WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, February 24, 2013

Tumesahau kujitawala, tujifunze upya kujitawala!




WIKI iliyopita niliandika kuhimiza uchapaji kazi nchini, na kusema kwamba maendeleo haya ambayo CCM na serikali yake wanayatambia hivi sasa yana walakini, kwa sababu, kwa kiasi kikubwa, hayatokani na uchapaji kazi wetu mkubwa; bali ukopaji wetu mkubwa.
Nataka kuuendeleza kidogo mjadala huu kwa sababu kiwewe hiki cha kukopa cha Serikali ya Rais Kikwete hadi kwenye mabenki ya biashara na mashirika ya hifadhi za jamii nchini, kisipodhibitiwa kitatuletea madhara makubwa huko mbele ya safari.
Wiki iliyopita nilipendekeza tuidhibiti hali hii kwa Bunge kuweka ukomo wa ukopaji (debt ceiling); yaani kiwango fulani kikishafikiwa hakuna tena kukopa mpaka madeni yaliyopo yapunguzwe kwanza hata kwa asilimia 50. Nadhani nilieleweka.
Msingi wa hoja yangu ni kwamba maendeleo yaliyokamilika na ya kujivunia ni yale yanayotokana na uchapaji kazi wetu katika kila sekta ya uzalishaji nchini kuanzia kilimo vijijini hadi kwenye viwanda, maofisini, sekta za utalii, madini nk.
Hatma ya uchapaji kazi huo ni kukua kwa uchumi wetu, hali ambayo inatuweka katika mazingira mazuri ya kujiletea wenyewe maendeleo tunayoyahitaji – iwe ni uboreshaji miundombinu, ujenzi wa viwanda, uboreshaji huduma za afya, elimu nk.
Japo mimi si mchumi, sihitaji kuwa mchumi kuelewa kwamba kama tutachapa kazi zaidi sekta ya utalii nk na kuzalisha zaidi katika kilimo na viwandani, na hapo hapo tukatoza kodi stahiki makampuni ya madini na mengine makubwa nchini, tukakomesha ufisadi, na pia tukapunguza matumizi ya serikali na hasa ukubwa wake, tunaweza kujiletea wenyewe maendeleo tunayoyahitaji bila Serikali kulazimika kukopa sana nje au kukopa sana mabenki ya kibiashara hapa nchini na hata kwenye asasi za hifadhi ya jamii.
Lakini kwa sababu tumeacha kuchapa kazi, na kwa sababu viongozi wetu wameacha kabisa kuzunguka nchini kuhimiza uchapaji kazi, kidogo kidogo tumegeuka taifa la wavivu - taifa linalotegemea misaada na pesa za kukopa kujiletea haya tunayoambiwa na CCM kuwa ni “maendeleo makubwa”.
Kwa sababu ya utamaduni huu wa uvivu tulioukumbatia, watawala wanalikimbia tatizo kwa kutegemea mikopo ya ndani na nje ya nchi kuendesha nchi. Na ndiyo maana ndani ya kipindi cha miaka mitano tu, Serikali ya Kikwete imeongeza deni la Taifa kutoka Sh. trilioni 6 hadi Sh. trilioni 21!
Ni hoja yangu kwamba kama tunataka maendeleo ya kweli na ya kujivunia, hatuna budi kuujenga upya utamaduni wa kuchapa kazi na kuuvunjilia mbali utamaduni wa uvivu ambao umeanza kutamalaki nchini.
Binafsi, sikumbuki mara ya mwisho kumsikia Rais Kikwete au Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakitoa hotuba za kuhimiza uchapaji kazi nchini kwa namna ile walivyofanya Nyerere na Sokoine. Ni nadra kuwasikia watawala wetu wa sasa wakihimza uchapaji kazi kwa wakulima vijijini au kwa wafanyakazi viwandani au hata maofisini!
Na ma-DC wao wengi huko wilayani ni hivyo hivyo. Wanaochapa kazi ni wachache mno. Wengi hawaonekani vijijini. Kutwa nzima wako maofisini wakipanga namna ya kutumia vyeo vyao vipya kujitajirisha. Kama wakienda vijijini ni pale tu wanapopokea taarifa za migogoro inayotishia amani.
Kwa hakika, tangu Mwalimu Nyerere anga’atuke madarakani na baadaye kufariki, suala la watawala wetu kuhimiza uchapaji kazi nchini ‘limefariki’ naye! 
Sasa niambieni:Ni taifa gani duniani ambalo linaendelea kwa kasi kwa sababu ya kukopa na kukopa zaidi na si kwa sababu ya uchapaji kazi uliotukuka? Si zile nchi za Mashariki ya Mbali zinazoitwa Asian Tigers na wala si India au Brazil.
Katika uvivu wetu huu ambao Watanzania tunaogelea nao, tunazungukwa na kuishi na matatizo; lakini hatuchukui hatua yo yote ya kujaribu kuyatatua mpaka aje mgeni (Mzungu) atuonyeshe namna ya kuyatatua, hata kama tulikuwa tunajua namna ya kuyatatua.
Saratani hii ya utegemezi wa mikopo na wafadhili (dependency syndrome) – kwa fikra, mawazo na hata kwa matendo, inaanzia serikalini. Zaidi ya asilimia 40 ya bajeti yetu ni pesa za wafadhili. Sehemu kubwa ya miradi mikubwa ya maendeleo inayoendelea nchini ni  mikopo ya vyombo vya fedha vya nje na vya ndani. Zaidi ya asilimia 50 ya mipango yetu ya maendeleo inaanzia kwanza kwenye fikra za kukopa nje na ndani ya nchi, na si kwenye pesa zetu wenyewe.
Tumefika mahali sasa tumeanza kuamini kuwa kazi ya rais kuongoza nchi sasa inarahisishwa na uhodari wake wa kukopa. Anayependwa na wafadhili ndiye tunayemtaka awe rais wetu kwa sababu tunajua kuwa itakuwa rahisi kwetu kukopeshwa na mataifa makubwa atakayoyafuata kuomba mikopo au misaada!
Ilivyo sasa, tumeaminishwa kuwa anayehitajiwa si rais mchapakazi na mbunifu, bali ni yule anayewasikiliza wafadhili na anayekubaliwa na wafadhili. Ni yule ambaye ni hodari wa kutembeza bakuli la omba omba Ughaibuni kabla ya kikao cha bajeti cha bunge letu!
Hatuna maadili yetu wenyewe. Hatuna dira yetu wenyewe. Hatuna mipango yetu wenyewe ya maendeleo isiyo na mkono wa wafadhili au wa mkopeshaji iwe ni IMF, World Bank, Exim Bank ya China au NSSF ya hapa nyumbani nk!
Hali hii ya kutegemea mikopo ya nje na ya ndani ya nchi kwa karibu kila mradi mkubwa wa maendeleo nchini imeua kabisa ule moyo wa kufikiri, kubuni, kuchacharika wa viongozi wetu. Imeua ule moyo wa kujitegemea uliojengwa katika kipindi cha utawala wa Mwalimu Nyerere.
Hali hii ya utegemezi kwa kila kitu imewalemaza na kuwabwetesha si tu viongozi wetu, lakini hata na sisi wananchi wa kawaida. Kule kwetu Upare kulikuwa na utaratibu wa kazi za kujiletea maendeleo ulioitwa Msaragambo ambao Wapare tuliurithi kutoka kwa mababu zetu. Zama hizo, kila tatizo la kijiji lililowagusa wanavijiji wote lilishughulikiwa kwa pamoja kwa njia ya Msaragambo.
Kama ni kuharibika kwa barabara au mfereji mkubwa unaotumika kwa kilimo cha umwagiliaji, basi, ilipigwa mbiu na wanavijiji walijitokeza kukalafati mfereji huo kwa njia ya Msaragambo. Asiyejitokeza alipigwa faini ya pesa kidogo au vitu kama vile kuku au mbuzi!
Lakini sasa Msaragambo na matumizi ya nguvukazi ya wanavijiji kutatua matatizo yao wenyewe, hakuna tena Upareni. Kinachosubiriwa ni pesa za Halmashauri au za wafadhili au pesa za mkopo!
Zamani utegemezi wa pesa za Wazungu au za Halmashauri kwa kazi ambazo wanavijiji wenyewe walimudu kuzifanya haukuwepo hata kidogo. Leo hii, hata kujenga choo tunasubiri pesa za wafadhili au za mkopo! Hata kufukia madimbwi ya maji ambayo ni mazalio ya mbu wanaosababisha malaria, tunasubiri tufanyiwe na wengine.
Miaka kadhaa iliyopita niliwahi kutembelea kijiji kimoja cha wilaya moja ya mkoa wa Tabora ambako nilitembezwa katika bwawa la mfano la kufugia samaki lililojengwa kijijini humo kwa pesa za wafadhili (Wazungu)!
Katika hali iliyonishangaza kabisa, wenyeji wetu waliona fahari kutuonyesha bwawa la kawaida kabisa lililojengwa kutokana na fedha za wafadhili! Hii maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba tumekuwa mazezeta tusiofanya lolote kujisaidia wenyewe mpaka waje Wazungu kutufanyia hata mambo tunayomudu kuyafanya sisi wenyewe.
Sasa, ungetaraji watawala wetu wangehaha kuuzima moto huu wa dependency syndrome usisambae kwa kasi nchini kwa kutembea kote nchini kuhimiza uchapaji kazi na kuhubiri juu ya manufaa ya dhana ya kujitegemea. Je; ndivyo wanavyofanya?
Jibu langu ni hapana. Na hawawezi kufanya hivyo kwa sababu wao wenyewe ni waumini wakubwa wa maendeleo yanayotokana na fedha za mikopo, na ndiyo maana miaka mitano tu deni la Taifa limeruka kutoka Sh. trilionji 6 hadi Sh. trilioni 21!
Mtunzi maarufu wa vitabu wa Nigeria, Chinua Achebe, akizungumzia hali ya mambo ilivyo katika nchi yake na katika nchi nyingine za Afrika, alipata kunukuliwa akisema: “We have to begin to learn to rule ourselves again” ; yaani: tunapaswa kuanza kujifunza namna ya kujitawala wenyewe tena” (tafsiri ni yangu).
Naamini Achebe hakukosea kusema hivyo, na naamini pia kwamba nasi Tanzania tunapaswa kuanza kujifunza upya kujitawala; maana yaelekea baada ya Nyerere kufariki tumesahau namna ya kujitawala.
Vinginevyo tusingejivunia mno maendeleo yanayotokana na pesa za kukopa na kukopa zaidi hata kutoka katika asasi za hifadhi za jamii zinakotunzwa pesa za masikini wastaafu wetu!
Tafakari.
Source: Raia Mwema: Johnson Mbwambo

No comments:

Post a Comment