WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, April 10, 2014

Katiba Mpya: Nimeitafakari Sana Njia Ya Kikwete...

1_ecfa4.jpg

Katiba Mpya: Nimeitafakari Sana Njia Ya Kikwete...
Ndugu zangu,
Naziona ishara za kuendelea kwa mvumo mbaya wa upepo wa kisiasa na hususan inapohusu hoja ya Muungano na muundo wa Serikali.
Mjadala unaoendelea sasa ni kama vile umefunikwa kwa chandarua kisicho na kinga ya wadudu wenye madhara kama mbu.
Tunakoelekea si kuzuri. Msimamo wangu uko wazi, kuwa tunahitaji muundo wa Serikali Tatu ili tuimarishe Muungano wetu. Kwamba tunahitaji uwepo wa Tanganyika kama nchi.
Lakini, nahofia katika tofauti hizi za mitazamo, kuna wenye kuamini katika Serikali Tatu lakini bila kuwa na nia njema kwa nchi. Na kuna wenye kuamini hivyo wakiwa na dhamira njema pia. Hivyo hivyo kwa wenye kuamini katika Serikali Mbili.
Hivyo, nimeipitia mara kadhaa hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa alipokuwa akifungua Bunge Maalum la Katiba. Nimejitahidi kuitafuta mantiki kwa alichokizungumza Rais wa Nchi. Naamini Jakaya Kikwete aliongea kile alichokiamini moyoni mwake. Kikwete alionyesha hofu juu ya Serikali Tatu ingawa aliweka wazi kuwa maamuzi ya mwisho ni ya Wabunge wenyewe. Ni haki ya Kikwete kama mwanadamu kuelezea hisia zake.
Lakini , Jakaya Kikwete si kama Watanzania wengine. Ni Rais wa Nchi. Nikifikiri leo, naamini ilikuwa sahihi kwa Kikwete kukisema alichokisema, hata kama hakifanani na misimamo kama ya kwangu.
Maana, nikiwasikiliza ndugu zetu wa Zanzibar , hasa wenye kuupinga Muungano katika hali iliyopo, na jinsi wanavyojadili, kwa kweli natishikia pia. Na hakika, kwa kuufuatilia mvumo wa upepo wa kisiasa unaoendelea sasa, Jakaya Kikwete alitusaidia kuyaweka wazi mawazo yake binafsi. Maana, ingawa Serikali Tatu na Tanganyika inahitajika, lakini, huu si wakati wake. Ni jambo la kusubiri lije tutakapokuwa tayari kama watu tulioungana; Visiwani na Bara. Na tuanze sasa kufanya jitihada za kuyatafuta maridhiano juu ya kwa nini haya ya kubadilli mfumo wa Serikali kwenda Serikali Tatu wakati wake haujafika.
Maana, kuendelea kujadili Serikali Tatu sasa ni kuzidi kuipeleka nchi yetu tunayoipenda kwenye mgawanyiko na mpasuko mkubwa. Ni busara nionavyo, kuwa Wabunge wetu kule Dodoma watambue kuwa rasimu ya Jaji Warioba, ukiacha muundo wa Muungano na mfumo wa Serikali , ina mengi sana ya muhimu ili kututoa hapa tulipo na kuwasaidia wananchi.
Waitafute busara ya kulisubirisha hili la Muuundo wa Muungano unaopendekezwa na Rasimu ya Warioba na hata muundo wa Serikali. Tubaki na Serikali Mbili na tuboreshe kinachoweza kuboreshwa.
Maana, si kila unachokigawa maana yake kuna kinachobaki. Kugawa pia kuna maana ya kumaliza pia.
Na mengine tuyafanyao katika wakati usio sahihi huzaa kutokuaminiana.
Na kwa mwanadamu pale mtaji wa imani unapomalizika, kinachobakia ni kumaliziana.
Usimwone nyani ana makovu ukadhani ni simba aliyemjeruhi. Nyani huishi kwa kumwogopa zaidi nyani mwenziwe.
Kugawanyika kwa shari ni kutawanya mitaji ya kuaminiana.
Na kitachobaki ni kuumizana, kwa kugombani kiduchu chunguni kilichogandiana...
Ni wakati sasa wa kutanguliza busara na hekima zitakazotunusuru na mpasuko mkubwa zaidi wa kijamii.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

Maggid,
Iringa.


No comments:

Post a Comment