WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, April 26, 2014

JK: Sitaki tena kusikia dawa za kulevya zinapita


Rais Jakaya Kikwete akifurahi muundo wa jengo la tatu la abiria katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana alipokwenda kuweka jiwe la Msingi. 


Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ameagiza kuimarishwa kwa udhibiti katika viwanja vya Ndege vya Kimataifa Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (Kia), kutumiwa kupitisha dawa za kulevya kwenda nje na kuingia nchini.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la tatu la abiria JNIA, Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema hajaridhishwa na kasi ya udhibiti wa dawa za kulevya katika viwanja hivyo.

Alisema inashangaza dawa za kulevya zinapita katika viwanja hivyo na watendaji wote wapo na zinakwenda kukamatiwa Afrika Kusini.

“Sijaridhishwa, unasikia kila siku mtu amekamatwa Afrika Kusini na dawa za kulevya, sijui mwanamuziki gani, siridhishwi hata kidogo,” alisema.

Rais Kikwete alimtaka Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Mhandisi Suleiman Suleiman kuhakikisha mianya hiyo inazibwa vinginevyo ataanza kumwadabisha yeye kisha wengine watafuata... “Nitaanza na wewe mkurugenzi na mwenyekiti wako wa bodi. Mtu anakuja hapa, sijui mwanamuziki gani, mara yoo...yoo... kwa kuwa mnamfahamu anapita, hatuwezi kuwa namna hiyo.”

Aliagiza apewe orodha ya majina ya maofisa wanaodhaniwa kujishughulisha na biashara hiyo naye atawaondoa kwa kuwa sheria inamruhusu... “Rais hashtakiwi, nitawaondoa, nipeni majina kwa kuwa kinachotokea hivi sasa kinaonyesha wote tunafanya biashara ya dawa za kulevya, wengine inatuumiza sana tunaonekana wote ndicho tunachofanya.”

Alibainisha kuwa haingii akilini kusikia kuna kitu kinakwamisha udhibiti wa dawa hizo katika viwanja hivyo ikiwamo Sheria ya Ununuzi wa Umma... “Miaka miwili hiyo sheria gani kwa kitu cha Sh2.5 milioni... je, ingekuwa Sh600 milioni si ndiyo kungegeuzwa gulio?” alihoji.

Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe alifafanua baadaye kuwa Rais alikuwa anazungumzia kuchelewa kufungwa kwa mfumo wa kubaini dawa za kulevya uwanjani hapo, kutokana na mchakato mrefu wa sheria hiyo.
Jengo la abiria

Rais Kikwete alisema atahakikisha Hazina inatoa fedha zinazotakiwa kuharakisha ujenzi wa jengo hilo la abiria ambalo litakuwa na maegesho ya ndege 18 kwa wakati mmoja, litakalohudumia abiria milioni sita kwa mwaka badala ya milioni 2.5 wa sasa.

Mradi huo ambao unatekelezwa na Kampuni ya Ujenzi ya Kimataifa ya BAM ya Uholanzi, utagharimu Sh518 bilioni na Serikali iliahidi kutoa asilimia 50 ya fedha hizo sawa na Sh89 bilioni huku kiasi kingine kikitolewa na Serikali ya Uholanzi.

Hata hivyo, hadi sasa fedha hizo hazijatolewa jambo ambalo liliwahi kulalamikiwa na Mkurugenzi wa TAA kwamba linakwamisha ujenzi huo.

Jengo hilo litakuwa na mifumo yote ya mawasiliano, usalama na uendeshaji na maegesho yenye uwezo wa kuhudumia ndege za aina zote, zikiwamo Airbus 380.
Awali, Suleiman alisema uwanja huo utakamilika kwa wakati kutegemeana na upatikanaji wa fedha na hivyo kuondoa msongamano wa abiria katika uwanja wa sasa (Terminal II) ambao licha ya kuhudumia milioni 2.5, uwezo wake ni kuhudumia abiria milioni 1.2 kwa mwaka.

Kabla ya Rais Kikwete kuzindua ujenzi huo, aliweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili katika eneo la Mloganzila nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza katika eneo hilo, Rais Kikwete aliagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhakikisha inatayarisha haraka iwezekavyo ramani ya ujenzi wa kituo hicho cha mafunzo kwa madaktari kinachotarajiwa kuwa kikubwa zaidi kwa Afrika Mashariki na Kati.

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment