WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, February 2, 2013

Demokrasia si chaguzi na ushindi wa vyama,ni watu


DEMOKRASIA imefafanuliwa kuwa ni Serikali ya watu inayoendeshwa na kusimamiwa na watu kwa ajili ya watu wenyewe.
Lakini kwa Wanasosholojia, wao huiangalia jamii kwa mtazamo wa kiuhusiano zaidi ambapo umoja wa kijamii ni kielelezo madhubuti cha uhusiano mzuri na ustaarabu wa jamii husika. Kwa mtazamo huo, demokrasia ni uhusiano kati ya watu, jinsi wanavyochukuliana na kutatua au kumaliza tofauti zao; na pia kati ya watu na serikali.
Demokrasia ya kweli inampa kila raia mtu mzima, mwenye akili timamu, haki ya kushiriki katika utawala na katika uamuzi wa serikali yake.  Lakini kwa kuwa si rahisi kuitisha kikao chenye kushirikisha watu wote kwa shughuli hii (kama ilivyokuwa enzi za mababu wa demokrasia – Wayunani), jamii imebuni mfumo wa demokrasia ya uwakilishi (“representative“ au “elective democracy“) ambapo watu huchagua wachache miongoni mwao wanaofikiri ni wazuri sana(aristoi) kuliko wengine katika kusimamia mambo kwa niaba ya hao wengi.
Kwa jinsi hii, demokrasia ni aina fulani ya utawala unaojumuisha haki ya kuwakilishwa na haki ya kusemewa katika masuala yanayowagusa wanaowakilishwa.  Uwakilishi huo huongozwa na Katiba ya nchi ambayo ni “msahafu“ au mkataba unaotungwa na wananchi kufafanua namna serikali yao inavyopaswa kuongoza.
Kuibuka kwa vyama vya upinzani kama njia moja ya mabadiliko ya Kikatiba ni tukio muhimu la kisiasa nchini mwetu na barani Afrika, ambapo tangu enzi za uhuru mfumo wa demokrasia ya Chama kimoja ulitawala. Lengo kuu la mabadiliko haya ni “uwajibikaji“ kwa watawala ndani ya mfumo wa vyama vingi vya siasa, unaosimamia uhuru wa mawazo na fikra tofauti bila ya kugombana.
Lakini, pamoja na hilo, mabadiliko hayo hayajaondoa ukweli kwamba, demokrasia kwa raia hivi sasa imefungwa kwenye rumande ya vyama vya siasa kiasi kwamba raia amewekewa masharti yanayomnyima haki ya kuchaguliwa au kushiriki katika utawala wa nchi, isipokuwa kupitia vyama vya siasa (Katiba ya nchi – Ibara 39 (c) na 67 b ).
Lengo hapa ni kuzuia demokrasia ya uwakilishi nje ya vyama vya siasa, kana kwamba mtu hana uwezo wa kufikiri isipokuwa kwa nguvu ya vyama vya siasa; hivi kwamba utawala sasa maana yake ni vyama vya siasa. Lakini kwenye vyama vya siasa huko ndiko demokrasia inakouawa.
Baada ya demokrasia ya uwakilishi kuhodhiwa na kudhibitiwa na vyama vya siasa (kwa kupiga marufuku wagombea binafsi), kile kinachoitwa “vikao vya chama“ vimegeuka machinjio ya demokrasia kupitia vikundi vya kidikteta vyenye uwezo kamili kuzima matarajio ya watu katika uongozi.
Hii ni pamoja na dhana mpya ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kwa mawaziri wa serikali kuwajibika kwa Halmashauri Kuu (|NEC) ya CCM katika utendaji kazi wao, badala ya kuwajibika kwa Rais wa nchi, kana kwamba serikali ni ya chama kimoja!. Mawaziri wanawajibika kwa wananchi (Bunge) kupitia Katiba ya nchi, na si kwa Chama cha siasa.  Iweje Katiba ya Chama ichukue nafasi ya Katiba ya nchi?
Vyama kinzani vinaweza kuingia malumbano kwa “kujibu mapigo“, kama Mwenyekiti wa CCM Taifa, Jakaya Kikwete, alivyowaelekeza makada wa CCM hivi karibuni. Lakini isiwe “kujibu mapigo“ tu hata penye ukweli;huko ni kukwaza maendeleo, kwani “ukweli“ hauna Chama wala itikadi.
Ni Mwalimu Julius Nyerere aliyetuonya katika kitabu chake “TUJISAHIHISHE“, kwamba, “Ukweli una tabia moja nzuri juu yake; kwa wakubwa na wadogo, kwa marafiki na maadui, “UKWELI“ ni ule ule kwa wote.  Na tabia moja ya ukweli ni kwamba, ukiubeza, siku zote utaujutia.  UKWELI haupendi kubezwa wala kupuuzwa“.
Kwa misingi ya demokrasia makini, ubora wa serikali ya nchi haupimwi kwa kigezo cha kuwekwa madarakani na wengi (kwa ushindi wa kishindo), bali kwa kigezo cha uhuru na uvumilivu inaotoa kwa wachache wanaotokea kutokukubaliana nayo, na ambao vinginevyo, ni wazalendo wema tu wenye kuzingatia sheria za nchi.  Kwa hiyo, kigezo cha demokrasia makini sio ushindi wa kishindo, wala ushindi huo si leseni ya kukiuka misingi ya utawala bora na utawala wa sheria.
Tunayo mifano mingi; mmoja ni ule kwamba, Adolf Hitler wa Ujerumani, aliingia madarakani kwa ushindi wa kimbunga kwa Chama chake cha NAZI, na nchi hiyo ikiwa na Katiba nzuri kuliko zote barani Ulaya enzi hizo; lakini bado Hitler alitokea kuwa dikteta mbaya mno ulimwengu huu umepata kuona. Hii ni kwa sababu Wajerumani walibweteka na kuamini kwa makosa kwamba, demokrasia hupimwa kwa kigezo cha vyama vya siasa. Hapo, udikteta wa serikali hugeuka kuwa udikteta wa Chama, ukiwakilishwa na kikundi kidogo cha wahafidhina wa kichama.
Inachefua leo chini ya dhana ya demokrasia ya vyama vingi, kusikia Viongozi wa Chama fulani kutishia kuwafukuza kazi wakuu wa mikoa na wilaya (wanaoteuliwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi), watakaoshindwa kutii maagizo ya Chama, kana kwamba Katiba ya Chama cha siasa ni sehemu ya Katiba ya nchi. Huo ni ubabe butu kutoka kaburini, wa mzimu wa uliokuwa mfumo (mfu) wa chama kimoja. Kama wakuu hao wa Kikatiba wanakubali hilo, heri wajiondoe wakahubiri vyama, badala ya kusimamia kikatiba, maendeleo ya wananchi yasiyofungamana na itikadi za kivikundi za vyama.
Uzalendo ndio msingi pekee ambao demokrasia ya kweli, au mfumo wowote wa serikali unaweza kufanya kazi.  Uzalendo unajumuisha utii wa mtu kwa Katiba ya nchi ambayo iko juu ya vyama vya siasa.  Chama  cha siasa kinapaswa kufanya kazi ndani ya Katiba ya nchi. Vyombo vya dola si mali ya Chama cha siasa, bali ni vya wananchi wote, wanachama na wasio wanachama wa vyama. Hivyo, havipashwi kutumika kwa manufaa ya kisiasa.
Ukandamizaji ni adui wa uzalendo; Chama hakiwezi kudai hatimiliki au kuhodhi uzalendo kuliko Chama kingine. Huo utakuwa udikteta wa vikundi, kama si kulewa madaraka.  Wahenga walisema, madaraka yote hulevya; lakini madaraka makubwa zaidi hulevya zaidi na kuhatarisha demokrasia.
Kwa nchi zenye demokrasia komavu, uzalendo unaonyeshwa na vyama vyote vya siasa kwa kupeperusha bendera ya taifa katika mikutano yake, sambamba na za vyama, na kumalizia shughuli kwa wimbo wa taifa ambao hauna Chama.
Kikwazo kwa demokrasia ya kweli hapa nchini ni kule kuichukulia siasa kama njia rahisi ya kujipatia utajiri na nguvu za kiuchumi.Kwa watu hawa kuachia madaraka ni suala la kufa na kupona, hata kama ni kwa gharama ya demokrasia, kwa sababu kufanya hivyo ni sawa na kuachia utajiri. Hawa ndio wamehalalisha rushwa na sheria tata ya uchaguzi kujijengea ngome. Uchaguzi siku hizi ni fedha, bila hivyo, kwa masikini, haki ya kuchaguliwa haipo.  Rushwa au “dau” wanavyoita, maana yake ni pesa kwanza nchi baadaye; hapa ni kupata bora viongozi badala ya viongozi bora.
Chaguzi za kidemokrasia hufanya serikali iwajibike kwa watu. Sheria za uchaguzi zinapashwa kuwa huru na za haki, badala ya kuweka mazingira yanayokaribisha fujo na rushwa na kuua misingi ya uadilifu, uwazi na utawala bora.
Demokrasia itashamiri vipi kama ilivyoshamiri kwa nchi zilizoendelea, wakati watu wetu wanateseka kwa njaa, wanatembea peku kwa ufukara, ili mradi wengine wachache wamiliki magari na majumba ya kifahari, wakila na kusaza?
Ili serikali ipate uhalali wa kutawala (legitimacy), inapaswa kutekeleza mambo yafuatayo: kupanua maendeleo ya kiuchumi; kujenga umoja wa kitaifa na kuongeza uwezo wa serikali katika kukabiliana na mabadiliko ya kijamii.
Uhalali huu utayoyoma kama tutaruhusu demokrasia ife msalabani kwa jina la siasa za vyama, uhasama wa vyama, ubinafsi, kulindana na kubinafsishwa kwa serikali na kikundi kidogo chenye nguvu ya fedha.
Uhalali huu utapotea pia kama tutaruhusu fedha inunue siasa na siasa inunue fedha, kufanya uongozi na uchumi kuwa mikononi mwa kikundi cha matajiri. Kumetokea nini leo, kwamba nafasi za chama tawala, ni jambo la kufa na kupona kwa wakuu wa wilaya na mikoa, wafanyabiashara, mawaziri na vigogo wengine?  Ni uchu wa madaraka ya kisiasa. Lengo ni kununua utajiri na si kutumikia; maadili na malengo ya taifa yanapotea haraka.
Kukosekana tabia ya kukosoa na kukosolewa huzaa kiburi,  maringo, majivuno, kunata, uongozi kwa mkono wa chuma na uhaba wa uvumilivu; na hapo ndipo, ngoma hulia sana ambapo mwisho wake ni kupasuka, kwani wale wanaojiona hawawezi kukosolewa sasa hujihesabu kama miungu watu; maisha hugeuka ya kuabudu mashujaa wa bandia ambao hupenda kuitwa “Waheshimiwa“ badala ya kuitwa “Ndugu“; wenye kutaka kutumikiwa badala ya kutumikia. Ni kuthibitisha ukweli wa Karl Marx kwamba, “Chama si chochote bali ni taasisi ya kitabaka kwa lengo la kunufaisha kikundi cha kitabaka kiuchumi“.
Katika “TUJISAHIHISHE“, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere anabainisha kuwa, tunapojadili masuala yanayoigusa jamii nzima, ni vyema kujifunza kusikiliza hoja zinazotolewa na wenzetu na kuzijibu kwa kuzikubali au kuzikataa, bila kujali zimeletwa na marafiki au watu wasio marafiki zetu. Inapokuwa hivyo hapana sababu ya  “kujibu mapigo“ penye ukweli.
Kuna sababu gani, kwa mfano, kukana au kukataa mchana kweupe, tuhuma za ufisadi nchini zilizo wazi, kwa sababu tu zimetolewa na wapinzani? Tujue kwamba, uzalendo hauna Chama wala itikadi; lazima tukubali yote yaliyo ya msingi kwa taifa, bila kujali yanatoka kambi gani. Wanasiasa wasitangulize maslahi yao binafsi na ya vyama vyao;  muhimu ni maslahi ya taifa kwanza na watu wake, vyama vya siasa baadaye. Tunaongozwa na Katiba ya nchi ambayo iko juu ya Katiba za vyama na juu ya sheria zingine zote za nchi.
Wanasiasa, tofauti na wanasosholojia na waandishi wa habari, ni watu waliopungukiwa milango ya hisia na fahamu  kuweza kunusa, kusikia au  kuonja, kujua kinachoendelea katika jamii; hawawezi kusoma alama za nyakati na maandishi ukutani. Kuna misemo miwili ya Kihaya kuthibitisha hatima yao kwamba:  “ugonjwa unaomuua Mbwa haraka ni ule unaoziba pua,”  kwa maana atakosa hisia na kula sumu na kufa. Au kwamba, “Kumbikumbi akikaribia kufa, huota mbawa na kuruka”. Lakini pamoja na hayo, je, haikusemwa kwamba “ngoma ikilia sana hupasuka”?  Ni lini wanasiasa watajenga utamaduni wa kujikosoa na kukubali kukosolewa kwa uvumilivu ili wasishikwe ugonjwa wa kuziba pua?
Kwa sasa tabaka hili haliwezi kuendelea kuishi au kuokolewa kwa njia ya utawala wa serikali yenye kutenda haki; njia pekee kwake sasa liweze kuishi, ni kujihami kwa kuhubiri injili ya ufisadi ili chama na serikali viache maadili ya kitaifa na kuabudu kwenye madhabahu ya ufisadi, kama utamaduni mpya!
Source: Raia Mwema: Joseph Mihangwa

No comments:

Post a Comment