WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, April 26, 2014

MAONI: Tuuenzi Muungano kwa vitendo

 
Waasisi wa Muungano Hayati baba wa Taifa Nyerere(kushoto) na Sheikh Abeid Aman Karume(kulia).PICHA|MAKTABA 

Leo ni miaka 50 tangu waasisi wetu, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume   (kwa sasa wote ni marehemu), walipoziunganisha nchi zetu mbili za Jamhuri ya Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mojawapo ya sifa kuu katika kuadhimisha miaka 50 ya Muungano ni kuendelea kuwapo, licha ya changamoto mbalimbali tangu kuasisiwa kwake Aprili 26, 1964 lakini bado umeendelea kuwa imara na hakuna dalili za kuuvunja wala mwenye nia ya kuuvunja Muungano.
Hadi Karume anauawa Aprili 7, 1972 mambo ya Muungano kwa mujibu wa Katiba yalikuwa 11, lakini yalifanyika marekebisho baadaye na hadi Mwalimu Nyerere anaondoka madarakani mwaka 1985, yalikuwa  yamefika 21 kwa mujibu wa Katiba.

Mwaka 1994 kulipozuka kundi la G-55 ndani ya Bunge la Muungano likidai Serikali ya Tanganyika, baada ya Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC), Rais Ali Hassan Mwinyi (kwa wakati huo) aliunda tume iliyoongozwa na William Shelukindo kuchunguza kero za Muungano.

Tume ya Shelukindo ilibaini kero 31 ambazo zilishughulikiwa. Rais Jakaya Kikwete alipoingia madarakani zilikuwa zimebaki kero 13 na ameshughulikia tisa, zimebaki nne na tatu kati ya hizo zinahitaji marekebisho ya Katiba.

Sisi Mwananchi tunasema Serikali imefanya kazi kubwa katika kipindi cha miaka 50, kwanza kuhakikisha Muungano unadumishwa, kushughulikia kero zinazojitokeza na sasa tuna mchakato wa Mabadiliko ya Katiba unaoendelea nchini.

Ni suala lisilopingika kwamba kila jambo lina changamoto zake na sisi tunaamini mjadala unaondelea kuhusu upi ni muundo sahihi wa Muungano ni changamoto ambazo utafika wakati zitakwisha na hatimaye Watanzania watapa kile walichokikusudia.

Siyo nia yetu kuhoji misimamo ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuhusu upi muundo sahihi wa Muungano, lakini hoja yetu kuu ni kuweka dhamira ya pamoja ya kuendelea kudumisha Muungano ambao una umri wa mtu mzima.

Kwa mantiki hiyo wazo lolote la kuvunja Muungano ni kutowatendea haki Watanzania.

Tunapenda kuwasihi wanasiasa kuwa malumbano yanayoendelea sasa ndani ya Bunge la Katiba na nje yasiwe hoja ya kutupeleka kuvunja Muungano, tupambane kwa hoja, lakini tusitupe hoja za wananchi kwa manufaa ya wachache.

Kama waasisi wa Muungano waliendelea kuuboresha ili uwe na tija zaidi kwa wananchi, hakuna sababu ya watu kutoa macho pale maboresho yanapotaka kufanyika kwa lengo la kuimarisha Muungano. 

Sisi wa Mwananchi Communications Limited tunaungana na Watanzania wenzetu katika kusherehekea nusu karne ya umoja wetu kwa kuweka msimamo wetu wazi.

Tunaamini katika kuulinda na kuuimarisha muungano wetu. Tunaamini katika ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda (regional economic integration).

Pia tunaamini katika kuwapa nafasi na sauti wasio na sauti, wanyonge na makundi madogo katika jamii (minorities). Tunaahidi kuendelea kutimiza wajibu wetu wa kutoa nafasi ya mijadala mbalimbali ya kitaifa yenye lengo la kuindeleza nchi yetu, muungano wetu na watu wake kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu. Huu ndiyo mchango wetu na ahadi yetu kwa taifa.

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment