WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, February 16, 2013

KILIO cha Taifa letu ni uongozi!


 
Ili tupige hatua kutoka hapa tulipo sasa, tunahitaji kiongozi bora, kiongozi mzalendo, kiongozi anayeyaishi maisha ya Watanzania.
Hiki ni kilio cha Taifa letu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015. Kuna uvumi kwamba wapo wanaojipanga vizuri kutumia kila njia kujisafisha; kosa la chama ni kushindwa kuwafukuza na kuwaachia uhuru wa kupima wenyewe na kuondoka; umekuwa ni wakati mzuri kwao kufanya mbinu za kujisafisha; wana fedha za kufanya hivyo na wana watu wengi nyuma yao ( Watu ni fedha, maana Watanzania tunanunuliwa kama bidhaa mnadani – mwenye fedha nyingi ni lazima awe na watu wengi nyuma yake), wanaamini ni haki yao kujisafisha maana ndani ya CCM kuna wachafu kama wao.
Inawezekana kabisa kwamba hoja ya kuandaliwa watu wa kumrithi Mwenyekiti wa chama, Jakaya Kikwete, ni ya kutungwa kwa lengo la kumchafua, hoja ihame kutoka kwa watuhumiwa ufisadi hadi kwenye kuandaa watu tena wa dini moja!
Lakini nimekuwa nikijiuliza hivi Hata hivyo Kikwete, amwandae nani ndani ya chama chake cha CCM?
Ni nani ndani ya CCM anaweza kusimama na kumnyoshea mwenzake kidole? Majina yote tunayoyajua na kuyasikia kila wakati yamechafuka! Nani ndani ya CCM ameshinda uchaguzi bila kutumia fedha? Ni nani kiongozi wa CCM anaishi maisha ya kawaida ya wananchi kama viongozi wale wa enzi za Mwalimu Nyerere?
Nafikiri tatizo kubwa ambalo ni lazima sote tulifanyie kazi ni: Nani atalivusha Taifa letu kutoka hapa lilipo? Hiki ndicho kilio kikubwa cha Taifa letu! Ni mtu gani huyu atakayeweza kulirudisha Taifa letu katika njia sahihi aliyoiandaa Mwalimu Nyerere?
Taifa letu likarejea kuwa juu ya udini; likawa juu ya ukabila na ukanda? Serikali ikawa ya wakulima na wafanyakazi badala ya hali ya sasa hivi ya kutekwa na wafanyabiashara na wenye fedha?
Ni mtu gani atakayevunja utamaduni huu kwamba ni lazima Tanzania iongozwe na chama kimoja cha siasa (CCM). Ni mtu gani huyu atakaye vunja utamaduni huu uliyojengeka wa kushughulikia mchakato wa kuingia madarakani badala ya kushughulikia mchakato wa kuleta maendeleo?
Sasa hivi makundi yanajengwa na fedha zinatafutwa. Wanaoutaka ubunge wanaanza kujiandaa, wanaoutaka urais wanaanza kujiandaa. Fitina zinaanza, chuki na wakati mwingine hata maisha ya watu kupotea. Maana hawa wanaotafuta fedha nyingi, wako tayari hata kujiingiza kwenye madawa ya kulevya. Kuna ushahidi wa kutosha kwamba Tanzania ni njia ya kupitishia madawa ya kulevya.
Kuingilia mtandao huu wa madawa ya kulevya kwa lengo la kuusimamisha ni kutafuta kifo. Wanaofanya biashara hii haiwezekani kuwa hawajulikani, na hawawezi kukamatwa.
Ni mtu gani atavunja utamaduni uliojengeka wa kutumia fedha kuingia madarakani? Mtu akachaguliwa kwa uwezo wake na uzalendo wake? Tumejenga utamaduni kwamba wananchi hawawezi kujichagulia mwakilishi wao kwa uhuru bila kununuliwa.
Hili ndio tatizo letu kubwa na hiki ndicho kilio cha Taifa. Tunaongozwa na fedha badala ya kuongozwa na fikira! Tumepotea njia, tuko gizani na tunahitaji mwanga mpya! Na mwanga huu si kazi ya mtu mmoja.
Kikwete peke yake hawezi kuleta mwanga huu, CCM na ukongwe wake hakiwezi kuleta mwanga huu peke yake na wala vyama vya upinzani peke yake haviwezi kuleta mwanga huu. Mwanga mpya katika Tanzania ni mradi wa pamoja.
Ndiyo maana Watanzania wanataka kuwa na Katiba mpya. Katiba itakayoweka msingi na kuhakikisha Taifa linakuwa juu ya udini juu ya ukabila na ukanda. Katiba itakayohakikisha Taifa linaongozwa kwa misingi ya sheria.
Kama tungekuwa na Katiba imara isiyokuwa bubu kwa baadhi ya mambo ya msingi kwa nini tuwe na wasiwasi kwamba kuna maandalizi ya kuachiana na madaraka.
Katiba mpya itatusaidia kuondoa fikra potofu kwamba kuna watu waliozaliwa kutawala; Tanzania ina watu zaidi ya milioni 40; miongoni mwao hao watu wengi mmoja tu anaweza kuwa rais kwa kipindi fulani. Na mtu huyo hakuzaliwa kutawala bali anachaguliwa kufuatana na uwezo wake wa kuongoza na uzalendo wake kwa nchi yake.
Hivyo kazi kubwa iliyo mbele yetu si kulalamika Ni kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha tunakuwa na Katiba mpya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015. Nguvu na fedha za baadhi ya wenzetu zitumike kuhakikisha mchakato wa Katiba mpya unakwenda vizuri. Tutapata mwanga mpya katika taifa letu, tukipata Katiba mpya! Wa kulivusha taifa letu hapa lilipo si mwingine bali ni Katiba mpya. Wakumaliza kilio cha Watanzania si mwingine bali ni Katiba mpya!
SOURCE RAIA MWEMA: Privatus Karugendo

No comments:

Post a Comment