WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, February 18, 2013

[update] Watatu wanahojiwa Zanzibar: Padre/Father Mushi auawa kwa risasi

Picture




Padre Evaristus Mushi

Picture
Gari alimokuwa Padre Mushi (Shukurani ya picha: Francis Dande)
Picture

Gari liliacha uelekeo na kugonga nyumba baada ya Padre Mushi kupigwa risasi (Shukurani ya picha: Francis Dande)
Picture

(Picha na Othman Maulid Othman-Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar)
Picture

(Picha na Othman Maulid Othman-Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar)
Picture

Waziri Dkt Nchimbi (wa pili kushoto) akiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mohamed Aboud na maafisa wengine walipotembelea eneo la tukio leo. (Shukurani ya picha: Francis Dande)

UPDATE/TAARIFA MPYA (saa 11 jioni Februari 17, 2013)  Salamu za rambirambi za Rais Jakaya Kikwete

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya kuuawa kwa Padri Evarist Mushi wa Parokia ya Minara Miwili ya Kanisa Katoliki  mjini Zanzibar, mauaji yaliyotokea Zanzibar.

Rais Kikwete anawapa pole nyingi na rambirambi za dhati ya moyo wangu Baba Askofu Augustino Shayo wa Jimbo Katoliki, Zanzibar, maaskofu wote nchini na waumini wote wa Parokia ya Minara Miwili kwa msiba huo mkubwa uliowakuta.

Rais kikwete amemwambia Baba Askofu Shayo. ”Napenda kuwahakikishia kuwa tupo pamoja katika kuomboleza kifo cha Mpendwa Marehemu Padri Evarist Mushin a kuwa msiba huu ni wa kwetu sote.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Nimeligiza Jeshi la Polisi nchini kukusanya nguvu zake zote na maarifa yake yote kuhakikisha kuwa uchunguzi wa kina na wa haraka sana unafanyika ili kubaini mhusika ama wahusika na kuwakamata ili kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.”

“Aidha, nimewaagiza Jeshi la Polisi washirikiane na vyombo vingine vya Usalama nchini na mashirika ya upepelezi ya nchi rafiki katika kufanya uchunguzi wa mauaji haya.”

Amesisitiza Rais Kikwete: “Nataka ukweli wake ujulikane ili kama kuna jambo lolote zaidi liweze kushughulikiwa na kukata mzizi wa fitina.”

Vile vile, Rais Kikwete amewataka waumini wa Kanisa katoliki na wananchi wote kuwa watulivu wakati Serikali inashughulikia suala hili na kuwa hakuna mtu wala watu ama kikundi cha watu kitachoruhusiwa kuvuruga amani ya nchi yetu.
UPDATE/TARIFA MPYA (saa 8 mchana Februari 17, 2013) Taarifa ya Polisi:

Watu watatu wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za mauaji ya Padre Mushi. Taarifa ya polisi imepachikwa hapo. (shukurani kwa Francis Dande).

UPDATE/TAARIFA MPYA (saa 7 mchana Februari 17, 2013) Taarifa ya habari Radio One Stereo:

Taarifa ya habari ya Radio One Stereo iliyosomwa saa 7 mchana imeripoti kuwa Padre Mushi aliuawa na watu walipolisimamisha gari la Padre huyo alipokuwa akielekea katika kanisa la Mtakatifu Theresia lililoko eneo la Mtoni, na alipopunguza mwendo ili awasikilize, ndipo alipopigwa risasi kichwani na kusababisha gari alilokuwamo kukosa uelekeo na kuigonga nyumba iliyokuwa jirani. Watu walioshuhudia tukio hilo walimchukua Padre Mushi ili kumwahisha hospitalini katika jitihada za kuokoa uhai wake, lakini alifariki dunia. Waliomwua Padre Mushi bado hawajakamatwa.
    
Picture                                                                                                   
Akina mama wakilia kwa uchungu kuomboleza kifo cha ghafla cha kupigwa risasi Padre Evaristus Mushi kilichotokea leo asubuhi muda mfupi kabla ya kuanza Misa ya Jumapili kwenye kanisa la Kigango cha Mtoni, Zanzibar. (Picha na Martin Kabemba via Lukwangule blog)
Taarifa kutoka Zanzibar zikiripotiwa na mwanahabari Donisia Thomas wakati kipindi cha Patapata cha WAPO radio FM kinaendelea, zinasema kuwa Padre Evaristus Mushi wa Kanisa la Parokia ya  St. Joseph, Shangani, Zanzibar amepigwa risasi katika Kanisa la Minara Miwili, Zanzibar majira ya saa moja asubuhi -na watu wasiofahamika- na kufariki dunia.

Taarifa za kufariki kwake zimethibitishwa na madaktari kutoka hospitalini alikopelekewa katika harakati za kuuokoa uhai wake.

Padre Mushi aliuawa katika eneo hilo lililo karibu na Beit-EL-Ras akiwa kwenye gari lake tayari kuingia Kanisani kwa ajili ya kuendesha misa ya kawaida ya Jumapili katika Kanisa la Mtoni, mjini la St. Joseph (Minara Miwili). Inaelezwa kuwa watu wasiofahamika walimfyatulia risasi Padre Mushi sehemu ya kichwani na hivyo kumsababisha majeraha na hivyo kuvuja damu nyingi.

Mwanahabari anasema tukio hilo limezua taharuki kubwa miongoni mwa waumini ambao wamekataa kuahirisha ibada iliyokuwa iendeshwe na Padre huyo na kusema ikiwa kusudio ni kuwaangamiza Wakristo wote, basi na waangamizi wafike Kanisani wawaangamize wakiwa pamoja.

Jeshi la Polisi limeshafika katika eneo la tukio na kuanza uchunguzi.

Wakizungumza kuhusu hilo,  raia wamesema hawana imani na Polisi wala Madaktari na hawatarajii jipya zaidi ya ripoti kuwa suala hili ni la uhalifu kwa kuwa tukio kama hili liliwahi kutokea mwishoni mwa mwaka jana kwa Padre Ambrose kupigwa risasi na taarifa zilisema lilikuwa ni tukio la kihalifu na kwamba risasi hazikutumika jambo ambalo halikuwa kweli kwani Padre Ambrose alikutikana na risasi alipohamishiwa katika hospitali ya Taifa, Muhimbili.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali fuatilia vyombo mbalimbali vya habari.
Picture

Aliyeketi katikati ni Padre Evaristus Mushi (sasa marehemu) [Shukurani ya picha: Francis Dande]

No comments:

Post a Comment