WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, April 10, 2014

Wasomi: Tunataka serikali moja

 
Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samia Suluhu Hassan (kushoto), akipokea nakala ya kijarida cha wanataaluma 100 cha kutafuta Katiba Bora Tanzania kutoka kwa Mwandishi wake, Profesa Teddy Malyamkono, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya EUSARP kwenye ofisi za Bunge mjini Dodoma jana.(Pichan na Khalfan Said)
Wanataaluma wa Taasisi ya Utafiti ya Vyuo Vikuu vya Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAURP) wamekabidhi kitabu kinachoitwa Katiba Bora Tanzania kwa ajili ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba huku wakipendekeza muundo wa serikali moja.
Kitabu hicho kilikabidhiwa jana mjini hapa kwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Hassan Suluhu na wanataaluma hao, Profesa Teddy Maliyamkono, Profesa Nehemiah Ossoro na Profesa Bonnaventure Rutinwa.

 Akizungumza kabla ya kukabidhi kitabu hicho, Profesa Maliyamkono ambaye ni Mkurugenzi wa ESAURP, alisema miaka 50 inatosha kutoka katika serikali mbili kwenda moja na siyo serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Alisema ingawa uchaguzi wa Tume hiyo ni kuwa na nchi yenye serikali tatu, lakini kuna matatizo kadhaa makubwa katika muundo huo.

Alisema ni muhimu kwa Tanzania kuwa na muundo wa serikali ambao utakidhi mahitaji yake,“Haya ni pamoja na tatizo kubwa la kukosekana kwa ulinganifu kati ya nchi hizi mbili na mchanganyo wa sekta ya uchumi Zanzibar unaosababisha matatizo ya kifedha wa serikali ya kitaifa na mchango wake wa kifedha kwa serikali ya Muungano,”

alisema Profesa Maliyamkono Akizungumzia muundo wa serikali tatu, Profesa Osoro ambaye ni mchumi aliybobea katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema katika utafiti wao, walibaini kuwa kupungua kwa gharama ya kuendesha serikali ya shirikisho inayopendekezwa itakuwa asilimia zaidi ya 97 ya gharama za  kuendesha muungano wenye serikali mbili.

Alisema punguzo hilo dogo katika gharama linatokana na kupunguza mambo ya Muungano kutoka 22 hadi saba , haiashirii kupungua kwa gharama za kuendesha serikali ya shirikisho inayopendekezwa kwa theluthi mbili.

 Alisema mambo saba ya Muungano yaliyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kubaki katika serikali ya Shirikisho ni yale ambayo yana matumizi makubwa, kama vile ulinzi na usalama na mambo ya nje.

“Hii inatokana na ukweli kwamba mambo haya saba ya Muungano ni vipengele vikubwa vya matumizi…utafiti huu unaonyesha kwamba tofauti katika gharama za kuendesha ama Muungano wa serikali mbili au tatu si kubwa sana,” alisema.

Hata hivyo, alisema katika Muungano wa serikali tatu, nchi mbili huru (Tanganyika na Zanzibar) kila moja itahitaji fedha za ziada kwa ajili ya matumizi yake.

Kuhusu gharama kuendesha mfumo wa Shirikisho uliopendekezwa, alisema Tanzania ni nchi kubwa na tajiri kwa madini na rasilimali nyingine za asili tofauti na Zanzibar ambayo ni nchi ndogo na ina idadi ya watu wasiopungua milioni na rasilimali zake ni chache.

“Kwa ufupi, Zanzibar mbali na utalii ni dhaifu sana kiuchumi…kwa Tanzania kuwa tajiri katika maliasili na utalii na idadi ya watu, inaweza kubeba gharama za kuendesha Muungano uliopo,” alisema

Alisema hilo linaweza kuwa ni tatizo kwa sababu Zanzibar inaweza kushindwa kuwasilisha mchango wake kama ilivyokubaliwa na pande zote mbili na Tanzania Bara pia itakataa kutoa msaada wowote wa ziada.

“Jambo hili linaweza kuwa na chanzo cha migogoro na misuguano kati ya nchi hizi mbili ambayo inaweza kuwa migumu kutatuliwa kisiasa…inaweza hata kusababisha kuvunjika kwa Muungano,” alisema

Alisema kwa kiasi fulani gharama za kuendesha mfumo wa serikali tatu inaweza kuwa kubwa ikilinganishwa na gharama yote ya kuendesha Muungano uliopo.

Naye Profesa Rutinwa, ambaye ni Mkuu wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kwamba wanaotaka serikali tatu msukumo wao unatokana na mabadiliko ya katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 ambayo imetamka kwamba Zanzibar ni nchi.

Hata hivyo, alisema hoja hizo hazina nguvu kwa sababu siyo mara ya kwanza  hoja kama hiyo kutolewa kwa kuwa kabla ya hapo, Katiba hiyo ilikuwa ikionyesha kwamba Zanzibar ni nchi.

Alitoa mfano kwamba, Katiba ya 2003 ina vifungu viwili cha 9 na 22 ambavyo vinaonyesha kwamba vinataja Zanzibar ni nchi na ni Taifa.

Alisema kwamba kwa upande wao suala la muundo wa serikali wanaliacha kwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba ili waweze kuliamua.

Akizungumza baada ya kupokea nakala hizo, Suluhu aliwashukuru wanataaluma hao kwa kujitolea kuandika kitabu hicho ambacho kitakuwa msaada mkubwa kwa wajumbe wa bunge hilo kwa ajili ya kutengeneza katiba yenye maslahi kwa Watanzania wote.

Alisema kwa sababu kanuni zinaruhusu kuwaita wataalamu kwa ajili ya kutoa ushauri, bunge hilo halitasita kuwaita wakati wowote watakapowahitaji.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment