuliko mikoa mingine nchini.
“Sasa ilibidi hizi hoja mbili zijadiliwe na wabunge na kisha uamuzi ufanyike, lakini mwenendo wa mjadala inategemea nani alifanya vizuri kazi ya kushawishi wabunge kabla ya kikao na hata wakati anapowasilisha hoja yake,” alieleza mjumbe huyo.
Wakati mjumbe huyo wa kamati ya uongozi akisema hayo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika kwa upande wake bado anaamini ameonewa na anakusudia kukata rufaa kupinga hoja yake kutupwa bungeni.
Hatua hiyo ya Mnyika inaungwa mkono na wabunge wengi wa Kambi ya Upinzani, ambao ni pamoja na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye ndiye aliyeongoza wabunge kusimama bungeni na kuzomea kwa lengo la kuonyesha kupinga uendeshaji wa kikao cha Bunge uliofanywa na Naibu Spika, Ndugai.
Lakini kuhusu ushawishi Msigwa ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii, anasema; “Hoja za wapinzani zipo wazi kabisa, kwa nini ufanye lobbying? Mimi nitawasilisha hoja binafsi kuhusu meno ya tembo kama kuna mbunge anahitaji kushawishiwa ili aone umuhimu wa hoja hii wakati tembo wanauawa basi huyo ana matatizo na hastahili kuwa mbunge.”
Msigwa anaongeza: “Kwanza lobbying ni sawa na compromise, hivi mimi nijishushe na kujipendekeza kwa Waziri Mkuu, au mawaziri wengine ili iweje? Si wao walioniingiza bungeni na wala si wao watakaonirudisha bungeni. Ni bora nionekane kama nilivyo, uhalisia wangu ujioneshe na si vinginevyo.”
Wakati hayo yakiendelea, Naibu Spika Ndugai, ambaye ndiye aliyeahirisha Bunge juzi Jumatatu kutokana na zomeazomea iliyofanywa na baadhi ya wabunge wa upinzani, amemweleza mwandishi wetu akisema; “Kilichotokea ni kwamba, Mnyika alifuata taratibu zote za kuwasilisha hoja binafsi, hoja hiyo ikapitishwa kwa taratibu za Bunge na wabunge wote kupewa nakala ya hoja hiyo.
“Lakini kabla hoja hiyo haijajadiliwa bungeni, Mnyika akawasilisha nyongeza ya marekebisho, akitaka hoja yake ihusu tatizo la maji kwa upana zaidi na si Dar es Salaam pekee. Marekebisho yake ni sawa na kuandika hoja nyingine mpya, kwa hiyo kiutaratibu alitakiwa ama kuendelea na hoja yake ya zamani au kuleta hoja mpya kwa kufuata taratibu za awali, yeye akaamua kwenda na hoja ya awali na Waziri akaleta hoja yake kuhusu suala la maji nchi nzima akisema Dar es Salaam imepewa bajeti kubwa kuliko mikoa mingine na miradi inaendelea kwa hiyo hoja ya Mnyika iondolewe,” anasema Ndugai.
Alipoulizwa ni kwa nini alimruhusu Waziri Maghembe kuchangia hoja ya Mnyika kwa zaidi ya dakika 15 walizopewa wabunge wengine, Ndugai alisema; “Waziri alikuwa akiwasilisha hoja yake kutaka hoja ya Mnyika iondolewe, kwa hiyo kwa utaratibu alikuwa na nusu saa ya kufanya hivyo.”
Ndugai alionyesha kusikitishwa na kitendo cha wabunge kuzomea bungeni, akisema ni “uhuni usiokuwa na mafunzo yoyote kwa vijana wenye kiu ya kujifunza kuwa viongozi bora wanaoshindana kwa hoja na si vihoja.”
Kwa upande wake, Mbunge wa NCCR-Mageuzi, Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila alisema anaunga mkono kitendo cha wabunge wa upinzani kusimama wote bungeni ili kupinga uendeshaji wa kikao cha Bunge lakini haungi mkono tabia ya kuzomea na kupiga kelele hovyo iliyofanywa na baadhi ya wabunge hao wa upinzani.
“Bunge linaangaliwa na watu wengi wastaarabu na hata wapenda fujo, kuna viongozi wa dini, maaskofu na mashekhe, wasomi na wasio wasomi, wanachotaka kuona ni mvutano wa uzito wa hoja na si kelele za kuzomea, nadhani baadhi yetu tumevuka kiwango,” alisema Kafulila.
Katika hatua nyingine, taarifa zaidi zinaeleza kwamba kikao cha dharura cha Kamati ya Uongozi ya Bunge kimemshambulia Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, kwa kudai kila anapokasimishwa madaraka na Freeman Mbowe kuongoza Kambi ya Upinzani Bungeni, amekuwa akivuruga mwenendo wa mijadala.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kamati hiyo ya uongozi, baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wameshangazwa na wabunge wengine wa Kambi ya Upinzani kuburuzwa na Lissu katika kila jambo bila kuchuja mambo hayo kwa kuzingatia uelewa wao binafsi na si uelewa wa mtu waliyemwita mvurugaji wa mijadala bungeni.
Ni kutokana na hali hiyo, inaelezwa kuwa baadhi ya wajumbe wanaamini mwenendo wa Lissu kila anapoachwa kuongoza Kambi ya Upinzani Bunge si mzuri, akidaiwa kutumia muda mwingi kukatisha wazungumzaji hata wale wa upinzani.
Vurugu za mabunge duniani
Vurugu si tu za kuzomea bali hata za kupigana na kuharibu vifaa vya ukumbi wa Bunge hutokea katika mabunge kadhaa duniani.
Kwa mfano, Novemba mwaka 2008, vurugu zilizuka katika Bunge la Ukraine wakati baadhi ya wabunge walipotaka kushinikiza kupigwa kura ya kumwondoa Spika wa Bunge hilo, Arseniy Yatsenyuk.
Bunge la Mexico pia liliingia katika rekodi ya vurugu, Desemba mwaka 2006, vurugu hizo zilikuwa zikionyeshwa moja kwa moja (live) na kituo cha televisheni nchini humo huku wabunge wakitwangana ngumi.
Juni, 2010 nchini Nigeria, ngumi zilipigwa baada ya baadhi ya wabunge kusimamishwa ubunge kutokana na shutuma walizopata kuzitoa kwamba Spika wao alikula rushwa.
Bunge la Korea Kusini ndiyo mara kadhaa limepata kuwa uwanja wa mpambano wa ngumi. Machi, mwaka 1998, wakati wa upigaji kura za kumuidhinisha Waziri Mkuu Kim Jong-pil, baadhi ya wabunge walirejesha karatasi tupu za kura zikiwa hazikuandikwa chochote, na hapo ngumi zilianza baada ya baadhi ya wabunge kutaka kura hizo zitambuliwe zimeharibika, na wengine wakibisha.
Zimewahi pia kuzuka vurugu wakati wa jaribio la kutaka kumng’oa madarakani, Machi 2004, Rais wa nchi hiyo, Roh Moo-hyun, wabunge wafuasi wa Rais wakitwangana na wabunge wa upinzani.
Lakini Julai, mwaka 2009, ngumi zilipigwa bungeni Korea Kusini baada ya kutokea mvutano kuhusu Muswada wa Mabadiliko katika sekta ya vyombo vya habari.
Katika mvutano huo, wabunge wa upinzani walitanda na kuzuia njia ya Spika kuingia bungeni, na wabunge waliokuwa wakipinga kitendo hicho waliinuka na kuanza mpambano, lakini hatimaye muswada huo ulipitishwa.
Huko Taiwan, sehemu inayokusudia kujitenga na China ili iwe nchi rasmi inayotambulika duniani, vurugu ziliwahi kutokea katika Bunge lao.
Huko, mwaka 1995 iliwahi kuelezwa kwamba pengine baadhi ya wabunge wangepewa nishani ya Nobel kwa kuwa mstari wa mbele kupambana kwa ngumi bungeni badala ya kuchambua mambo kwa ajili ya kukabiliana na mataifa mengine katika masuala mbalimbali, yakiwamo ya maendeleo.
Machi, 2004, vurugu ziliibuka kati ya wabunge wa upinzani na chama tawala, baada ya kuwapo mvutano wa kutaka kura zilizopigwa wakati wa uchaguzi wa rais zirudiwe.
Lakini Mei, mwaka 2004, wabunge Chu Hsing-yu na Lai Ching-teh, walitwangana ngumi baada ya ubishi kuhusu taratibu za Bunge, huku vituo ya televisheni vikionyesha Mbunge Chu, akimkwida mwenzake, Lai, huku akijaribu kumpiga ngwara.
Katika Bunge la Uingereza imewahi kutokea wabunge wa upinzani na wale wa upande wa utawala kuchorewa mstari wa kuwatenganisha bungeni kwenye zuria.
Mstari huo mwekundu ulichorwa mbele ya mabenchi ya pande hizo mbili, mbunge wa upande mmoja hakuwa akiruhusiwa kuvuka kwenda upande mwingine, ikihofiwa anaweza kuvuka kwenda kumshambulia mbunge wa upande mwingine, na kwa wakati huo wabunge walikuwa wakiruhusiwa kuingia na silaha bungeni.
Vurugu nyingine zimewahi kutokea mwaka 1972 katika Bunge la Uingereza na mwaka 1976.
Marekani, Februari mwaka 1798, kuliwahi kuzuka vurugu, msingi wake ukiwa ni katuni ya kisiasa na hatimaye kuzua ugomvi kati ya wabunge Roger Griswold kutoka Connecticut na Matthew Lyon.
Wakati huo huo, mwandishi wetu Hafidh Kido anaripoti kwamba Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willbrod Slaa amewataka wabunge wa chama hicho kususia kikao cha Tume ya Haki na Madaraka ya Bunge, ikiwa wataitwa kujieleza kutokana na mambo yaliyotokea bungeni jana na juzi, hadi hapo Spika wa Bunge, Anne Makinda atakapotoa hadharani matokeo ya rufaa kumi walizoweka tangu Makinda kushika kiti hicho.
Akizungumzia msimamo wa CHADEMA mbele ya waandishi wa habari katika Makao Makuu ya chama hicho jana, Dk Slaa alitamka kulaani kiti cha Spika na wale wote wanaoendesha majukumu yao katika Bunge la Tanzania kwa kufuata matakwa ya vyama vyao.
“CHADEMA tunalaani kiti cha Spika na wale wote walioonyesha ubaguzi wa wazi katika kuondoa hoja tatu za wabunge John Mnyika (CHADEMA), James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Dk Hamis Kigwangala (CCM) kinyume na kanuzi ya Nane ya Bunge inayotamka Spika hatakiwi kuwa na upande,” alisema Dk Slaa na kuongeza:
“Ninachotaka kuwaeleza wabunge wangu wa CHADEMA, ikiwa wataitwa katika Tume ya Haki na Madaraka ya Bunge wasiende. Wamweleze Anne Makinda wapi zilipo zile rufani 10 zilizokatwa na CHADEMA tangu aingie madarakani. Kwanza watoe majibu ya rufani hizo tulizokata, tena mbele ya ukumbi wa Bunge baada ya hapo wabunge wangu watakuwa tayari kusimamishwa mbele ya tume hiyo.
“Kinachotokea sasa bungeni mjini Dodoma ni kuendesha vikao vya Bunge kwa chuki, uongo na kutofuata haki. Bunge ndiyo sehemu ya kupatikana haki na kutungwa sheria lakini pamegeuka kichaka cha udhalilishaji, uovu, chuki na ubaguzi wa kichama.
“Enzi za uspika wa Samwel Sitta kulikuwa na ubabe kidogo lakini namsifia Sitta kwani hakupenda kupindisha haki na kanuni za bunge ni bora Sitta angeendelea kuwa Spika ni mtu makini sana. Bunge haliwezi kuwa na haki wacha nikuchekeshe kamati ya uongozi wa wabunge wa CCM ina wajumbe 18 ambao ni viongozi wa kamati kuu ya chama chao. Katika kamati hiyo hata maspika wanaingia hoja zote zinazotakiwa kujadiliwa katika kikao cha bunge lazima zijadiliwe na kamati hiyo ya wabunge 18 wa CCM unadhani lini haki itapatikana, lazima tuzichukue hoja zetu na tuzipeleke kwa wananchi na tukifanya hivyo wasituite wachochezi.”
Source: Raia Mwema

No comments:

Post a Comment