WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, February 15, 2013

SASA UDINI UMEPATA KITI CHA ENZI


UDINI umekuwapo Tanzania kwa muda mrefu sana. Ukisoma maandishi ya mwanaharakati wa Kiislamu Mohammed Said anasimulia kuwa tangu mwaka 1953 kulikuwapo na makundi ya wazee wa Kiislamu wa Jijini Dar es Saalam ambao walikuwa wanaeneza chuki za kidini dhidi ya Julius Nyerere na Ukatoliki wake.
Wazee hawa walijaribu mara tatu kumvuruga Nyerere na utawala wake lakini walishindwa mbele ya kundi la wazee wengine wa Kiislamu ambao kwao utaifa ulikuwa juu mno na umoja wa nchi ulikuwa msingi zaidi.
Hata hivyo, wazee wale wale ambao walishindwa mara tatu bado walijaribu kuvuruga utawala wa Taifa changa na matokeo yake utawala wa Nyerere ukachukua hatua kali mapema miaka ya sitini na kuwatimua baadhi yao kutoka TANU. Baadhi yao waliendelea na kisirani dhidi ya Nyerere na Ukatoliki wake na baadhi ya watoto na wajukuu wao wanaendelea na hilo leo hii.
Lakini kulikuwa na hisia ya udini na ukabila vile vile ambapo baadhi ya watu waliona kuwa Wakristu wanapendelewa na hasa makabila ya Wanyakyusa, Wachagga na Wahaya.
Hii ilikuwa pia miaka ya sitini. Na manung’uniko hayo yalikuwa makali sana kiasi kwamba Nyerere hakuweza kuyapuuza. Aliunda Tume maarufu ya Chifu Mang’enya kwenda kuyapitia madai yaliyokuwa yanatolewa.
Nyerere alielewa hatari ya kulea hisia za udini na ukabila. Mojawapo ya maamuzi ya kupambana nayo ilikuwa ni pamoja na kutaifisha shule za mashirika ya kidini (nyingi zikiwa ni za Kikristu) na wakati huo huo kuweka uangalizi sana wa shule za misingi ya kidini. Katika hili hakuwa na huruma. Alivunja Baraza la Machifu wa jadi na kuzuia kuendelea kwa EAMWS.
Na kwa muda mrefu harakati hizi za kupambana na udini zilianza kuzaa matunda na kuanza kupongeza tofauti ambayo ilirithiwa kutoka wakati wa ukoloni kati ya Wakristu na Waislamu.
Kulikuwapo na tatizo la kweli ambalo Baba wa Taifa alilipa uzito unaostahili na kushughulikia. Na kwa kiasi kikubwa alifanikiwa sana kiasi kwamba Wakristu na Waislamu hasa kuelekea miaka ya sabini na themanini walikuwa kitu kimoja sana huku wakiheshimu tofauti zao.
Wakati ule Mkristu mtaani akitaka kuchinja kuku kwa makusudi tu anatafuta kijana wa Kiislamu kuja kuchinja ili asije akamkwaza mtu; hakuhitaji waziri wa serikali aje kumwambia achinje vipi kuku au mbuzi wake.
Waislamu nao waliweza kufanya mambo yao ya ibada bila ndugu zao Wakristu kuhisi wameingiliwa uhuru wao. Tulijifunza kuishi kwa pamoja katika jamii iliyo na tofauti tofauti nyingi (pluralistic society).
Hii ikaendana na uhuru wa watu kubadili dini na hata kuoleana. Masuala haya yalikuwa ya binafsi sana na hayakusumbua watu sana wakati ule. Ukimkuta Mkristu kaamua kusilimu na anaitwa Abdallah watu waliheshimu uamuzi wake huo na aliishi maisha yake katika dini mpya. Ilikuwa kweli pia kwa Waislamu walioamua kuokoka au kuingia katika Ukristu.
Kwa miaka nenda rudi Watanzania walijifunza kuishi kwa pamoja, wakiheshimu tofauti zao na kujali hisia za kiimani za wengine. Watu hawakutaka kusema maneno mabaya dhidi ya dini nyingine kwani walijua kuwa kufanya hivyo pia ni sawa na mtu kushambulia nyumba yake mwenyewe.
Kwani wapo wengi ambao kama wao wenyewe hawakuwa na ndugu wa dini nyingine, wengi walijikuta wanalazimika kuwa na marafiki wa dini nyingine – iwe JKT, shuleni au hata kazini.
Haikuwa ajabu kumkuta Joyce akiwa na rafiki yake kipenzi Rehema au kijana Allen akiwa na rafiki yake Rama. Siku ya Jumapili mtu alienda kanisani na Ijumaa mwenzie alienda msikitini na watu walikutana baadaya ya ibada na kuendelea na maisha kama kawaida.
Kwa kiasi kikubwa hali hii bado inaendelea. Lakini sasa hivi kuna doa limewekwa ambalo limetokea tu wakati huu wa utawala wa sasa. Tunashuhudia mfarakano wa kidini na sasa tumefika mahali tunaanza kugawana mabucha ya nyama.
Tusipoangalia tutajikuta tunaamua kugawana na Bunge (upande mmoja wakae Waislamu na upande mwingine wakae Wakristu) na labda hivyo hiyo kwenye baraza la mawaziri.
Doa hili la udini ambalo limepandikizwa kama mbegu na sasa limekua linahusiana moja kwa moja na utawala wa sasa kuachilia hali hii iendelee huku wenyewe ukiwa ni mnufaika wa udini huo.
Ni matokeo ya kampeni chafu ya udini wakati wa Uchaguzi Mkuu dhidi ya Dk. Wilbroad Slaa na kwa bahati mbaya mgombea wa CCM, wakati ule, Jakaya Kikwete alikaa kimya, na sasa kama kiongozi wa nchi bado amekaa kimya. Sasa nyoka aliyemfuga amerudi kumuuma!
Utawala wake umevumilia lugha kali ya kidini dhidi ya Ukristu na Wakristu na chuki hii imepandwa kwenye masafa ya umma ya habari huku mawaziri wake wakiwa kimya.
Tumeshuhudia watu wakitumia udini kupotosha historia ya Tanganyika huku wakieneza propaganda ya udini wakiisifia kama kuweka historia sahihi ya ushiriki wa wazee ‘wao’.
Kumbe wanafanya hivyo huku wakirusha madongo mazito yenye sumu kali ya udini dhidi ya Wakristu na Ukristu. Kwa hawa, ndugu zao ni Waislamu na si Wakristu na hivyo baya likiwakuta Wakristu wao halitowasumbua. Na wapo wengi wanafanya hivyo kwa sababu wanajua Rais ni Mwislamu, Mkuu wa Usalama wa Taifa ni Mwislamu na Mkuu wa Jeshi la Polisi Mwislamu.
Tumeshuhudia haya pale Mbagala na mwitikio wa serikali – ati wote wanajionesha kushangaa tumefikaje. Yaani, mchana kweupe wanaona watu wamebeba mbegu ya udini, wanaimwagilia maji na kuilinda na sasa imeota watawala wetu wanashangaa. Na tulipofika sasa udini uko pande zote.
Tumeona ile hisia ya kujali na kuheshimu dini ya Uislamu inazidi kupungua na wapo Wakristu ambao nao wanakuja hivyo hivyo na udini.
Wengine nao wanaanza kuangalia mtu wa kumwajiri ni nani; wakiona jina la Muislamu wanakwepa. Wengine (na ninafahamu baadhi yao) wakisikia mtoto wao sijui ana rafiki wa kiume wa Muislamu basi ni ugomvi. Tumefika pabaya.
Lakini tumefika pabaya hapa kwa sababu tumefikiwa na utawala ambao umesimama na kujikita katika kutumia udini kupata nafasi yake. Wanaogopa kuwaudhi “wenzao” na matokeo yake taifa zima linalipa gaharama ya kushindwa kwao. Njia ya kutoka ipi na wanaijua lakini hawatoichagua kwani ni hilo linawahakikishia kurudi tena madarakani.
Ndugu zangu, udini huu si makosa ya Kikwete tu bali ni makosa ya viongozi wetu kukosa hekima; kucheka na nyani sasa wanavuna mabua!
Nyerere hakucheka na wadini na udini; aliwatimua. Hakujali kama alikuwa shehe, maalim au padri! Nyerere alielewa tishio kubwa la udini lilivyo na hakucheza nalo – leo yeye anaitwa mdini!
Utawala uliosimikwa kwa udini utaanguka kwa udini; damu iliyomwagika Geita haitokoma. Itatokea tena na tena hadi tujirudi na kutambua tumepotoka.
Nyerere alisema kweli – ukweli haupendi kupuuzwa. Kwamba udini na ukabila ni dhambi mbaya sana za ubaguzi kwa hakika itarudi tena.
Mnafikiri itaishia kwenye mabucha; kwani iliishia kwenye kuchoma makanisa? Mnafikiri itaisha hivi hivi kwa kuombea? Au itaisha kwa kutoa hotuba za “sisi ni Taifa moja”. Mbona yangeisha.
Yataisha vipi kama udini umepata kiti cha enzi? Na itakuwaje kama kiti cha enzi hicho tulikibeba sisi wenyewe?

source: Raia Mwema: Lula wa Ndali Mwananzela

No comments:

Post a Comment