WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, April 18, 2014

Kikwete: Ni utovu wa nidhamu kuwatukana waasisi wa Taifa

Rais Jakaya Kikwete


Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amesema ni utovu wa nidhamu na ukosefu wa adabu unaoonyeshwa na baadhi ya Watanzania kuwatukana, kuwadhihaki na kuwakejeli waanzilishi wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa kwenye mahojiano maalumu na wahariri wa baadhi ya vyombo vya habari (wa Mwananchi hawakuwapo) ya kuadhimisha miaka 50 ya Muungano.

Kauli hiyo ilikuwa ni jibu la moja ya maswali alilokuwa ameulizwa na wahariri hao kuhusu matusi, kejeli na dhihaka ambazo zimekuwa zinaonyeshwa na wajumbe wachache wa Bunge Maalumu la Katiba juu ya waasisi hao wa Tanzania na wabunifu wakuu wa Muungano wa Tanzania.

“Ni kukosa adabu na ni utovu mkubwa wa nidhamu kwa Mtanzania yeyote kuwatukana, kuwadhihaki au kuwakejeli waasisi wa Taifa letu. Hawa ni watu ambao waliifanyia nchi yetu mambo makubwa,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Mzee Karume yule aliongoza Mapinduzi yaliyoondoa dhuluma na uonevu pale Visiwani. Waafrika walio wengi walikuwa wanaonewa sana pale Tanzania Visiwani, pengine watu wamesahau, lakini hata pale walipokuwa wanashinda uchaguzi, bado walikuwa hawapewi nafasi ya kuongoza maisha yao wenyewe.”
Rais alisisitiza kuwa ni ukosefu wa adabu kwa yeyote kumshutumu mtu aliyejitolea kiasi hicho ili kubadilisha mfumo dhalimu na kujenga maisha na mazingira ya maisha bora kwa wengi.

“Mzee Nyerere yule ametuachia Taifa moja, lililoungana, lenye umoja, lenye amani na mshikamano. Misingi ambayo aliijenga yeye ndiyo imeendelea kuongoza Taifa letu kwa miaka yote hii,” alisema.

Wakati huo huo, Rais Kikwete alipokea rasmi tuzo ya Kiongozi Bora wa Maendeleo Afrika –kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe aliyeipokea kwa niaba yake huko Marekani, Aprili 9, mwaka huu.

Rais Kikwete alisema amepokea tuzo hiyo na amewazawadia Watanzania wote, kwa sababu wao ndiyo waliochangia maendeleo yaliyomwezesha kupata heshima hiyo.

“Napokea Tuzo hii kwa niaba ya Watanzania wote. Aidha, naitoa kwa Watanzania kwa sababu, hata kama nimekuwa kiongozi, ukweli ni kwamba mafanikio na maendeleo yote yaliyopatikana hadi kutunukiwa tuzo hii, yametokana na juhudi zetu za pamoja,” alisema.

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment