WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, February 13, 2013

Pigo jipya kwa Sitta, Membe, Lowassa




 
·          
Rafu za mtandao zawakutanisha Salim, Mangula
KUUNDWA kwa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ni pigo jipya kwa watu wanaotajwa kuweza kuwania nafasi ya kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Raia Mwema, limebaini.
Taarifa zinasema fursa ya kujieleza mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ilikuwa ni kete nyingine kwa wagombea hao watarajiwa, Samuel Sitta, Edward Lowassa na Benard Membe kuomba kura za wajumbe ili wachaguliwe kuwa wajumbe wa Kamati Kuu kama majina yao yangepenedezwa na Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete.
Inaelezwa kuwa ingefahamika mgombea yupi mtarajiwa kati yao ana ushawishi wa kura za NEC yenye wajumbe ambao ndio hao hao watakaopitisha majina ya wagombea urais kwenda Mkutano Mkuu 2015.
Hadi sasa, kati ya wanaotajwa ni Membe pekee ndiye aliyejipima ubavu katika vikao vya kitaifa vya CCM katika hekaheka ya kuomba kura, akiwa amejitosa kuwania ujumbe wa NEC kwa kupigiwa kura na Mkutano Mkuu ambao ndio hupitisha jina la mgombea urais.
Wenzake ambao nao wanatajwa kuweza kuwania urais 2015, Lowassa aligombea u-NEC katika Wilaya ya Monduli anakotoka, wakati Sitta aligombea u-NEC kupitia nafasi za wabunge wa CCM.
Wengine wanaotajwa katika kinyang’anyiro cha urais ambao nao hawakupata nafasi ya kupima ubavu wao wa kuomba kura za NEC, ni pamoja na Dk. John Magufuli na Dk. Harrison Mwakyembe.
Kwa hiyo, kwa mujibu wa vyanzo kadhaa vya habari, majina ya wagombea hao watarajiwa kutopendekezwa na Kikwete ni pigo moja lakini pigo jingine ni kwao kushindwa kupima nguvu zao ndani ya NEC mpya.
Pigo jingine zaidi kwao linatajwa kuwa ni kushindwa kuwamo katika Kamati Kuu (CC), kikao kinachotajwa kutengeneza mizengwe kuhusu mbinu za kumpata mgombea, kama wangeingia wangeweza kukuza mikakati yao ya kisiasa kwa kutumia mwenendo wa vikao hivyo vya CC.
Hata hivyo, kuwa mjumbe wa Kamati Kuu si tiketi ya moja kwa moja ya kujihakikishia ushindi. Mifano ya kuthibitisha hilo pamoja na yaliyojitokeza kwa Benjamin Mkapa mwaka 1995. Wakati huo hakuwa mjumbe wa Kamati Kuu, lakini kwa kutegemea zaidi nguvu za ushawishi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alishinda.
Wapo pia waliowahi kuwa wajumbe wa Kamati Kuu na wakaanguka kwenye mbio za urais ndani ya CCM, hao ni pamoja na Frederick Sumaye, akiwa Waziri Mkuu, 2005 Cleopa David Msuya (1995) na John Malecela (2005), akiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM.
Kamati Kuu mpya ya CCM
Kurejea kwa Dk. Salim Ahmed Salim kwenye siasa za juu za CCM, mapema wiki hii mjini Dodoma, ambaye katika kinyang’anyiro cha urais 2005 alichuana na Jakaya Kikwete na kupigwa mzengwe kunatafsiriwa kuwa ni ishara nyingine ya chama hicho kupuuza siasa za kimtandao zilizokuwa zikiendeshwa kwa takriban miaka zaidi ya 10 sasa.
Hata hivyo, inaelezwa kwamba mwendelezo wa siasa hizo za kimtandao kwa sehemu kubwa, pamoja na udhaifu wa serikali, vimetoa nguvu kwa siasa za upinzani kukomaa nchini kwa sababu CCM ilijikuta ikitumia muda mwingi kukabili mashambulizi ya ndani, hadi kuundwa kwa Kamati Maalumu kukabili mpasuko.
Kamati hiyo maalumu iliongozwa na rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi na wajumbe Pius Msekwa na Katibu Mkuu wa sasa wa CCM, Abdulrahaman Kinana. Wakati huo, kambi mbili kuu bungeni zilikuwa zikitafunana kwa kujitambulisha kwa majina ya kambi ya mafisadi na kambi ya wapinga ufisadi.
Rafu zawarejesha wakongwe
Ukiondoa wajumbe wengine wapya wa Kamati Kuu hiyo mpya, bado jina la Dk. Salim linaendeleza mjadala kwa kuhusishwa na siasa za maji taka alizowahi kufanyiwa mwaka 2005 na kundi linalotajwa kuwa la mtandao.
Wajumbe hao katika orodha hiyo inayomjumuisha Dk. Salim ni pamoja na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Uratibu), William Lukuvi; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano), Stephen Wassira, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Wengine ni Mbunge wa Viti Maalumu, Pindi Chana; Meya wa Manispaa ya Ilala (Dar es Salaam) Jerry Silaa; Meya wa Manispaa ya Dodoma, Adam Kimbisa; Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi; mwanasiasa mpya, Profesa Makame Mbarawa; Dk. Maua Daftari, Khadija Aboud pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan.
Ni kwa kuichambua orodha hiyo mpya ya wajumbe wa Kamati Kuu iliyopitishwa Dodoma mwanzoni mwa wiki hii, inabainika ya kwamba, kurejea kwa Dk. Salim na kukubaliwa kwake na kura za waNEC kuwa Kamati Kuu ni mjadala mpana zaidi.
Katika vikao vya Kamati Kuu Salim atakutana na majeruhi mwenzake wa siasa za kimtandao, Philip Mangula, ambaye kwa wakati huo, mwaka 2005, alipoteza ukatibu mkuu wa CCM ghafla, akijikuta hana gari ya kurejea mjini Dodoma kutokea ukumbi wa mkutano wa CCM-Chimwaga, baada ya gari la hadhi ya Katibu Mkuu kuchukuliwa. Makamba ndiye aliyerithi mikoba yake.
Kwa sasa, taarifa zinaeleza uzito wa Kamati Kuu na hadhi yake inapewa nguvu mbele ya umma kutokana na kuwapo kwa Dk. Salim, Mangula, Kinana na katika mtazamo wa kimataifa, Profesa Tibaijuka na Dk. Asha Rose Migiro, huku nafasi ya vijana ikibebwa na Nape Nnauye, Jerry Silaa na Mwigulu Nchemba.
Hata hivyo, katika Kamati Kuu hiyo wapo wajumbe ambao wanatiliwa shaka kuendeleza siasa za makundi na wengine wakiwa na harufu ya rushwa, wakihusishwa katika vitendo vya rushwa katika changuzi za chama hicho zilizopita.
Source: Raia Mwema

No comments:

Post a Comment