WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, April 19, 2014

Rais Kikwete afunguka tena


Rais Jakaya Kikwete  akiwa katika mahojiano maalumu na Mtangazaji Daniel Kalinaki wa Kituo cha Televisheni cha Nation (NTV) kinachomilikiwa na Nation Media Group, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ameendelea kusisitiza kuwa Tume ya Jaji Joseph Warioba haina ushahidi kwamba Watanzania wengi wanataka muundo wa Muungano wa serikali tatu.
Kauli hiyo aliitoa wiki hii jijini Dar es Salaam kwenye mahojiano maalumu na Kituo cha Televisheni cha NTV kilichopo chini ya Nation Media Group (NMG).
Baadhi ya vyombo vingine vya habari vilivyo chini ya NMG ni gazeti hili la Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti kwa upande wa Tanzania, Daily Monitor kwa upande wa Uganda na Daily Nation kwa upande wa Kenya.
Rais Kikwete ambaye moja ya mambo atakayokumbukwa kwenye uongozi wake ni kuasisi mchakato wa Katiba, alizungumzia hoja ya serikali tatu akisema, hakuna ushahidi kwamba Watanzania wengi wanataka muundo wa Muungano wa serikali tatu.
“Hakuna ushahidi kwamba watu wengi katika nchi hii wanataka serikali tatu, hakuna ushahidi wa namna hiyo, hata tume yenyewe haikubaini hicho. Kinachofanywa na vyombo vya habari ni kuandika habari za wajumbe wa Bunge la Katiba wanaotaka serikali tatu, ndiyo kwenye masilahi yao, wanapaza sauti za wale wanaotaka serikali tatu, hao ndiyo sauti zao zinasikika. Lakini hawataki kupaza sauti za wale wanaotaka serikali mbili,” alifafanua.
Hii ni mara ya pili kwa Rais Kikwete kuikosoa ripoti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba. Mara ya kwanza aliikosoa wakati akizindua Bunge la Katiba Machi 21 mjini Dodoma.
Rais Kikwete ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa kipindi cha miaka 10, katika mahojiano hayo alisema katika kuadhimisha miaka 50 ya Muungano, jambo muhimu na kubwa ni kuendelea kuwapo kwa Muungano.
“Tunayo mifano ya nchi zilizojaribu kuungana, lakini zilishindwa, Senegal-Gambia, Ghana-Guinea, Misri na Libya.
“Muungano umeendelea kuwepo kwa nusu ya karne ni mafanikio makubwa. Kumekuwepo na wakati mgumu na changamoto mbalimbali, lakini tumeweza kukabiliana nazo na umeendelea kuwa imara zaidi. Siyo kuendelea kuwepo tu pia umeendelea kuimarika na mchakato wa mabadiliko ya Katiba utaimarisha zaidi Muungano na tutakuwa na Muungano imara baada ya kupata Katiba Mpya,” alifafanua Rais Kikwete.
Akizungumza kwa kujiamini kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu ndani ya CCM na Serikali, Rais Kikwete alisema Muungano ulikotoka ulikuwa imara na umeendelea kukua katika hali ya uimara wake.
“Kuna mambo ambayo tumefanya yamezidi kuimarisha Muungano na umeendelea kuwa na mafanikio makubwa.”
Alisema suala si kuendelea kwa muundo ulivyo sasa, suala la msingi ni kujadili namna ya kutengeneza muundo wa Muungano, kwamba upi ni bora.
Rais Kikwete: “Mimi ni mmoja wa wanaoamini kwamba muundo wa serikali mbili ni bora zaidi kwetu. Siyo suala la kuendeleza hali iliyopo, ni muhimu kubadilika kama kuna sauti zinazotaka kubadilika na pia kama kuna hoja nzito ya kutaka mabadiliko, lakini sioni kama Muungano wa Serikali tatu ni hoja nzito ya kufanya mabadiliko, itasababisha matatizo mengine na mwisho kusababisha muungano kuvunjika.”
Rais Kikwete ambaye katika uzoefu wake wa kazi za kisiasa amewahi kufanya kazi Zanzibar, alisema alipoingia madarakani mwaka 2005 hoja kuu ilikuwa ni kutatua mzozo wa kisiasa uliokuwa ukiendelea kwa muda mrefu kati ya vyama vya CUF na CCM visiwani humo.
Alisema: “Tumeweza kuutatua na sasa tuna Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Kabla ya hapo kulikuwa na matatizo mengi, wakati wa uchaguzi mambo yanatulia, ukimalizika uchaguzi kunazuka matatizo ya kisiasa, tukaamua kuvileta vyama hivi pamoja tukafanya mjadala wa kina na uamuzi uliofikiwa ni kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa, na sasa Zanzibar kuna utulivu wa kisiasa.”
Rais Kikwete akizungumzia suala la Muungano alisema wakati wa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, aliunda tume, Tume ya Shelukindo (iliongozwa na William Shelukindo) kuangalia kero za Muungano na walikuja na kero 31.
Alisema alipoanza kazi mwaka 2006 kero za Muungano zilikuwa zimebaki 13, akashughulikia kero tisa, zimebaki kero nne tu.
Rais Kikwete alisema kimsingi uhuru wa vyombo vya habari kwa Tanzania ni mpana na kwamba hata gazeti lililofungiwa ni moja na mengine yalifungiwa kwa muda tu.
Alisisitiza kwamba habari za kuchochea majeshi kufanya mapinduzi, habari za kuchochea vijana kuleta vurugu hatazivumilia, na kwamba chombo cha habari kitakachojielekeza kwenye habari za namna hiyo kitafungiwa.
“Wakiandika Rais Kikwete nchi imemshinda hainipi tabu, kwa kuwa najua nchi haijanishinda,” alisema Rais Kikwete huku akitoa mfano wa namna redio Mille Collines ya Rwanda ilivyochangia mauaji ya halaiki nchini humo.
Rais Kikwete alitoa mfano mwingine wa namna vyombo vya habari vilivyochangia uvunjaji wa amani ni mwandishi wa habari wa Kenya ambaye amefunguliwa mashtaka ya uhalifu wa kimataifa katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), iliyopo The Hague nchini Uholanzi.
Mwandishi wa habari aliyefunguliwa mashtaka ICC ni mtangazaji wa Kituo cha Redio ya Kass FM, Joshua arap Sang. Rais Kikwete huku akicheka alimuhoji mtangazaji wa NTV “Unataka habari kama hizo tuzivumilie?”
Kuhusu rushwa, Rais Kikwete aliitaja idara ya mahakama kuwa ni moja ya changamoto na wiki iliyopita alizungumza na Jaji Mkuu kuona namna gani wanaweza kuboresha, kuongeza mafunzo kwa wapelelezi au waendesha mashtaka, kutokana na watuhumiwa wengi wa rushwa kuachiwa huru.
Kuhusu uchumi, Rais Kikwete ambaye amewahi kuwa Waziri wa Fedha alisema kinachofanyika ni kuimarisha uchumi mkubwa, na kwa mujibu wa wachumi, uchumi wa nchi ukikua kwa asilimia saba katika kipindi cha miaka 10, pato la taifa huongezeka mara mbili na uchumi wa Tanzania umekuwa ukikua kwa asilimia saba kwa kipindi hicho.
Akizungumzia uhusiano wake na Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais Kikwete alisema hana mgogoro na kiongozi huyo, alichokifanya ni kutoa ushauri kuhusu namna ya kutatua migogoro ndani ya nchi yao, ni hiari yao kufuata ushauri wake

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment