WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, February 26, 2013

Sheikh Khalifa aitaka Serikali kudhibiti chuki


MWENYEKITI wa Taasisi ya Kiislamu ya Imamu Bukhary, Sheikh Khalifa Khamis ameishauri  Serikali kuchukua hatua za haraka kulinusuru taifa ili lisiingie katika dimbwi la umwagaji damu kwa misingi ya chuki za kidini.

Hivi karibuni kulitokea matukio ya kuuawa kwa viongozi wa kidini mkoani Geita na visiwani Zanzibar ambapo Padre Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki aliuawa baada ya kupigwa risasi.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Sheikh Khamis alisema vitendo vya mauaji ya viongozi wa kidini, uchomaji wa nyumba za ibada na vurugu za maandamano ya kila siku ya Ijumaa vinaashiria kuwepo kwa kikundi cha watu wachache ambao wamechoka kuishi kwa amani.

“Hatuamini kama mauaji hayo yametekelezwa na waislamu kwa sababu Uislamu unahimiza amani na unapinga waziwazi vitendo vya kinyama kama hivyo,” alisema Sheikh Khamis.

Sheikh huyo alisema kuna baadhi ya vikundi ambavyo vimekuwa vikiwatumia vijana wasiojua kitu kwa masilahi yao binafsi na kwamba vikundi hivyo vinaitia fedheha na aibu jamii ya Kiislamu kwa kulitumia vibaya jina la Uislamu.

Alisema vikundi hivyo vimekuwa vikivamia baadhi ya misikiti na kuiteka huku wakiigeuza mingine kuwa vituo vya kujifunzia kareti na kufanyia mikutano na hotuba za kuwahamasisha waislamu kufanya vurugu.
Alisema hakuna mahala ambapo Uislamu unafundisha kujichukulia sheria mikononi, kupuuza au kutokuheshimu mamlaka ya dola na vyombo vya sheria.

Alisema kitendo cha baadhi ya waumini wa dini hiyo kujitumbukiza katika maandamano ya kuishinikiza Serikali, mahakama na Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP) ili kumwachia kwa dhamana Sheikh Ponda na wenzake ni kinyume na taratibu za kisheria zilizowekwa katika kumpatia mtuhumiwa dhamana.

Mwenyekiti huyo aliwaasa waislamu wote Tanzania kuendelea kuilinda amani na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kufanikiwa kuwakamata wauaji na  wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
 

Pia aliishauri Serikali iache kufumbia macho matendo maovu na ya kuvunja sheria badala yake itumie uwezo na dhamira yake ili kudumisha amani iliyoko nchini.

source Mwananchi

No comments:

Post a Comment