WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, April 18, 2014

SITTA:UKAWA WAJE TUZUNGUMZE

SittaMaalum_6acaa.png

WAJUMBE wa Bunge Maalum la Katiba wanaotoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), waliotoka bungeni juzi jioni wamepanga kufanya mkutano wa hadhara Zanzibar kesho, kwa kile walichodai ni kuwaeleza wananchi ukweli wa mambo yanayojiri katika Bunge linaloendelea hivi sasa.

Ukawa wameamua kuchukua hatua hiyo, huku Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta akisema ofisi yake ipo tayari kwa mazungumzo na wajumbe hao ikiwa ni njia ya kuwezesha mchakato wa kutunga Katiba kuendelea kwa pamoja na kwa amani.
“ Mimi nadhani sababu za kitendo chao walichokifanya jana (juzi) hazitoshi, mlango wangu uko wazi, nimeongea na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na yeye kama kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mlango wake upo wazi kwa mazungumzo,” alisema Sitta jana.(Martha Magessa)

Akizungumza na wajumbe wa Ukawa kwenye ukumbi wa African Dream mjini hapa jana, Mjumbe wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema wameamua kuchukua hatua hiyo ili kuwaeleza ukweli wananchi juu ya mambo yanayoendelea hivi sasa Dodoma.

“Tulitoka jana bungeni kwa sababu hatukuona haja ya kuendelea kuwepo huku lugha zinazotumika ni za matusi, ubaguzi, kejeli na pia Rasimu iliyokuwa ikijadiliwa sio ile ya Tume iliyowasilishwa bungeni,” alisema Lipumba.

Kutokana na hali hiyo, alisema wameamua kwenda Zanzibar kufanya mkutano na wananchi na kuwaeleza hayo ikiwa ni pamoja na kuwaeleza kauli ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uratibu na Bunge, William Lukuvi aliyoitoa hivi karibuni wakati alipokuwa mgeni rasmi katika sherehe za kusimikwa kwa Askofu Joseph wa Kanisa la Methodist mjini hapa.

Alisema wajumbe wote wa Ukawa wasio na dharura watasafiri Jumamosi asubuhi kwenda Zanzibar kushiriki mkutano huo na nia yao ni kutaka Bunge lijadili rasimu ya Katiba mpya iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na sio rasimu ambayo haijawasilishwa na Tume.

Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe alisema Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalum ilikutana jana ambapo yeye alipewa taarifa kuwa ni Kamati ya Uongozi kuhusu Bunge la Bajeti, lakini alipofika ndani alikuta mjadala unaoendelea ni kuhusu Bunge Maalum, aliondoka. 

HABARILEO

No comments:

Post a Comment